TDMA rudisheni mashindano ya disco taifa

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
AKHLAN wasaalan msomaji wangu wa Jamvi la Kulonga, nianze kwa kukutakia heri ya mwaka 2011, kwa kuweza kuingia kwa kishindo lakini zote zikiwa ni neema zake Muumba wa mbingu na ardhi.

Hili ni Jamvi la Kulonga la kwanza katika mwaka huu mpya ambao nakuahidi kukupa habari motomoto zitakazokuwezesha kufahamu mambo mengi yanayohusu tasnia ya habari za burudani na sanaa kwa ujumla.

Leo katika Jamvi hili nataka nizungumzie kupotea kwa mashindano ya taifa ya disco na uwepo wanenguaji wasiokidhi umri wa miaka 18 kushiriki katika shughuli za unenguaji huku chama cha muziki wa disco Tanzania (TDMA) chenye dhamana ya kuyaandaa kikiwa kimekaa kimya jambo ambalo ni kutowatendea haki wadau wa muziki wa huo.

Katikati ya miaka ya 1980 hadi mwanzoni mwa mwaka 2000 kulikuwa na msisimko wa mashindano ya disco nchini yaliyokuwa yakiandaliwa na Chama cha muziki huo ambayo yaliweza kuibua vipaji vya madansa mbalimbali ambao waliing’arisha Tanzania kimataifa, ingawa wengine waliipa kisogo fani hiyo na kujikita katika uimbaji.

Jamvi la Kulonga linakumbuka mashindano kuwa yaliweza kutengeneza ajira kwa vijana waliokuwa wakishiriki katika mashindano hayo ikiwamo kuitangaza Tanzania kupitia mashindano ambayo yalikuwa yakizihusisha nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Miongoni mwa madansa ambao waling’ara katika mashindano hayo ambao Jamvi hili lilipata bahati ya kuwashudia ni hayati Mussa Simba ‘Black Moses’, Athumani Digadiga, Ally Baucha, Sabah A. Jackson, Super Ngedere, Askof Pompiduu, Bob Rich, Sammy Cool, Maganga Michael Jackson, Cadet Bongoman na Coco Rico ‘Bileku Mpasi’.

Hao ni baadhi tu ya madansa ambao waliweza kuleta ushindani na msisimko katika mashindano mbalimbali yaliyokuwa yakiandaliwa na TDMA chini ya usimamizi madhubuti wa Baraza la Taifa Sanaa Tanzania (BASATA).

Hoja ya Jamvi hili ni kuona tangu mashindano hayo yalipofanyika mara ya mwisho mwaka 2000, hakujawahi kutokea kitu kingine ambacho kinafanana na mashindano hayo zaidi ya kushuhudia kumbi mbalimbali za burudani na baa zikiendesha shoo kwa wanenguaji hao kiholela wakiwa utupu na bila baraka za TDMA na BASATA.

Swali ambalo Jamvi hili linajiuliza, TDMA ipo hai kweli? Na kama jibu ni ndiyo wanafanya nini kuturejeshea mashindano hayo ambayo yalikuwa ni sehemu ya burudani kwa wananchi mbalimbali lakini pia yakiwa ni sehemu ya njia ya kuitangaza Tanzania katika nyanja ya sanaa.

Kubwa la kushangaza ni kuona uongozi wa chama hicho ulio chini ya Mwenyekiti Ibra Radi Washokera, Katibu Mkuu wake, Samwel Semkuruto na Naibu wake, Selemani Mchovu ‘Cisco’ tangu umeingia madarakani kushindwa kuandaa mashindano ya Disco au kusimamia uchezeshwaji holela wa mabinti walio chini ya umri wa miaka 18 katika kumbi na baa mbalimbali nchini.

Pengine tuwaulize wa TDMA tuambieni mmekwama wapi kuturejeshea mashindano yetu ambayo yalikuwa yakijaza mamia ya watu katika kumbi za Lang’ata, Kinondoni, Magomeni kwa Macheni, Sweet Corner, Madoto na Vijana Social Hall jijini Dar es Salaam, wakati Morogoro ilikuwa ni Mango Garden na Kaumba wakati Mwanza ni Deluxe.

Mashindano ya disco nchini yalikuwa yakifanyika kuanzia mikoani na hatimaye fainali zake kufanyika jijini na kupatikana bingwa ambaye alikuwa akiiwakilisha Tanzania katika mashindano ya ukanda wa Afrika Mashariki ambapo kwa miaka kadhaa nchi iliweza kutangazika nje ya mipaka kupitia madansa hao.

Jamvi la Kulonga linahoji, nini kinakwamisha mashindano hayo yasifanyike ikiwa viongozi hao wapo madarakani muda mrefu na wameshindwa kutangaza mipango waliyonayo katika kurudisha hadhi ya mashindano hayo na chama kwa ujumla.

Lakini pia TDMA imekuwa kimya ikipuuzia madisco yanayopigwa mitaani kiholela na shoo zinazofanywa na wanenguaji walio chini ya umri huo ingawa bado suala hili linaigusa pia na BASATA katika kusimamia maadili.

Katika siku za hivi karibuni kumeibuka uyoga wa madisco mitaani ambayo yanapiga muziki na kutumia wanenguaji wasiokidhi umri husika, jambo ambalo ni kwenda kinyume na taratibu zinazokiongoza chama hicho na BASATA kwa ujumla.

Jamvi hili linakumbuka miaka ya nyuma maofisa wa TDMA walikuwa wakihangaika huku na kule hadi usiku wa manane kuingia katika kumbi za burudani kukagua vibali vya kupiga disco, jambo lililokisaidia chama hicho kujiongezea kipato na pia kusimamia maadili ya shoo hizo ili kuepuka vijana walio chini ya umri huo kujiingiza katika unenguaji.

Lakini hali imekuwa tofauti hakuna kinachofanyika ndani ya TDMA kutokana na viongozi wake kukaa kimya bila kuanika mipango waliyonayo katika kukiendeleza chama na kurudisha hadhi ya muziki wa disco.

Jamvi hili linapata wasiwasi pengine chama hiki hakipo katika orodha ya vyama wanachama wa BASATA ambao wanapaswa kuwasilisha kalenda yao inayoonyesha mipango yao ya mwaka mzima ili wadau na wapenzi mbalimbali wa mashindano ya gisco waweze kujitolea kuyaandaa iwapo chama kinakabiliwa na ukata.

Ni wakati wa BASATA kuanza kuvikagua vyama vyake kuona vinatekeleza vipi majukumu kwa wanachama wao ambao wanahitaji kuona wanatekeleza kile ambacho wametumwa na watu waliowachagua, lakini pia ikiwezekana kuvifutia uanachama kwa kushindwa kuwajibika kwa wanachama wao.

Kwa leo nalikunja Jamvi nikikusihi tuwasiliane Ijumaa ijayo kwa habari zaidi za burudani na sanaa.
 
Back
Top Bottom