Tatizo kubwa kwenye filamu zetu ni kukosa waongozaji

M'bongo

JF-Expert Member
Apr 20, 2011
265
298
Imeandikwa na Bishop J. Hiluka

Msomaji mmoja wa makala zangu alinitumia ujumbe kupitia baruapepe
akitaka kujua mtazamo wangu kuhusu mapungufu yaliyopo katika filamu
za Kibongo, huku yeye akitupia lawama moja kwa moja kwa waigizaji na
waandishi wa muswaada andishi (scriptwriters) kwa kutokuwa na uwezo.


Msomaji huyo aliyejitambulisha kwa jina la Masengwa, mkazi wa Kazima,
Tabora alisema kuwa waigizaji wengi wa filamu za Kibongo wamekuwa
wanashindwa kabisa kuuvaa uhalisia wanapoigiza! Akitolea mfano wa filamu
moja (anaitaja jina) ambapo ilionekana mwigizaji akiigiza analia lakini uso wake
ulikuwa umebeba tabasamu la chati! Na kuongeza kuwa, kwenye filamu zetu si
ajabu kuona tukio la utekaji nyara katika filamu huku mtekwaji akionesha dalili
zote za kukaa tayari kwa kutekwa!


Msomaji huyo pia alitaka kujua nini maoni yangu kuhusu uandishi mbovu wa
miongozo ya filamu hasa kwa kuwa mimi mwenyewe ninajitambulisha kama
mmoja wa waandishi, ingawa yeye hakuficha hisia zake kwa kusema kuwa
uandishi limekuwa tatizo kubwa kwenye filamu zetu, akisema kuwa stori mbovu
kamwe haiwezi kutoa filamu nzuri hata kama wachezaji wa filamu hiyo watakuwa
ni magwiji wa filamu kutoka Hollywood!


Nakubaliana naye kwa kiasi fulani japo mimi ninaweza kuwa na mtazamo tofauti
kidogo. Kwa kifupi mimi hupenda kuiangalia filamu na kuupima uzuri wake kwa
kuangalia mambo makuu matano: Mwongozo mzuri (script), Waigizaji wazuri,
Wapigapicha wazuri, Muongozaji mzuri na Mhariri mzuri.


Naamini kuwa mwongozo mzuri wa filamu ni sawa na msingi imara wa nyumba
unaotokana na ramani nzuri (stori). Kama mwongozo hautakuwa mzuri naamini
hata filamu haiwezi kuwa nzuri kabisa, hii inamaanisha kuwa kwa script mbovu
hata ukimleta Denzel Washington hawezi kucheza katika kiwango tulichozoea
kumuona akicheza.


Waigizaji ni sawa na matofali yanayotumika katika ujenzi wa nyumba, huku
wapigapicha nikiwafananisha na simenti na maji kwa ajili ya kujengea nyumba.
Muongozaji ndiye fundi mjenzi, anayepaswa kuchanganya vizuri simenti, maji
na mchanga ili kupata kile kinachotakiwa, hivyo bila kuwa makini nyumba haiwezi
kuwa imara.


Bahati nzuri tasnia yetu imebarikiwa kuwa na waigizaji wengi wazuri, wapigapicha
wengi wazuri na hata wahariri wengi wazuri, lakini inakosa waandishi wazuri wa
script na waongozaji wazuri wa filamu.


Hii haimaanishi kuwa hakuna kabisa waandishi au waongozaaji wazuri hapa
nchini, wapo wengi tu wenye uzoefu na elimu ya kutosha katika uandishi na
uongozaji wa filamu, tatizo ni mfumo uliopo unaowafanya kutupwa nje ya ulingo
wa soko la filamu kwa kuwa hawathaminiki, hawatumiki wala hawapewi heshima
inayostahili.


Ile hoja ya kuwa uandishi wa script ni tatizo kubwa kwenye filamu zetu, ina
mantiki hasa kwa kuwa mwongozo wa filamu ni moja ya vipengele muhimu sana
katika uandaaji wa filamu na michezo ya kuigiza na dhana ya kuwa script ni
hatua ya mwanzo, ni ramani ya kutuongoza kutoka kwenye wazo (concept)
hadi kazi inapokamilika (final edit).


Lakini watazamaji walio wengi hukimbilia kumlaumu mwandishi wa script pindi
filamu inapokuwa mbaya, ikisababishwa na kutoelewa nani hasa mwenye jukumu
la kuhakikisha filamu inakuwa nzuri. Hapa ndipo script inapokuwa chanzo cha
mahusiano mabaya (a hate relationship) kati ya mwandishi na muongozaji wa filamu.

Uhusiano mbaya huja pale muongozaji wa filamu anapoamua kubadili baadhi ya
matukio ndani ya script, wakati mwingine hubadili sehemu kubwa ya script bila
hata kumshirikisha mwandishi na hivyo kuvuruga mtiririko mzima wa stori. Kitendo
hiki kinaweza kusababisha kuzalishwa hadithi tofauti kabisa na iliyoandikwa
mwanzo ingawa jina la mwandishi litabaki lilelile. Haya yamekuwa yakitokea sana,
binafsi yamenikuta na nimeshawahi kushuhudia yakitokea hata kwa waandishi na
waongozaji wakubwa duniani.

Mwandishi ndiye mtu wa kwanza anayeiona sinema wakati akiandika, muongozaji
huiona pale anapopitia script ili kuongoza upigaji picha (shooting). Tatizo linakuja
pale muongozaji anapoiona kwa jicho tofauti. Filamu ikiwa mbaya lawama
humwangukia mwandishi kama ambavyo msomaji ameelekeza lawama zake.


Kwa kawaida filamu ni zao la muongozaji na wala si la mtayarishaji, mwandishi
au muigizaji kama ambavyo wengine wanadhani. Katika makala ya leo nitajaribu
kujikita zaidi katika kumwangalia muongozaji wa filamu na mchango wake katika
kufanikisha kazi nzima.


Hoja ya kwamba waongozaji wa filamu za Kibongo hawakusoma ndiyo maana
wanashindwa kuongoza inaweza isiwe sababu ya msingi, kwani hata Hollywood
kuna waongozaji ambao hawakusoma kabisa lakini bado wamekuwa waongozaji
wazuri na wanaoheshimika sana duniani.


Waongozaji ambao hawakwenda shule ni pamoja na; Steven Soderbergh,
Robert Rodriguez, Quentin Tarantino, Richard Linklater, Spike Jonze...


Muongozaji wa filamu anapaswa kuwa mbunifu na kiungo muhimu kati yake na
timu ya uzalishaji. Muongozaji anawajibika katika kutafsiri script iliyoandikwa
kwenye karatasi na kuihamishia katika picha halisi na sauti kwenye skrini – na
anapaswa kuiona taswira halisi na kutafsiri mtindo na muundo wa filamu, na hivyo
kufanya kazi zote mbili kama kiongozi wa timu na msimulizi kwa kutoa picha halisi.


Tatizo kubwa lililopo kwenye tasnia ya filamu hapa Tanzania ni kwa waongozaji
wetu wa filamu kudhani kuwa kazi ya uongozaji wa filamu ni kujua: "standby...
action... cut!
" na kusahau kuwa muongozaji ndiye anayepaswa kumtengeneza
mhusika kwa kutegemea muongozo unasemaje. Kama muigizaji atashindwa kuvaa
uhalisia, hilo sio kosa lake ni kosa la muongozaji na hutafsiri uwezo wa muongozaji
ulipokomea.


Binafsi siwezi kumlaumu muigizaji anapochemsha, huwa namtupia lawama
muongozaji wa filamu, kama muongozaji ni mzuri hawezi kukubali kuona muigizaji
anashindwa kuvaa uhalisia kwa kuwa atamharibia kazi.


Nimewahi kuwauliza baadhi ya watazamaji wa filamu za nje (Hollywood au Bollywood)
kuwa ukiona filamu ambayo mhusika mkuu ni mtoto mdogo, ambaye amefanikiwa
sana kuvaa uhalisia kiasi kwamba unaweza kudhani hakuwa akiigiza, ina maanisha
nini, ana akili nyingi kuwazidi watu wazima waliopo kwetu?


Kwa swali hilo utagundua kuwa muongozaji kafanikiwa kumtengeneza, kitu ambacho
kinakosekana kwa waongozaji wetu wanaodhani ukijua kusema "action... cut..."
utakuwa umefuzu kuwa muongozaji wa filamu.


Muongozaji anapaswa kuwa na uelewa mkubwa katika kuitafsiri script na
kuihamishia katika picha halisi na hata kupendekeza sauti zitakazotumika
kwenye skrini, pia anapaswa kuangalia mtu anayefaa kuigiza, ndiyo maana
mojawapo ya majukumu ya muongozaji ni pamoja na kufanya usaili (casting).


Wakati masuala muhimu katika utayarishaji wa filamu, kama vile fedha na masoko,
hubakia mikononi mwa Mtayarishaji wa filamu (producer), Muongozaji anapaswa
pia kuwa na ufahamu wa bajeti inayotumika kwenye filamu anayoiongoza na kujua
ratiba. Katika baadhi ya filamu, Waongozaji huhodhi majukumu mengi kama
Muongozaji/Mtayarishaji au Muongozaji/Mwandishi, jambo ambalo halikatazwi
kama atakuwa na uwezo wa kuyatenda kwa ufanisi.


Sifa nyingine ya mtu kuwa muongozaji wa filamu ni kuwa na uelewa wa kina
wa jinsi sinema inavyotengenezwa, kuwa na ubunifu mkubwa (creative vision),
ufahamu wa namna ya kuandika script na kujitoa kwa dhati (commitment) katika
kufanikisha. Muongozaji anahusika moja kwa moja kwenye mafanikio yoyote ya
kisanii, mafanikio ya kibiashara au kushindwa kwa filamu katika soko.


Muongozaji anaweza kuandika script ya filamu au kusimamia uandikwaji baada
ya rasimu ya awali ya script kukamilika. Baada ya kupata waigizaji, muongozaji
husimamia mazoezi (rehearsals) na upigaji picha wa filamu (shooting). Muongozaji
pia anapaswa kusimamia masuala ya kiufundi ya sinema, ikiwa ni pamoja na
kamera, sauti, taa, ubunifu na kadhalika.


Wakati wa uhalili (post-production), Muongozaji hufanya kazi kwa ukaribu na
Wahariri katika mchakato wa kiufundi wa uhariri, hadi kufikia mwisho wa kazi.
Katika hatua zote, Muongozaji anawajibika kuhamasisha timu yake kutayarisha
kazi bora. Muongozaji pia anapaswa kuyafahamu mahitaji na matarajio ya soko
la filamu.


Mwisho, muongozaji awe na uwezo wa kufanya mawasiliano (communication skills)
na watu wengine katika kufanikisha.

SOURCE: Mwanaharakati

 
  • Thanks
Reactions: 3D.
Wana JF, huyu Bishop Hiluka katuletea kitu kingine kipya ambacho
tunapaswa tukijadili kwa maendeleo ya tasnia ya filamu. Binafsi napenda
sana kusoma makala zake zinazoelimisha na kueleza mustakabali wa tasnia
ya filamu hapa nchini ingawa bado naona kuna giza nene kwenye tasnia hii.
 
Ni kweli M'bongo, mimi ni mtazamaji mkubwa wa sinema za Kitanzania
lakini nimekuwa nakatishwa tamaa sana, bahati mbaya kwa kuwa mimi
si mtaalamu kama Bishop Hiluka, sikujua kama tatizo ni waongozaji, bali
nilikuwa nikiwatupia lawama waigizaji na waandishi wa script.
Big up Bishop Hiluka
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom