TASNIA YA FILAMU: Tuhuma za Steps kuwagawa wasanii na utetezi dhaifu!

WISDOM SEEDS

JF-Expert Member
Jun 1, 2011
841
282
Makala hii imeandikwa na Bishop J. Hiluka kwenye gazeti la KULIKONI
leo JUNI 3, 2011


SIKU zote naamini kuwa penye ukweli uongo hujitenga. Jumamosi iliyopita,
katika kipindi cha Baragumu kinachorushwa asubuhi kwenye moja ya vituo
vyetu vya televisheni kulikuwa na mada inayozungumzia changamoto zinazoigusa
tasnia ya filamu Tanzania, ambapo kampuni ya usambazaji wa filamu ya
Steps Entertainment
ilimtuma mwakilishi wake, anayejiita Kambarage, kujibu
baadhi ya tuhuma zinazoikabili kampuni hiyo.



Kwa kweli sikutegemea kwa kampuni kubwa inayoaminika kuwa na watu makini
kama Steps Entertainment kuwakilishwa na msemaji wa aina ile aliyeishia kujisifia
kwa kusafiri kwenda Kenya, Burundi, Rwanda na Kongo, lakini akionekana kutojua
mambo mengi kwa jinsi alivyokuwa akibabaika kujieleza, japo mwendeshaji wa kipindi,
Fred Mwanjala alionekana kumuuliza maswali ya kumbeba.



Nilimsikia Kambarage akikanusha kuwa kampuni yao haihusiki na mgawanyiko
uliopo wa wasanii, alikanusha vikali kuhusu kampuni yao kuchochea mgawanyiko
baina ya Shirikisho la Filamu (TAFF) na wasanii waliounda Bongo Movie Club, lakini
hapohapo akageuka kuwa msemaji wa Bongo Movie Club kitendo kilichoonesha
kujichanganya mwenyewe.



Pia madai kwamba mikataba wanayoingia na wasanii inawakataza kufanya kazi na
watu wengine, msemaji huyo alijichanganya pia, kwa kudai kuwa si kweli ingawa alikiri
kuwa mikataba wanayoingia wasanii na kampuni hiyo ina masharti magumu ambayo si
rahisi kwa wasanii kufanya kazi na watu wengine! Eti kwa kuwa Steps ndiyo wanagharimia
pesa (Executive Producer) za kufanyia kazi.



Akijibu tuhuma kuwa kampuni yao inawabagua wasanii wengine alisema kuwa wao kama
wafanyabiashara huangalia zaidi biashara kwa kuchagua filamu nzuri inayouza kwa maana
ya hadithi (maudhui) na yenye ubora, na kwamba kampuni yao ina watu makini wanaoangalia
filamu kabla hazijatoka wakikazia zaidi kuangalia maadili na maudhui.



Jambo la kushangaza ni kwamba kama kweli wanaangalia maadili na maudhui inakuwaje
sinema wanazosambaza ndizo zinazolalamikiwa kwa kukosa maadili na kuwa na maudhui
mabaya? Ni watu wa aina gani ambao kampuni hiyo inawatumia kukagua sinema hizo?
Je, vipi kuhusu weledi wao katika masuala yanayohusu filamu? Haya ni mambo yanayopaswa
kujibiwa na mtu makini lakini si msemaji aliyetumwa siku hiyo.



Ni jambo zuri kwa kampuni ya usambazaji kuamua kuzikagua filamu zake kabla
hazijaingia dukani hasa kwa kuwa Bodi ya Ukaguzi wa Filamu imeonekana kulala usingizi,
lakini kwa jinsi nijuavyo kampuni hiyo haina watu weledi wa kukagua maadili na hata maudhui
ya hadithi zenyewe. Kinachoangaliwa zaidi ni sinema kacheza nani, au imetayarishwa na nani basi.



Msemaji wa steps pia aliendelea kujichanganya pale aliposema kuwa kampuni yao
inazipanga sinema katika madaraja (akitumia neno la Kiingereza 'class') kulingana na
umaarufu wa wasanii, hii inamaanisha kuwa wao hawaangalii ubora wa kazi husika bali ustaa!
Pia alinishangaza pale aliposisitiza kuwa eti wasanii wachanga wanaibuliwa na kina Kanumba
akitolea mfano wa muigizaji mdogo, Jennifer aliyeibuliwa kwenye filamu ya This Is It!



Ina maana kuibua vipaji vipya ni hadi wasanii hao washirikishwe na Kanumba, Ray na
wengineo waliopo kwenye lebo ya Steps? Kama huo si ubaguzi basi ni nini? Kwao Steps,
sinema nzuri ni ile inayoandaliwa na wasanii wanaowaita wakubwa, basi huipitisha moja kwa moja.



Kuna ushahidi wa kutosha kuwa watu wengi wamekataliwa sinema zao kwa kuwa tu
hazikuwashirikisha wasanii wakubwa, na hata alipotakiwa kujibu msemaji huyo alijitetea
kuwa sinema nyingi wanazozikataa huwapa ushauri watayarishaji wake namna ya kuziboresha,
jambo ambalo sio kweli. Ushauri ambao mara zote wanautoa huwa ni kuwataka wawatumie
wasanii maarufu japo kwenye scene moja au mbili ili sinema hizo zipate nafasi hapo Steps,
kitu ambacho hakiendani na taaluma ya tasnia ya sinema.



Hata ile hoja kwamba wanasambaza sinema za wengine, akitolea mfano sinema ya
White Chair
bado ni hoja dhaifu sana, kwani sinema hiyo pia ilipewa sharti la kumtumia
japo msanii mmoja anayeaminika kuuza wa lebo hiyo. Na ndipo mtayarishaji wa sinema hiyo
alipolazimika kuingiza scene mpya na kumtafuta msanii Issa Mussa maarufu kama Claude
na kumchezesha kwenye scene moja tu ya kwanza.



Pia ieleweke kuwa sinema yoyote isiyokuwa na wanaodaiwa kuwa 'mastaa wanaouza'
ikiwemo hiyo ya White Chair, japo ilimchezesha Claude zimewekewa masharti magumu
ikiwa ni pamoja na kulipwa pesa kiduchu, kiasi ambacho ni aibu hata kukitaja.



Msemaji wa Steps pia hakuona aibu kuudanganya umma wa Watanzania kuwa kampuni
ya Steps imemleta mtengeneza filamu, John Riber kutoka Zimbabwe kufanya kazi na Steps.
Ukweli ni kwamba John Riber na mwanaye, Jordan Riber si Wazimbabwe na wala hawaishi
Zimbabwe bali ni raia wa Marekani wanaoishi na kufanyia kazi zao jijini Dar es Salaam.



John Riber ana kampuni inayoitwa Media for Development International (MFDI), yenye maskani
yake barabara ya Kimweri, Msasani jijini Dar es Salaam, akiwa anaishi nchini tangu 2004,
akitokea Zimbabwe alikoishi kuanzia 1987. Kazi alizotengeneza John Riber ni pamoja na Chumo
(2011), Mwamba Ngoma (2009), Yellow Card (2000), Everyone's Child (1996), More Time (1994)
na Neria (1993). Pia ndiye producer wa kipindi maarufu cha redio cha Wahapahapa.



Suala la usambazaji wa filamu nchini ni jambo linaloumiza sana kichwa, biashara hii imejengewa
mazingira ya kuwa ngumu kuliko biashara nyingine yoyote. Watayarishaji wa filamu wengi ambao
wamekuwa wakipeleka kazi zao Steps, kazi ambazo ni nzuri kwa maana ya ubora wa picha na maudhui
yanayozingatia mazingira, tamaduni na hali halisi, hujikuta wakikwamishwa na kazi zao kukataliwa kwa
sababu tu hawakuwachezesha wasanii ambao ni "lebo" ya msambazaji.



Kampuni ya Steps ndiyo iliyokuja na wazo la kuwalazimisha watayarishaji wa filamu
kutengeneza sinema yenye sehemu mbili, maarufu kama Part 1 na 2 hata kama hadithi
hairuhusu, kitu ambacho si haki kabisa na kinyume cha taaluma husika.



Kulazimisha sinema iwe na namba moja na mbili kunasababisha kuoneshwa kipande kimoja
cha mtu kwa zaidi ya dakika tano akifanya tukio moja, jambo ambalo limekuwa likiwakera
watazamaji badala ya kuwaburudisha na kuwaelimisha kama ilivyo dhana nzima ya filamu na
uigizaji.



Hata ile hoja kwamba bila wasanii au majina makubwa sinema haiwezi kufanya vizuri sokoni
haina mantiki yoyote na ina lengo la kuwakweza watu fulani. Kama ingekuwa kweli kwa nini
filamu za hao wanaouza zinafanyiwa promosheni kubwa sana, kuanzia kwenye magazeti,
mabango makubwa ya barabarani, magari ya matangazo, hadi kwenye vituo vya redio na
televisheni, huku wengine wakiwa hawapati kabisa fursa hiyo ya kutangaziwa kazi zao!



Pia mwakilishi wa Steps aliwaponda wanaodai kwamba kampuni yao iliamua kushusha bei
ya mauzo ya DVD na VCD kutoka wastani wa sh. 5000 hadi 1,500 ili kuwaua wasambazaji
wengine wadogo (jambo ambalo wamefanikiwa), akidai kuwa walishusha bei ili kupambana
na wezi wa filamu (pirates).



Madai yake yaliyosisitizwa na kauli kwamba wanachopata ni faida ya shilingi 100 tu kwa
kila nakala, lakini akashindwa kufafanua kuwa kwa kampuni kubwa kama Steps yenye
uwezo wa kuagiza DVD tupu nje (ingawa hazina ubora), yenye mitambo ya kudurufu (dubbing)
kazi zake na hata kazi za wengine, inapata faida ya shilingi 100, hawa wasambazaji wengine
wanaotegemea kununua DVD tupu kutoka kwao na kufanyiwa dubbing watamudu vipi soko?



Pia mwakilishi huyo hakujibu madai kwamba kampuni yao inatumia mwanya wa filamu
inazoziuza kwa bei ndogo kwa kuwa inapata faida kwa matangazo yake ya biashara
yaliyomo ndani ya filamu hizo, kama vile pikipiki, set za Tv na bidhaa zingine ambayo hata
hivyo hayalipiwi kodi!



Katika suala la kununua hakimiliki za wasanii na watayarishaji, mwakilishi huyo alishindwa
kabisa kujibu tuhuma za kununua hakimiliki za wasanii kwa kuwasainisha mikataba
inayokiuka sheria za hakimiliki, hata pale alipoonekana kusaidiwa kujibu na mwendesha
kipindi, Fred Mwanjala. Sidhani kama kweli mwakilishi huyo anaelewa maana ya
Intellectual Property.



Katika kipindi cha karibuni kumekuwepo ongezeko la wimbi la kupeleka filamu za
Kitanzania kwenye vituo vya televisheni ili zioneshwe. Vituo vya televisheni vya hapa
nchini siku hizi vinaonesha filamu za Kitanzania, jambo ambalo ni zuri lakini bado lina utata.
Utata huu unatokana na kuwa filamu hizo zinapelekwa huko na kampuni inayozisambaza
filamu hizo kutokana na tatizo kubwa la kutokuwa na mikataba sahihi au kutambua maana ya
intellectual property.



Msambazaji kazi yake ni kusambaza kazi, na hivyo mkataba wake unatakiwa umruhusu
kwa kazi ya usambazaji tu. Haki za kurusha au kuonesha kazi zinatakiwa zibaki kwa mwenye
filamu ili aweze kufaidika tena kutokana na kurusha hewani kazi hizo, na si kama inavyofanyika
hapa kwetu.



Jana, Alhamisi niliitwa kwenye kikao cha Kamatikazi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
ambao wanaangalia jinsi ya kuiokoa tasnia hii kwa kuangalia miundo ya soko letu na kulifanya
Taifa lipate mapato yatokanayo na kazi za sanaa, ikiwemo kuangalia suala la intellectual property.



Hivyo naamini kuwa haki ya mtu haitapotea hata kama utatungwa uongo wa aina gani, na hakuna
marefu yasiyo na ncha. Hivi sasa mwanga wa haki unaanza kuonekana na siku za karibuni haki itajidhihirisha.



Naomba kutoka hoja.

Bishop Hiluka ni mtafiti wa masuala ya filamu,
mwandishi wa miongozo ya filamu (script) na muongozaji sinema.


SOURCE: Gazeti la Kulikoni, lakini pia inapatikana HAPA
 
I see umeanzisha mada nzuri saana ambayo wadau tunapaswa tuchanagie, mimi pia nimeisoma
makala hii kwenye gazeti leo asubuhi ingawa hata huapa JF nimeirudia tena.

Mi' nadhani hapa kuna matatizo sehemu zote mbili, watayalishaji wa filamu nchini hasa hao
wanaojiita "masupastaa" wamekosa kabisa mafunzo ya msingi (nitty-gritty) ya namna ya
kutengeneza kazi zao katika kiwango kinachokubalika japo wanabebwa na msambazaji.


Pia ubinafsi katika tasnia hii umechangia kwa kiasi kikubwa sana na kufanya filamu zetu
kuwa si kitu kinachozingatia au kuhitaji taaluma yoyote. Watu wanalipua kazi na wanafanya
mambo bila kuzingatia utaalam. Wanafanya mambo ili mradi wanajua watauza (yupo anayewabeba)
na kupata pesa, basi.


Ubinafsi huu umekuwa ni sababu kubwa ya kuufanya uwanja wa filamu wa Tanzania kuwa sehemu
inayoongoza kwa kutokuwa na mgawanyo wa majukumu. Si ajabu kukuta mkurugenzi wa kampuni
ya kutengeneza filamu, ndiye aliyeandika skripti, ndiye muongozaji mkuu, ndiye muigizaji mkuu,
ndiye mhariri na kadhalika.


Pia Serikali kwa upande wake inapaswa kuwa wakala wa kusaidia masoko yaweze kufikia
kwenye "ubora" unaotakiwa na binafsi nimekuwa nikitegemea kuona serikali ikianzisha sera "bora"
na makini kwa kutuanzishia chombo maalum kitakachokuwa na uwezo wa kuzitangaza kazi zetu.



Vinginevyo wataalam kama huyu Bishop na wengine wataendelea kulalamika tu huku soko
likizidi kudodora.

Huo ndiyo mchango wangu
 
Kinacholeta ukakasi zaidi ni kwamba,kwa sasa kuna Shirikisho la Filamu linalounganisha wasanii wote na kutambuliwa kisheria lakini hawa supastaaz wamejitenga na kuanzisha kitu kinachoitwa Bongo Movie Club na kinadhaminiwa na Steps haohao.Ni ujinga walionao wasanii wetu.Wanakubali kugawanywa na msambazaji ili awanyonye.Hawajali kwamba chini ya Umoja wao katika shirikisho wangeweza kufika mbali kwa kupanga mikakati mizito ambayo itawainua.

Ni jambo la ajabu sana kwamba, wasanii wa filamu wanaanzisha umoja wa kucheza soka tena wakijitenga na wenzao kwa kile kinachoonesha kwamba ni ubinafsi mtupu.

Wasanii wetu wanatakiwa kukuna vichwa sana na kubadilika kwani huko tuendako watakosa watetezi kabisa kwa sababu hawapendani na ni wabinafsi + wanafiki wakubwa.
 
ndo maana hawatatoka watabaki kuendesha magari ya kifahari na kutembea na wanawake warembo na starehe kwa wingiiii plus mabichwa kuwa makubwaaaa,
 
Kinacholeta ukakasi zaidi ni kwamba,kwa sasa kuna Shirikisho la Filamu linalounganisha wasanii wote na kutambuliwa kisheria lakini hawa supastaaz wamejitenga na kuanzisha kitu kinachoitwa Bongo Movie Club na kinadhaminiwa na Steps haohao.Ni ujinga walionao wasanii wetu.Wanakubali kugawanywa na msambazaji ili awanyonye.Hawajali kwamba chini ya Umoja wao katika shirikisho wangeweza kufika mbali kwa kupanga mikakati mizito ambayo itawainua.

Ni jambo la ajabu sana kwamba, wasanii wa filamu wanaanzisha umoja wa kucheza soka tena wakijitenga na wenzao kwa kile kinachoonesha kwamba ni ubinafsi mtupu.

Wasanii wetu wanatakiwa kukuna vichwa sana na kubadilika kwani huko tuendako watakosa watetezi kabisa kwa sababu hawapendani na ni wabinafsi + wanafiki wakubwa.

Ni kweli, hapa ndipo kwenye tatizo na kwa kuwa Steps wamegundua kuwa upeo wa watu hawa ni mdogo
ndiyo maana wakatumia ile falsafa ya 'divide and rule' ili waendelee kuchuma. Wanadhani kuendesha Harrier
ni bora zaidi kuliko hizo haki wanazokosa.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom