wanasema kulindana pia ahadi hewa za viongozi navyo vinachangia kwa kiasi kikubwa kutoisha kwa matatizo yetu.
Makala -Tuna watu, ardhi, siasa safi, kwanini hatuendelei?
Tuna watu, ardhi, siasa safi, kwanini hatuendelei?
Osoro Nyawangah
TAKRIBAN miaka 45 sasa baada ya Jamhuri ya Tanzania kujitawala kutoka katika minyororo ya wakoloni, bado taifa hili lililojaliwa kuwa na akiba kubwa ya rasilimali nyingi na za kuvutia linaendelea kulia kilio cha umaskini uliokithiri miongoni wa jamii, licha ya kuwapo mikakati mingi ya kupambana na umaskini huo.
Katika mahojiano na baadhi ya wananchi, wapo ambao tayari wamekwisha kukata tamaa kuwa serikali yetu imeshindwa kabisa kupambana na umaskini na matokeo yake imeamua kuwaacha wananchi wapambane na adui huyo kwa mbinu na staili binafsi.
Lengo kuu la kupambana na wakoloni katika nchi nyingi za Kiafrika ilikuwa kuwawezesha wazawa kukamata hatamu za uongozi ili kuweza kuongeza kasi ya kujenga uchumi wa taifa ili wazawa waweze kufaidika na maliasili na rasilimali za taifa walizopewa na Mungu.
Mara baada ya kupata uhuru, Tanzania chini ya uongozi shupavu wa Mwalimu Julius Nyerere, ilitangaza vita kabambe dhidi ya maadui watatu wakuu wa taifa hili ambao ni ujinga, maradhi na umaskini, maadui ambao hata leo hii hakuna dalili ya kuonyesha kuwapo na mafanikio ya kuwashinda.
Kumekuwapo maazimio mengi yaliyotangazwa na taifa kupitia Chama cha TANU na ASP, na baadaye Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambayo yalilenga kuleta msukumo na mbinu mpya za kupambana na maadui hao watatu ili kuwajengea wananchi wetu angalau ahueni ya maisha ili nao wafurahie matunda ya uhuru.
Azimio la Arusha, Azimio la Musoma, Azimio la Iringa, Azimio la Zanzibar na milolongo mingine ya maazimio yaliyolenga kwa dhati kulikwamua taifa hili ndani ya lindi la umaskini, maradhi na ujinga, hadi leo kuna watu wanaishi katika taifa hili wakiwa hawana fedha za kujinunulia hata mlo mmoja wa chakula kwa siku, hawajui kusoma na kuandika licha ya kuwapo utitiri wa shule za msingi za bure na wengine wengi wanapoteza maisha kutokana na maradhi yenye kinga na tiba.
Nyerere katika moja ya hotuba zake ambazo kwa kiasi kikubwa zilitoa dira ya uongozi wa taifa, aliwahi kusema ili taifa liendelee, linahitaji mambo makuu manne: Watu, ardhi siasa safi na uongozi bora.
Tanzania kama moja ya mataifa barani Afrika, tumejaliwa kuwa na watu wengi wenye nguvu na ari kubwa ya kufanya kazi, tuna ardhi kubwa na yenye rutuba nyingi ambayo hadi sasa kuna maeneo ambayo hayajawahi kulimwa na mtu yeyote licha ya kukanyagwa, kila baada ya miaka mitano tunaendesha uchaguzi wa kuwapata viongozi bora,
kutokana na uchaguzi huru na wa haki, kila mara na chama kinachoongoza taifa hili ni kile kile ambacho kila siku kinajinadi kwa kuwa na sera na siasa safi, je, falsafa hii ya Nyerere ina kasoro?
Mbona tuna vitu hivyo vyote ambavyo ni muhimu kwa taifa kuendelea lakini bado wananchi wetu wanaendelea kuimba wimbo usio na muitikiaji wa umaskini uliokithiri?
Mbona watu wetu wanaendelea kufa kutokana na maambukizi ya malaria, homa ya matumbo na utapiamlo? Kwa nini bado tuna asilimia kubwa ya wananchi wasiojua kusoma, kuhesabu na kuandika?
Hapa ndipo tunapata changamoto ya kutaka kujua kile kinachotukwaza katika kupiga hatua madhubuti za maendeleo. Licha ya kuwa na vitu hivyo muhimu, hapa ndipo inapofikia wakati tunataka kuuliza uhalali wa siasa na sera zinazotuongoza na uhalali wa viongozi tulionao.
Kwa mtazamo wangu, taifa hili haliwezi kuendelea endapo tutaendekeza uongozi wa kulindana katika nyanja mbalimbali za uongozi, hatutaendelea endapo tutaendekeza viongozi wanaoendeleza blabla na propaganda za siasa za umimi na kujitafutia umaarufu, nitatoa mifano.
Hivi karibuni katika kikao cha Baraza la Halmashauri ya Wilaya ya Magu, mhandisi wa maji alitoa taarifa ya utekelezaji wa mwaka ambapo alieleza jinsi alivyotumia mamilioni ya fedha kukarabati malambo na kuweka pampu za mikono kwenye visima katika vijiji mbalimbali, lakini wakati madiwani walipoanza kuhoji uhalali wa taarifa hiyo, ilibainika kuwa lambo moja la Lwangwe ambalo lilitajwa kuwa limekamilika kwa asilimi 80 halipo kabisa.
Pia ilibainika kuwa pampu zilizofungwa kwenye visima hivyo zilikuwa hazina ubora kiasi ambacho diwani mmoja alidai kuwa katika kijiji chake pampu iliyopo ina uwezo wa kujaza lita 60 tu za maji kwa siku. Hizi ndizo taarifa zinazotamalaki katika halmashauri zetu.
Taarifa ya Ofisa Kilimo/Mifugo pia haikuonyesha matumizi ya jumla ya sh 20,000,000 zilizotolewa kukarabati majosho manne wilayani hapo na pia ameshindwa kuandika taarifa ya jinsi alivyotumia fedha za awali katika miradi hiyo ili apewe kiasi kingine cha fedha.
Licha ya kuwapo dosari hizo za wazi ambazo zimerudisha nyuma maendeleo ya wananchi katika sehemu husika, bado viongozi wa halmashauri hiyo wameshindwa kuwachukulia hatua watendaji wa aina hiyo, kitu kinachojenga hisia kuwa nao ni washiriki katika uhalifu huo.
Haiwezekani mtendaji aandae taarifa ya mwaka na akasahau matumizi ya kiasi kikubwa cha fedha kama hicho, pia haiwezekani ikaandaliwa taarifa ya lambo ambalo halipo kabisa lakini watu hao wakaendelea kukalia nyadhifa zao, kuna kitu.
Takriban miezi mitatu iliyopita, Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Juma Abubakar, alitoa ahadi ya nguvu ya kuwapatia mchele magunia matano watoto yatima wanaolelewa katika Kituo cha Bethany Family baada ya kuguswa na hali yao na jinsi wanavyokosa upendo wa mama zao ambao hawapo tena.
Yeye kama mzazi alitoa ahadi hiyo ambayo iliamsha ari kubwa miongoni mwa jamii ya kuona umuhimu wa kuwasaidia watoto yatima na wale walio katika mazingira magumu ambao wanaongezeka kwa kasi ya ajabu kutokana na kuendelea kuenea kwa maambukizi ya UKIMWI, lakini hadi sasa bado watoto hao hawajapokea mchele huo!
Hizi ndizo ahadi za viongozi wa kisiasa ambazo badala ya kuchochea maendeleo ya jamii, zinatolewa kwa lengo la kujipatia umaarufu na baadaye hazitekelezwi.
Viongozi wa kituo hicho wamefuatilia hadi wamechoka na wamesema kuwa hawataki mgogoro na serikali.
Mfano mwingine ni ule wa uteuzi wa eneo la kujenga makao makuu ya wilaya ya mpya Rorya, mkoani Mara, ambapo madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime wamependekeza kuwa makao hayo yawe kwenye Kijiji cha Utegi badala ya mji wa Shirati au Kijiji cha Randa, ambacho kipo katikati mwa jimbo hilo.
Kimsingi haya ni maamuzi ya kisiasa ambayo yanalenga kumjengea mtu mmoja au baadhi ya watu umaarufu binafsi bila ya kujali masilahi ya jamii husika katika eneo hilo, kwa sababu unapoamua kujenga makao ya wilaya kwenye eneo ambalo liko pembezoni mwa jimbo, hauwatakii mema wananchi watakaoathirika kwa umbali unauchochea.
Mimi ni mmoja wa wakazi wa jimbo hilo, nimefarijiwa sana na uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete, kwa wakazi wa jimbo hilo kupata wilaya, lakini uamuzi huo tayari umenyakuliwa na baadhi ya viongozi wenye uchu wa kunufaisha nia na dhamira zao binafsi na kusahau hali na umaskini unaowakabili wapiga kura wao kwa maslahi binafsi.
Kimsingi, Shirati si katikati ya jimbo hilo na kama mimi ningekuwa mmoja wa wapiga kura, ningeipigia Shirati kura kwa sababu kuu moja kuwa ina miundombinu yote muhimu kwa ajili ya kuwa makao makuu ya wilaya; ina mahakama, hospitali kubwa mbili, shule za sekondari tatu, bandari, uwanja wa ndege, ofisi za Uhamiaji, posta, mtandao wa maji ya bomba na kuna idadi kubwa ya watu na eneo kubwa la kujenga makao ya serikali.
Kwa mantiki hiyo inakipiku Kijiji cha Utegi ambacho najua kimepigiwa kura kutokana na sababu kuu moja kuwa Mbunge na Mwenyekiti wa halmashauri wanatoka katika eneo hilo, na hakina miundombinu.
Hivyo, kukijenga kijiji hicho kuwa makao makuu ya wilaya kutawagharimu sana wakazi wa jimbo hilo ambao hadi sasa wanakabiliwa na matatizo lukuki, ikiwamo umaskini uliokithiri kutokana na kukosa zao la biashara la uhakika.
Bado pamekuwapo mikakati mingi ya kuendeleza mazingira ya Ziwa Victoria kupitia miradi mbalimbali inayoingiza fedha kutoka kwa wafadhili au mikopo kutoka mashirika mbalimbali; kumekuwapo makongamano, semina na warsha nyingi zilizokwisha kufanyika kwa jina la hifadhi ya Ziwa Victoria lakini yako wapi matokeo?
Bado kuna uharibifu mkubwa wa mazingira unaendelea kandokando mwa ziwa hilo kwa kasi ya ajabu huku viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia hifadhi yake wakiendelea kuandika maombi mengine ya mikopo bila kujua kuwa kwa kufanya hivyo wanatuendelezea mzigo mkubwa wa madeni.
Ziwa hili limeendelea kuharibika kwa kasi ya ajabu kutokana na maamuzi ya kisiasa, samaki wamepungua na sasa kuna taarifa kuwa hewa ya oksijeni nayo imepungua kwa kiasi kikubwa na hivyo kuhatarisha uhai wa ziwa hilo.
Ili tuendelee tunahitaji uongozi bora na si bora uongozi, tunahitaji siasa safi na si siasa zenye kaulimbiu za ajabu kila kiongozi anapochaguliwa!
Tunahitaji viongozi wanaojali watu waliowachagua na si wale wababaishaji na wanaopiga propaganda.
Ukienda mkoani Kilimanjaro utaona jinsi kilimo cha kahawa kilivyosimamiwa na viongozi wa mkoa huo na kubadilisha maisha ya wanachi wa eneo hilo, utaona jinsi wananchi walivyojengewa uwezo wa kuwahoji viongozi wababaishaji.
Katika Kanda ya Ziwa, eneo lenye utajiri mkubwa wa madini, mabonde ya nafaka, mbuga za wanyama na ziwa, hali ya wakazi wa eneo hili ambao kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Uchaguzi ndio wapiga kura wakuu kwenye chaguzi za kitaifa, lakini eneo hili limeendelea
kuwa duni kiasi cha wakazi wake kushindwa kujinunulia hata kiti cha kukalia katika kaya.
Kwa nini tuendelee kuendekeza siasa ndogondogo za kibinafsi kwa ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya? Je, kwa hali hii tutaweza kweli kuwatokomeza maadui hao?
osoropjn@yahoo.co.uk
Makala -Tuna watu, ardhi, siasa safi, kwanini hatuendelei?