Tanganzo la kifo cha mwanaharakati mwenzetu- marehemu mbwana masoud

jamii01

JF-Expert Member
Oct 1, 2010
1,974
1,400
TANZIA YA KIFO KWENYE UCHAGUZI MDOGO WA JIMBO LA IGUNGA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Ubungo Mkoa wa Kichama wa Kinondoni Kanda Maalumu Dar es salaam kinasikitika kutangaza kifo cha mwanachama Mbwana Masoud kilichotokea wakati wa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga.

Marehemu Mbwana Masoud alikuwa ni mmoja wa wanachama walijitolea kusafiri kwenda Igunga kwa ajili ya kuwa wakala kwenye uchaguzi uliofanyika tarehe 2 Oktoba 2011. Marehemu Mbwana Masoud alitoweka katika mazingira ya kutatanisha wilayani Igunga tarehe 2 Oktoba 2011.

Baada ya jitihada za viongozi wa chama kumtafuta marehemu kushindikana Mwenyekiti wa Chama Mkoa wa Kinondoni ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, John Mnyika (Mb) alitoa taarifa polisi tarehe 3 Oktoba 2011 na kufungua jalada RB/748/2011.

Tarehe 9 Oktoba 2011 wananchi wilayani Igunga walikuta mwili wa marehemu ukiwa porini katika eneo ambalo linajulikana zaidi kama msitu wa magereza.

Taarifa ilitolewa na wananchi kwa diwani wa kata ya Igunga Vicent Kamanga (CHADEMA) ambaye alifika katika eneo hilo na baadaye maafisa wa polisi walifika na kupeleka mwili huo katika chumba cha kuhifadhia maiti.

Tarehe 9 Oktoba 2011 Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alitembelea nyumbani kwa marehemu katika mtaa wa Kwa Jongo Kata ya Makurumla kuifariji familia ya marehemu na kukubaliana na ndugu wa marehemu kutuma wawakilishi wa chama na familia kwenda Igunga kuhakiki mwili uliopatikana.

Tarehe 10 Oktoba 2011 wawakilishi wa familia wakiwa pamoja na Katibu Mwenezi wa Chama Wilaya ya Ubungo Ali Makwilo walishuhudia mwili husika na kuthibitisha kuwa ni wa marehemu Mbwana Masoud.

Leo Tarehe 11 Oktoba 2011 mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi wa kidaktari (post mortem) kuweza kubaini chanzo cha kifo na ripoti wamepatiwa jeshi la polisi. Hata hivyo, mazingira ya kupatikana kwa mwili wa marehemu yanaashiria marehemu Mbwana Masoud aliuwawa.

Kutokana na hali ya mwili wa marehemu, maziko yatafanyika leo tarehe 11 Oktoba 2011 alasiri katika kata ya Igunga yakihusisha wawakilishi wa familia ya marehemu, viongozi wa chama, wanachama na wananchi wa maeneo husika kwa ujumla.

Viongozi waliopo kwenye maziko hayo ni pamoja na Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Tabora, Halfan Athumani, Diwani wa Kata ya Igunga Vicent Kamanga na aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Igunga kupitia CHADEMA, Joseph Kashindye.

Hitma ya Marehemu itafanyika hapa Dar es salaam nyumbani kwa marehemu Mtaa wa kwa Jongo Kata ya Makurumla tarehe 13 Oktoba 2011 saa 7 mchana baada ya swala ya adhuhuri na itahudhuriwa na viongozi waaandamizi wa chama ngazi mbalimbali akiwemo Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika.

Chama kitaendelea kuwa pamoja kwa hali na mali na wafiwa katika kipindi hiki kigumu na kinavitaka vyombo vya dola kuharakisha uchunguzi ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wahusika. Marehemu amekufa akiwa katika safari ya kulinda haki na kutetea demokrasia na maendeleo; apumzike kwa amani.

Imetolewa tarehe 11 Oktoba 2011 na:

Nasor Balozi
Katibu-Wilaya ya Ubungo
0713/0767/0783-636676
 
Back
Top Bottom