Tanesco: Kifaa cha kudhibiti umeme kimeharibika vibaya

Mwanajamii

JF-Expert Member
Mar 5, 2008
7,063
68
SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema kifaa cha kudhibiti umeme (Reactor) kilichowaka juzi, kimeharibika kwa kiwango kisichoweza kutengenezeka ingawaje tangi la mafuta halikulipuka.

Kadhalika limesema nyaya muhimu zinazosaidia kuendesha, kudhibiti mitambo pamoja na mawasiliano ziendazo upande wa eneo la msongo wa kilovoti 220, zimeharibiwa na moto.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Sophia Mgonja iliyotolewa jana Dar es Salaam ilisema chanzo cha tukio kitajulikana baada ya uchunguzi wa kitaalamu kukamilika.

Mgonja alisema baada ya kifaa kuwaka moto, vituo vyote vya ufuaji umeme kwenye gridi vilizimika kwa usalama na umeme kukatika sehemu zote zinazohudumiwa na Gridi ya Taifa.

Alisema hadi jana jioni, maeneo mengi yaliyounganishwa kwenye Gridi ya Taifa yalikuwa na umeme na kwamba kutokana na laini za kilovoti 220 kuanzia Morogoro hadi Dar es Salaam kuwa nje udhibiti wa msongo wa umeme unahitaji umakini wa hali ya juu.

Kuhusu urejeshaji wa umeme alisema katika Gridi ya Kusini Magharibi, Kaskazini Magharibi na Kaskazini Mashariki katika Mkoa wa Iringa na Mufindi, Mbeya umeme ulirejeshwa kwa saa tofauti kuanzia saa 10:57.

Katika mikoa ya Dodoma, Singida, Shinyanga, Mwanza, Musoma ulirejeshwa kuanzia saa 11:15 katika mikoa ya Moshi na Arusha kuanzia saa 12:03.

Alisema katika Gridi ya Mashariki, Mkoa wa Morogoro ulipata umeme saa 12:41 na kwa Mkoa wa Dar es Salaam na Zanzibar umeme ulipatikana kuanzia saa 8:10 alfajiri kwa kupitia upande wa laini ya kutoka Mlandizi ya msongo wa kilovoti 132.

Aidha, alisema kazi inayoendelea ni ya kurekebisha nyaya zilizoungua kwa upande wa msongo wa kilovoti 220 na kwamba inatarajiwa hadi jana jioni marekebisho hayo kukamilika na hali ya umeme kurudi kama kawaida.

Shirika hilo liliwaomba radhi wateja wake kutokana na usumbufu wowote uliojitokeza kutokana na ajali hiyo na wananchi wawe wavumilivu wakati mafundi wakifanya kazi ya kurudisha umeme katika hali ya kawaida.
 
Back
Top Bottom