TAKUKURU kusaka watumishi hewa Pwani, K’njaro

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,531
SUALA la kusaka watumishi hewa limeendelea kushika kasi nchini baada ya mikoa kadhaa kutangaza kuikabidhi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza kwa kina huku watendaji waliohusika wakisimamishwa kazi.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda juzi aliitaka Takukuru kuchunguza watumishi hewa katika mkoa wake baada ya kutoridhishwa na idadi ya watu 71 waliobainika. Mkoani Kilimanjaro, Mkuu wa Mkoa huo, Said Mecky Sadiki, ameagiza kusimamishwa kazi Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, William Msapali na kutaka Takukuru imchunguze mtumishi Agapit Chuwa aliyepo masomoni nchini Japan kwa miaka 13.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo ameikabidhi Takukuru kuchunguza maelezo ya halmashauri za wilaya katika mkoa wake ikiwa ni kweli zimerejesha Hazina Sh milioni 249 ambazo ni sehemu ya Sh milioni 641 zilizopotea kwa kulipa watumishi hewa na kuitaka Sekretarieti ya Mkoa kufuatilia suala hilo kwa wakurugenzi.

Sadiki, ameagiza Halmashauri ya wilaya ya Mwanga kumsimamisha kazi Msapali kwa madai ya kushindwa kutoa ushirikiano wakati wilaya hiyo ikihakiki watumishi hewa na kuwabaini 21 ambao wameisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh milioni 199. Alisema tuhuma nyingine kwa Msapali ni kushindwa kubainisha taratibu zilizomruhusu mtumishi wa sekta ya afya, Chuwa ambaye mwaka 2004 aliomba kibali kwenda masomoni nchini Urusi ambapo alijiongezea muda na sasa yupo nchini Japan huku akilipwa mshahara.

Sadiki aliitaka Takukuru pia kumchunguza mtumishi huyo aliyepo masomoni kwa zaidi ya miaka 13 kwani ameisababishia serikali hasara ya Sh milioni 54. Kutokana hilo, Sadiki alitaka taratibu kufanyika ili kusitisha mshahara kwa mtumishi huyo na kuitaka Takukuru kufanya uchunguzi wa kina ili kujiridhisha na baadaye kumfikisha mahakamani mtumishi huyo aliyepo masomoni na wengine wote walioisababishia serikali hasara.

Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Jamhuri William alisema hakuna kumbukumbu za kutosha za taarifa za Chuwa ingawa alipewa ruhusa ya miaka mitatu kuanzia mwaka 2004. Alisema mtumishi huyo alikuwa akijiongezea ruhusa kwa kushirikiana na maofisa Utumishi waliokuwapo ingawa baadaye tena alipewa ruhusa nyingine mwaka 2014 hadi 2016 kuendelea na masomo katika mazingira ya kutatanisha.

Alisema barua ya kuomba ruhusa ya mtumishi huyo iliandikwa lugha ya Kijapan lakini pia kwa Kiingereza ambacho hakikuwa kinasomeka vizuri jambo lililosababisha badala ya kupewa ruhusa ya miaka miwili, akapewa ya miaka mitatu. Awali katika taarifa yake kwa mkuu huyo wa mkoa, Mkuu wa Wilaya hiyo, Shaibu Ndemanga alisema wilaya hiyo yenye jumla ya watumishi 2,048 ilitambua watumishi hewa 21 walioisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh milioni 199.

Alisema walitumia hati ya malipo ya Septemba mwaka jana na kwenda katika kila ofisi kujua kama wahusika wapo ofisini ambapo 17 walikuwa wagonjwa, 14 waliomba ruhusa, 20 walikuwa likizo, 26 watoro, 26 walihama lakini bado walisomeka kwenye hati ya malipo.

Huko mkoani Pwani, Ndikilo akizungumza na gazeti hili ofisini kwake, alisema ameituma Sekretarieti ya Mkoa huo kufuatilia kwa wakurugenzi wa halmashauri za wilaya za mkoa huo kuchunguza ikiwa ni kweli kuwa Sh 249, 452,390 zimerudishwa Hazina. Fedha hizo ni sehemu ya fedha kiasi cha Sh 641,361,239 ambazo ni hasara zilizolipwa kwa watumishi hewa 25 mkoani humo na zinadaiwa zilirejeshwa Hazina.

Mbali na kuiagiza Sekretarieti kufuatilia fedha hizo, pia Ndikilo amewaagiza wakuu wa wilaya mkoani humo kuvitumia vyombo vya dola kama Jeshi la Polisi, Takukuru kufuatilia watu waliohusika kuchukua fedha hizo. Ndikilo alisema kuwa serikali haijaridhishwa na majibu ya wakurugenzi wa halmashauri za wilaya hizo kuwa fedha hizo wamezirejesha Hazina kwani hakuna viambatanisho vyovyote vinaoonesha kuwa fedha hizo zilipelekwa Hazina.

Ndikilo alisema kuwa kati ya hao watumishi hewa wamo waliofariki dunia, wasiokuwapo kazini, walioacha kazi na wastaafu, lakini walikuwa wanalipwa kama vile wako kazini jambo lililo kinyume cha sheria na wanastahili kuchukuliwa hatua kali mara watakapokutwa na tuhuma hizo.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom