Tafiti za Twaweza zina lengo gani?

EJL

Member
Jan 14, 2012
83
54
TATIFI ZA TWAWEZA ZINA LENGO GANI?
Serikali nyingi duniani ikiwemo Tanzania hutegemea sana taarifa za utafiti kutoka katika taasisi zake au za binafsi. Aidha kwa miaka mingi nyuma taasisi za utafiti zilijijengea heshima kubwa sana kwa kufanya utafiti makini (unaokidhi vigezo vyote vya utafiti) na wenye kutoa matokeo halisi na sahihi na mapendekezo mazuri kwa nia ya kuwezesha wafanya maamuzi kutumia taarifa hizo kufanya maamuzi yenye manufaa. Taasisi ya Twaweza ilipoanza ilijijengea jina kubwa lakini miaka ya hivi karibuni imekuwa ikitoa taarifa za utafiti zenye ukakasi mwingi. Sikuwahi na sitajadili matokeo ya utafiti wao kwa masuala ya kisiasa kwa sababu huko si eneo langu huwa kuna chenga nyingi.
Leo hii nimesoma katika vyombo vya habari, kuwa wametoa matokeo ya utafiti juu ya huduma za afya ambao unasema huduma zimekuwa bora ! Najiuliza ubora upi wa huduma?? Bahati mbaya pamoja na taarifa yao kutoa majumuisho kuwa huduma za afya zimeboreka (kwa kuwa waliiohojiwa wanasema walipokelewa vizuri hospitalini, hawakusubiri sana, na walionwa na wahudumu) lakini bado utafiti wao unaonesha kuna uhaba mkubwa wa vifaa tiba na dawa. Haujazungumzia kuhusu uhaba wa wahudumu. Maswali ya kujiuliza ni haya:
1. Je, kwa kupokelewa vizuri (hawajasema uzuri huo ni upi) lakini hakuna dawa na vifaa tiba kunahakikishaje afya ya mtanzania?
2. Je, ni lini tatizo la uhaba wa watumishi wa afya lilipatiwa ufumbuzi wakati sote tunajua kuwa serikali haijaajiri tangu iingie madarakani?
3. Hivi , Twaweza hawakuweza kuona bado wazee wanalipia huduma za afya tena kwa bei sawasawa na wengine? Tarehe 4 mwezi huu nilikuwa Muhimbili, nikiwa dirishani kwenye kulipia nikakutana na mzee mmoja amechanganyikiwa kwa sababu anatakiwa alipie naye hakujua hayo. Baada ya kuonana na daktari niliandikiwa vipimo nikaenda maabara. Akaja mzee mmoja akafanyiwa hesabu zake akaambiwa, "baba , vipimo vyako unatakiwa kulipia 25,000/" Mzee akasema mie nina msamaha! Akajibiwa msahama huo ni wa gharama za kumuona daktari tu, vipimo na dawa unatakiwa kulipia. Mzee akasema sina fedha mamangu. Akaambiwa nami sina la kukusaidia labda kamuone daktari wako. Mzee akaanza kujipapasa na kufungua wallet yake alikuwa na 20,000/ tu . Nikaotoa 10,000/ niliyokuw anayo nikampa aongezee. Sikumlaumu yule dada mhudumu kwa sababu ndio utaratibu alioambiwa! Sikumlaumu mzee kwa kutokuja na hela kwa sababu kila siku tunasikia wimbo wa wazee watibiwe bure! Muhimbili kila kona kuna matangazo "MPISHE MZEE AHUDUMIWE KWANZA" nilidhani kuna unafuu wa huduma. Najiuliza Twaweza haya hawayaoni? Ni nini kinasukuma kuconclude kuwa huduma za afya zimeboreka???

4. Niliona utayari wa madaktari, wauguzi na wahudumu wengine wa afya pale Muhimbili katika kuhudumia wagonjwa. Lakini nikaona wana changamoto za wazi kabisa kukosa vifaa. Yaani unamuona nesi au daktari anao ufahamu wa tatizo lako na tiba yako lakini hana vifaa na dawa kuweza kukusaidia. Mara zote ninapotembelea hospitali zetu hizi za umma, ninachojifunza ni kuwa tunao wataalam wazuri, wenye moyo wa kutuhudumia lakini hakuna vifaa. Kwa hiyo wakati mwingine wanakuwa wakali kwa sababu ya msongo wa mawazo, mazingira yao ya kazi ni mabaya. Fikiria daktari hana BP mashine kwenye ofisi yake analazimika kuomba chumba cha pili!!!

Kwa kuwa Tanzania imepata Rais "msikivu na mtendaji", ni fursa nzuri kwa taasisi za utafiti kama Twaweza, kurejea maadili na kanuni za utafiti. Wafanye tafiti makini na sahihi. Watoe matokeo halisi na sahihi yatakayowezesha serikali kupanga vipaumbele na kugawa vema rasilimali. Taasisi za utafiti ambazo si za serikali , zikitoa taarifa ambayo inaonesha hali ni mbaya (kwa kuwa ndio ukweli wenyewe) hazina cha kuhofia! Maana si waajiriwa wa serikali hawa. Iifike mahali tuweze kutofautisha ipi ni kazi ya watafiti guru na ipi ni matokeo ya swali la kipima joto !

MUNGU ATUREHEMU WATANZANIA

Lugano EJ
 
Back
Top Bottom