Tafakari: "Ng'ombe wengine wana Mapembe!"

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246
Ndugu zangu,

Kule kwetu Usangu ng’ombe dume na mwenye pembe huitwa kambako. Na kila zizi lina kambako zake. Wengine wanasema ‘ Makambako’. Na si unajua? Kuna mji unaitwa Makambako mpakani mwa Iringa na bonde la asili ya mababu zangu; Bonde la Usangu.


Naam, CCM nayo ina kambako zake zizini. Kuna wanaotakiwa watoke zizini ifikapo Septemba mwaka huu. Ni mwisho wa mwezi ujao; ‘ Habari ndo hiyo’. Kambako zimesikia, lakini zimezila. Na unafanye unapotaka kuzitoa zizini kambako zilizozila? ( Kuzila ni sawa na kugoma)


Marehemu babu yangu angeniambia; “ Kuna vumbi litatimka, hivyo, hakikisha umeimarisha wigo wa zizi. Na kama mlango wa zizi ni mwembamba, basi, ongeza ukubwa wa mlango. Hakikisha pia , unaongeza nguvu ya watu mlangoni. Zitoke kambako tu, na si ng’ombe wengine. Maana , kila kambako ana ng’ombe wengine nyuma yake."


Ningemwuliza babu swali la nyongeza; lakini, unafanyaje na kambako aliyezila akiwa amekaa chini zizini? Maana, kabla ya kumswaga kambako nje ya zizi ni lazima ainuke. Nina mfano hai, utotoni ilishawahi kunitokea. Nilipokuwa nachunga ng’ombe wa babu kuna siku kambako ilizila kwenda.

Nikaenda kwa babu kumpa taarifa. Naye akaniambia; ” Kambako ikigoma kuinuka ing’ate mkia”. Nilifanya hivyo, na kweli , kambako ikainuka kwa kishindo! Ndio, babu yangu alikula chumvi nyingi. Alipata pia kuiambia; ”Ng’ombe haujui umuhimu wa mkia wake mpaka ung’atwe. Ng’ombe ni mkia”


Na unafanyaje basi, pale kambako inapogoma kuinuka hata inapong’atwa mkia? Natamani babu yangu angekuwa hai anijibu swali hili!


Naam, ng’ombe wengine wana mapembe. Na hili ni Neno La Leo.

Maggid,
Dar es Salaam,
Agosti 3, 2011
0754 678 252
MJENGWA - Picha, Habari & Matangazo
 

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom