Tafadhali Usininukuu: Afrika Uwaziri Mkuu Ni Cheo Cha Lawama!

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246
Ndugu zangu,

Mwalimu Nyerere alipong'atuka alipata kumwelezea rafiki yake Rashid Kawawa. Alitamka; " Huyu Rashid huyu sidhani kama kuna mtu mwingine anayeweza kufanana naye."

Mwalimu alimwagia sifa nyingi Rashid Kawawa ikiwemo moja kubwa ya uvumilivu. Rashid Kawawa ama maarufu kama ' Simba wa Vita' alipata kuwa Waziri Mkuu wakati wa uongozi wa Mwalimu.

Na Afrika cheo cha Uwaziri Mkuu ni sawa na binadamu kugeuzwa ' Tingatinga', tena lenye mabawa. Kazi ya tingatinga ni kutangulia mbele kusafisha njia. Waziri Mkuu hutangulia mbele. Atakayofanya yakiwa mema hachelewi kutamka; " Jamani haya yote yanatokana na hekima na busara za Kiongozi Mkuu" - Na Afrika hakuna anachofanya Waziri Mkuu bila Kiongozi Mkuu kujua na zaidi kutoa baraka zake.

Na mambo yakienda kombo?

Waziri Mkuu anapaswa kuyakabili madongo na mawe yote yatakayorushwa. Ahakikishe kuwa Kiongozi Mkuu haguswi hata na changarawe. Afrika ukiona mawe yanarushwa na yanamgusa Kiongozi Mkuu, basi, ujue kuwa Waziri Mkuu hafanyi kazi yake inavyopaswa iwe. Huyo atakuwa amekalia kuti kavu. Maana, cheo cha Uwaziri Mkuu ni cha kujitoa muhanga au kutolewa kafara. Ndio, punda afe, mzigo wa bwana ufike! Afrika Waziri Mkuu ikibidi kufa na afe ( ajiuzuru) ili mradi kufanya hivyo kutahakikisha Serikali inayoongozwa na Kiongozi Mkuu inabaki hai na salama.

Hivyo basi, Waziri Mkuu pia ni Mshauri Mkuu kwa Kiongozi Mkuu. Afrika ukiona katika nchi mambo yanaharibika na mpaka Kiongozi Mkuu anaguswa na madongo na mawe yanayorushwa, basi, kuna mawili, ama, Waziri Mkuu hana ushauri mzuri kwa Kiongozi Mkuu, au Kiongozi Mkuu hashauriki.

Na ilikuwaje kisa cha Julius na Rashid?

Hawa walikuwa ni marafiki wawili. Katika vyeo mbali mbali alivyopata kumpa Kawawa, Julius Nyerere alimpa rafiki yake Rashid cheo cha Uwaziri Mkuu. Si kwa sababu ya urafiki wao, ni kwa sababu Rashid alikuwa hodari na mchapakazi.

Na kwenye kutekeleza mambo ya Serikali, Rashid alikuwa tingatinga kweli kweli. Watanzania tunakumbuka alivyosimamia operesheni ya maduka ya ushirika. Kila alipokwenda Rashid alitoa maagizo maduka binafsi yafungwe na yaanzishwe maduka ya ushirika.

WaTanzania wa vijijini na hata mijini hawakuwa na uzoefu wa biashara ya maduka. Hali ikawa mbaya. Maduka ya ushirika hayakuwa na ufanisi . Wananchi wakalalamika sana. Aliyekuwa akitupiwa lawama ni Rashid Kawawa kana kwamba ule ulikuwa ni mpango wa Kawawa. Na Julius akapima upepo. Akabaini, kuwa tingatinga lake ( Rashid) limekwama porini.

Nyerere hadharani akaikosoa operesheni ile na hata kuonyesha kumshangaa Rashid. Na akamvua rafiki yake cheo cha Uwaziri Mkuu. Tena akamwita na kumwomba ushauri Rashid wa nani anafikiri anafaa kuchukua nafasi yake.

Mpaka anakufa, Rashid hakuwahi kumlaumu Julius kwa maagizo yaliyoufanya umma umwite Rashid majina kadhaa ya kejeli ikiwamo moja la gea ya gari aina ya Landrover. Naam, Afrika Uwaziri Mkuu ni cheo cha lawama. Tafadhali usininukuu!

Maggid Mjengwa,
Iringa
 
Hatumtaki EL. Kuna watanzania wengi tu wajasiri na wenye nia njema na nchi yetu. We will be alright.
 
Back
Top Bottom