Sumaye: Siyo dhambi kudai katiba mpya

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
WAZIRI Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye amesema siyo dhambi watu kudai katiba ya mpya wanapobaini kuwa iliyopo ina kasoro.

Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 katika Serikali ya Awamu ya Tatu, alisema katiba ya nchi ni kiungo muhimu katika taifa na maisha ya Watanzania kwa ujumla.

Mtendaji huyo wa Serikali ya Rais Benjamini Mkapa aliiambia Mwananchi Jumapili, kuwa kama kuna watu wanaodhani kuna mambo hayaendi vizuri ni wajibu wao kudai marekebisho ya katiba ili kupata katiba wanayoamini kuwa itawalinda.

“Kwanza Katiba ni chombo kinachotuongoza watu wote, kinachosimamia masuala ya kiuchumi, kijamii na kisiasa, hivyo kama kuna watu wanaona kuna kasoro katika maeneo hayo, si dhambi wakisema madai yao,” alisema Sumaye.

Hata hivyo, Sumaye ambaye alikuwa Mbunge wa Hanang, mkoani Manyara kwa miaka mingi, alionya kuwa ni vema madai hayo yakafanywa kwa utaratibu unaoeleweka na sio watu kuongea pembeni bila kuweka bayana kasoro wanazoziona kuwa zinahitaji kurekebishwa kwa kuwa na katiba mpya.

“Si sahihi kudai katiba mpya bila kueleza kivipi katiba iliyopo ina matatizo,” alisema Sumaye na kutaka watu wenye hoja za kudai katiba mpya na kuziwasilisha kwenye vyombo husika.

“Wakati huu kuna wabunge wengi wa upinzani, na si wabunge wa upinzani tu, hata wale wa CCM wanaoona kuna haja ya kuwa na katiba mpya, ni vema wakatengeneza hoja na kuipeleka bungeni kuulezea umma kasoro zilizopo,” alisema Sumaye.

Aliongeza kuwa kuna tatizo la watu kulalamika bila kufafanua hatua kwa hatua kasoro wanazoziona kwenye katiba ya sasa, lakini akasema ana imani na Spika wa Bunge kwamba akipelekewa hoja hiyo, ataipokea na kujadiliwa bungeni.

Sumaye hakuwa tayari kueleza msimamo wake endapo kuna haja ya katiba mpya au la badala yake alisema “Kila mtu anatafsiri na uelewa wake. Hao wanaoona ina mapungufu watueleze ni mapungufu gani waliyoyaona.”

Aliongeza kuwa hoja ya kuifanyia marekebisho katiba inategemea na mahitaji yaliyopo kwa kipindi hicho na kutoa mfano wa serikali ya umoja wa kitaifa visiwani Zanzibar.

“Kwa mfano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar sasa ni ya Umoja wa kitaifa ambayo imepewa muda wa miaka mitano wa majaribio. Tukisema tubadilishe katiba hivi sasa, na ikija kutokea mabadiliko baadaye, tutabadilisha tena? Alihoji Sumaye.

Kwa mujibu wa Sumaye haitakuwa busara kila linapotokea jambo dogo kuwepo kwa mabadilika na kwamba katiba ya Tanzania ina mambo mengi ikilinganishwa na katiba za nchi nyingine.

Muda mrefu sasa, kumekuwa na vuguvugu la madai ya kuwepo kwa Katiba mpya kutoka kwa taasisi mbalimbali, viongozi wa dini na wanasiasa. Joto hilo liliongezeka baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 31 wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kilipoamua kulivalia njuga madai ya katiba mpya.

Kilio hicho cha Chadema kimekuwa kikipata watu wanaoikiunga mkono wakiwamo wanasiasa mashuhuri nchini.
Hivi karibuni Rais Mstaafu Benjamin Mkapa alipokuwa katika mkutano wa Chama Cha Mawakili wa Afrika Mashariki nchini Burundi alisema kuwa katiba ya nchi yoyote ni sawa na roho katika mwili wa binadamu, hivyo kuwa na kitaba bora ni jambo muhimu kwa maendeleo ya nchi zetu.

Katika mkutano huo Mkapa alisisitiza ushirikishwaji wa wananchi katika mchakato mzima wa kuandaa katiba mpya, kuwa na tume huru ya uchaguzi yenye kuwajibika na kuwepo kwa namna bora ya uteuzi wa makamishna.

Hoja ya kuwepo kwa Katiba mpya pia imewahi kuungwa mkono na watu waliobobea katika masuala ya sheria na waliowahi kushika nyadhifa mbalimbali katika serikali.

Miongoni mwa watu hao ni aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Jaji Mkuu Mstaafu Mark Bomani ambaye alisema kuwa ni wazi kuwa katiba ya sasa imepitwa na wakati lakini kinachoisumbua serikali katika suala hilo, ni hofu isiyokuwa na msingi.

Wengine waliounga mkono ni Askofu Methodius Kilaini wa Jimbo Kuu Katoliki la Bukoba.

Kalaini alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akiwataka wanasiasa kuorodhesha mahitaji muhimu yanayotakiwa katika mabadiliko hayo ya katiba ili wadau wengine waongeze nguvu katika kuidai
 
Back
Top Bottom