Sumari, Sarakikya wajipanga mashambulizi

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,319
33,125
Siyol(1).jpg

Siyoi Sumari


Makada wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) watakaochuana katika kura za maoni kupata mgombea atakayepeperusha bendera ya chama hicho katika Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki, wamesema wamekubaliana na maamuzi ya Kamati Kuu (CC) ya kuamuru kupigwa kwa kura raundi ya pili.

Wagombea hao, Siyoi Sumari na William Sarakikya, wakizungumza na NIPASHE jana, walisema uamuzi wa CC wameupokea kwa mikono miwili na sasa wanajipanga kuhakikisha wanapambana katika uchaguzi wa marudio wa kura za maoni kesho.

SIYOI: BUSARA IMETUMIKA

“Nimekubaliana na maamuzi ya Kamati Kuu na kwa kweli busara kubwa ilitumika na sababu ilikuwa ya msingi, na kama mwanachama wa CCM lazima nitii maamuzi ya vikao vya juu na muda huu unavyoongea na mimi nipo njiani kuelekea jimboni kuweka mambo sawa,” alisema Sumari.

Kuhusu madai kwamba kutenguliwa kwa matokeo ya awali kunamlenga yeye ili kumdondosha katika kinyang’anyiro hicho, alisema hana ukakika kama kweli kuna hila kama hizo dhidi yake na kwamba pale kwenye ukweli hizo hila haziwezi kufanikiwa.
Sumari alisema iwapo atashindwa atakubaliana na matokeo na chama kikimpitisha Sarakikya, atamuunga mkono.

Alipoulizwa kwamba jimbo hilo linataka kufanywa kama la kifalme kwa sababu baba yake alikuwa mbunge, alisema alichukua fomu za kuwania ubunge kwa ridhaa yake mwenyewe hivyo wanaowaza hivyo ni wapotoshaji.

“Muongozo wa CCM Ibara ya 14 inaeleza kuwa mwanachama ana haki ya kidemokrasia kwa mujibu wa Katiba kuwani nafasi yeyote katika ngazi ya chama hivyo ndiyo maana nilipata msukumo wa kuchukua fomu,” alisema Sumari.

Kuhusu madai kwamba siyo raia wa Tanzania, alisema tuhuma hizo hazina ukweli, kwani pamoja na kwamba alizaliwa Kenya, lakini wazazi wake ni Watanzania hivyo kulingana na Sheria ya Uraia ya mwaka 1995 yeye ni raia wa Tanzania.

“Citizenship Act ya 1995 inaeleza wazi uraia kwa mtu ambaye ni Mtanzania aliyezaliwa nje ya nchi, inaeleza kuwa kama mtu alizaliwa nje ya nchi, lakini wazazi wake wote wawili ni Watanzania anatambuliwa kama raia wa Tanzania,” alisema Sumari.

Sumari pia alielezea shinikizo la baadhi ya wanachama kushinikiza vikao vya juu vya chama vimteue yeye kuwa mgombea, akisema hilo haliwezi kumuathiri kisiasa kwa sababu kila mwanachama wa CCM ana haki ya kidemokrasia kumshabikia mgombea anayemuona anafaa.

SARAKIKYA: SINA TATIZO NA UAMUZI

Kwa upande wake Sarakikya alisema hana tatizo na uamuzi uliochukuliwa na CC na kwamba amejipanga vyema kuhakikisha anaibuka na ushindi na pia atakubaliana na matokeo iwapo atashindwa.

Juzi CC ilitangaza kutengua matokeo ya kura za maoni kufuatia wanachama waliochukua fomu kuomba kuteuliwa kuwania ubunge katika jimbo hilo kushindwa kufikisha asilimia 50 ya kura zilizopigwa na kuamuru uchaguzi huo kurudiwa kesho.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Mnauye, alisema uchaguzi huo utawakutanisha Siyoi aliyeshika nafasi ya kwanza na William aliyeshika nafasi ya pili.

Katika kura za maoni, Siyoi Sumari alipata kura 361, William Sarakikya (259), Elirehema Kaaya (205), Elishilia Kaaya (176), Anthony Musani (22) na Rishankira Urio (11).

VIJANA WAFURAHIA

Wanachama wa Jumuiya ya Vijana (UVCCM) Mkoa wa Arusha wamefurahishwa na uamuzi wa CC kwa kutengua matokeo ya kura za maoni na kuamuru kurudiwa kesho kati ya Sumari na Sarakikya, lakini wametaka mianya ya rushwa izibwe.
Mjumbe wa Baraza la UVCCM Mkoa wa Arusha na Mwenyekiti wa Uchumi na Fedha wa Jumuiya hiyo wilayani Arumeru, Kennedy Mpumilwa, alisema uchaguzi huo usingerudiwa kama alivyowahi kusema, wangekuwa wamekiuka Ibara ya 21 inayotaka mgombea kupata kura nusu ya wapiga kura.

“Sasa hapa wapiga kura walikuwa 1,034 ila aliyeshinda alipata kura 361, ulipaswa kurudiwa hata siku ile ili kuepusha gharama zisizo za lazima,” alisema Mpumilwa.

Alisema kuwa kitu kikubwa kinachotakiwa kufanywa na kamati ya uchaguzi ni kuhakikisha wanaziba mianya ya rushwa eneo la upigaji kura siku hiyo na kwa kuanzia alishauri kutafuta ukumbi wenye vyoo ndani kuepusha wajumbe kutoka nje na kupeana milungula.



“Ule ukumbi wa awali wa Fikiria Kwanza haukuwa na vyoo ndani kiasi kwamba wajumbe walikuwa wanatoka nje kila mara na huko kulikuwa na masuala ya rushwa, sasa hili lisijirudie kama hapo hakuna choo basi watafute ukumbi mwingine,” alisema Mpumilwa.

Aidha alisema kuwa siku ya kupiga kura ni vizuri kuwepo na uhakiki wa hali ya juu wa majina yalingane na vitambulisho vya chama na atakayeonyesha apigwe muhuri wa siri katika kitambulisho chake na mkononi ili kuzuia kubadilishana vitambulisho na kupata kibali cha kitambulisho cha mjumbe mpiga kura.



“Nasema hivi kwa sababu siku ile kulikuwa na uchakachuaji mwingi wa watu kubadilishana vitambulisho na kwa kuwa hakukuwa na kuangalia sura katika kitambulisho cha chama na orodha ya majina ya wapiga kura, ilikuwa ngumu kuufanya uchaguzi uwe halali kwa sababu kuna mamluki waliingia,” alisema Mpumilwa.



Mpumilwa pia alisema kuwa iwapo watadhibi hilo watafanikiwa kumpata mgombea atakayeshinda kihalali bila uchakachuaji wa aina yoyote.



Aidha alisema kwa kurudiwa uchaguzi kutawafanya wale waliodhani anakosoa uchaguzi huo kwa sababu ya kutumika na upinzani, sasa watakaa pamoja kujenga chama na siyo kukibomoa kwa kutoleana matamko ya ajabu na kuwataka viongozi na vyama vya siasa kuyafanyia kazi maoni ya wanachama wadogo bila kujali vyeo vyao au umri.



Naye Katibu Muhamasishaji Arumeru Mashariki, John Nyiti, alisema amefurahishwa na uamuzi huo na wanashukuru kurudishiwa vijana, ambao yeyote atakayeshinda watamuunga mkono kupeperusha bendera ya CCM.

Alisema pia alifurahishwa na kitendo cha Nape kumsafisha Sumari kuwa si Mtanzania na anastahili kuchaguliwa na kuchagua kiongozi anayemtaka.

Naye kada wa CCM Anthony Msani, ambaye alihamia Chadema alisema kuwa kurudiwa kwa uchaguzi huo siyo jawabu la kudumu katika chama hicho.
Alisema hiyo ni hatua moja tu ya kuelekea kutafuta utatuzi wa matatizo yaliopo na wanachopaswa kufanya ni kuwa makini.

“Lakini nayatoa haya maoni siyo mwanachama tena wa CCM, natoa kama mtu wa kawaida huko nilishatoka mimi,” alisema Msani ambaye amehamia Chadema.

KURA ZA CHADEMA LEO

Mkutano Mkuu wa Jimbo la Arumeru Mashariki wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) unatarajiwa kufanyika kwa ajili ya kura za awali (maoni), kisha kitafuatia kikao cha Kamati ya Utendaji Wilaya ya Meru, kitakachofanyika kesho kwa ajili ya kufanya uteuzi wa awali wa mgombea wa chama hicho katika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki.

Taarifa ya Kurugenzi ya Habari ya Chadema iliyotolewa jana, ilisema Kamati Kuu ya Chadema inatarajiwa kuketi mjini Arusha, Machi 3, mwaka huu kwa ajili ya kufanya uteuzi wa mwisho wa jina la mwanachama atakayepeperusha bendera ya chama hicho kuwania ubunge wa Arumeru Mashariki.



CHANZO: NIPASHE
 
wanaibiana kura wenyewe kwa wenyewe watashindwaje kuiba kura za upinzani?
 
Back
Top Bottom