Ssra na mafao ya wafu

shabibu

New Member
Apr 20, 2012
3
0
Salaam,
Nikiamini kuwa Mola ni mkarimu na mwema kwetu kwa kutujaalia afya, uzima na uhai hata muda huu. Ni mapenzi yake ya dhati ambayo kamwe binadamu hata wawe wema kiasi gani hawawezi kuyadiriki. Ni maajabu twashangaa vitengenezwa badala ya kushangaa mtengenezaji wake. Sitaki kuamini kuwa watanzania wote tuna akili kama za baadhi ya watawala wetu ambao hawaamini kuwa watawaliwa wao wana akili na shuleni au chuoni wanaenda kutafuta maarifa tu.

Ni ukweli dhahiri usiohitaji, lenzi mbinuko wala mbonyeo kuukuza wala kuudogosha ili watu wauone. Ukweli kuhusu ukakasi wa sheria mpya ya Mifuko ya Jamii kama ilivyopitishwa bungeni na kushadidiwa ni Mamlaka ya mifuko ya Hifadhi (SSRA). Ni ukweli ambao takriban kila alochangia mafao yake kule ameshtushwa na kushtuka pale aliposikia kuwa michango yake itakuwa salama ikitumika kuendeshea shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa 'maslahi ya wenye nchi'.

Nimejaribu kupitia taarifa mbalimbali kupitia mitandao kutaka kujua na kubaini ni kwa kiasi gani mafao ya wafanyakazi hawa yatawasaidia kujikwamua baada ya kufikisha miaka 55 ya kustaafu kwa mujibu wa sheria.

Hii ni kwa sababu wastani wa umri wa kuishi kwa Tanzania ni kati ya miaka 51 na Kwa kifupi nilichogundua ni kuwa kama wapo watakaofanikiwa kupata mafao hayo basi watayatumia au yatatumika kununulia jeneza, sanda na kusakafia makaburi yao badaya ya kuyatumia kuendeshea maisha yao ya hapa duniani.

Miongozi mwa vyanzo mtandao hivyo ni: Index Mundo Tanzania Life expectancy at birth, UNDP Human Development Report 2011, etc. kama zilivyoorodhesha chini.

Tanzania Life expectancy at birth - Demographics
http://hdrstats.undp.org/images/explanations/TZA.pdf
Average Life Span Expectancy Chart - How Long Will I Live

Yawezekana nimekuwa na mawazo ya kishabiki zaidi wakati napitia vyanzo hivyo, ila naamini takwimu zilizowekwa ni sahihi au zinakaribia kwenye ukweli. Kwa mantiki hii wangapi wataishi kuchukua na kutumia mafao yao zaidi ya kutumika kununulia sanda na majeneza na kujengea makaburi yao au kufanyia arobaini na kusomea khitma!

Tumewasikia Mh. Job Ngugai, Nicholaus Mgaya na wanaharakati wakionesha msimamo unaokaribiana au kushabihiana na ule wa wafanyakazi hasa wa hali ya chini wa kutoridhika na Marekebisho ya Sheria ya mifuko ya jamii.

Naombeni wataalamu na wataaluma wa fani husika watusaidie kuelewa manufaa ya sheria hii badala ya kulalamika kwani kwangu na kwa ufahamu wangu finyu haya ni MAFAO YA WAFU.

Nakutakieni kila la kheri na nakuombeni tusimtangulie Mungu katika uumbaji wake na makadirio yake kwa viumbe wake bali tumtegemee yeye kwa dhati kwani wanasiasa na watawala wanataka tuwaabudu na kuwanyenyekea ili watende yenye manufaa kwetu. Nani anajua, yawezekana tukaishi miaka au umri wa ahadi yaani 70+ na mafao haya yakatusaidia kweli!
 
Back
Top Bottom