Spika Sitta: Viongozi wanakwamisha maendeleo

Gudboy

JF-Expert Member
Aug 14, 2009
867
77
Na Simon Mhina
22nd September 2009

Spika wa Bunge, Samwel Sitta.
Spika wa Bunge, Samwel Sitta, amesema viongozi wanachangia kurudisha maendeleo nyuma nchini kutokana na kukosa mikakati endelevu ya kusimamia miradi mbalimbali.
Kauli hiyo ilitolewa wiki ilipita na Spika wa Bunge wakati akifungua kongamano la kilimo kwa watendaji na maafisa ugani wa Wilaya ya Urambo, mkoani Tabora.
Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki wa Chama cha Mapinduzi (CCM), alifungua kongamano hilo kwa ajili ya kujadili matatizo ya kilimo ambayo yamekuwa yakileta changamoto kwa wakulima na kuyatafutia ufumbuzi ili kuleta mapinduzi ya kijani wilayani humo.
Alisema ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na Serikali ya kuleta mapinduzi ya kijani katika kilimo na watumishi wa serikali hawana budi kubadilika.
“Hivyo basi imeazimiwa kwamba kilimo kwanza iwe ndiyo dhana ya kuleta mapinduzi ya kijani kwa lengo la kuleta mabadiliko katika uzalishaji," alisema Sitta na kuongeza kuwa:
“ Kwa njia hiyo basi kila mtumishi wa ngazi husika awe mfano katika kusimamia utekelezaji wa mipango endelevu ya halmashauri kwa kuwafikia wananchi kwa muda uliopangwa.”
Alisisitiza kuwa lengo zaidi la Serikali ni kuhakikisha taifa linakuwa na chakula cha kutosha ili kuiondolea mzigo wa kuagiza chakula nje kwa ajili ya sehemu zinazokumbwa na njaa.
Akizungumzia kuhusu hali ya kilimo katika Wilaya ya Urambo, alisema siyo nzuri sana kwa sababu uzalishaji wa mazao kwa eneo ni mdogo, matumizi ya mbegu bora ni yako chini na matumizi ya mbolea kwa mazao ya chakula hayaridhishi.
Vilevile, Sitta, alisema wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto za bei za pembejeo za kilimo, uchache wa wataalamu wa ugani, mitaji midogo na kukosekana kwa mradi mkubwa wa umwagiliaji wa kiwilaya.
Katika kongamano hilo la siku mbili halmashauri hiyo ilitoa piki piki 10 kwa ajili ya wataalamu wagani wa kata 23 za wilaya hiyo ili kuwawezesha kufika na kutoa huduma kwa wakulima kwa muda uliopangwa.
Akikabidhi piki piki hizo kwa wagani hao, Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Anna Magowa amewataka kuzitumia kama changamoto ya kuleta mabadiliko katika kilimo na maisha bora kwa wakulima.

CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom