Spika Sitta alia na mafisadi wa bara la Afrika

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,792
287,994
Spika Sitta alia na mafisadi wa bara la Afrika

Na Leon Bahati

Mwananchi

UCHUNGUZI uliofanyika hivi karibuni umebaini kuwa mafisadi barani Afrika wanaiba fedha nyingi za serikali ambazo kiwango chake kinapita kile kinachotolewa na wahisani katika kusaidia bajeti za nchi husika, Spika Samuel Sitta amesema.

Sita alisema hayo jana kwenye mkutano wa nne wa Muungano wa Vyombo vya Fedha vya Mabunge ya Nchi za Afrika Mashariki (EAAPAC), unaofanyika jijini Dar es Salaam.

Sita alisema kuwa uchunguzi huo uliofanywa na vyombo huru vya kimataifa ulibaini kuwa mwaka 2006, fedha zilizoibwa na mafisadi katika serikali za Afrika ni Dola 20 bilioni za Kimarekani wakati misaada iliyotolewa ilikuwa Dola 18 bilioni za Kimarekani.

Akihojiwa na waandishi wa habari nje ya mkutano huo, Spika Sita alisema kuwa hiyo inaonyesha wazi kwamba kama siyo mafisadi, serikali nyingi za Afrika zingekuwa na uwezo wa kujitosheleza kibajeti, bila kuwategemea wahisani.

Kwa sababu hiyo alisema ni wajibu wa mabunge ya Afrika kuongeza juhudi za kuwabana mafisadi kwa kuwa bila kufanya hivyo, fedha nyingi za umma zitaendelea kuibiwa na nchi kuzidi kuzama kwenye wimbi la umasikini.

“Maana kama mianya hiyo haitazibwa, fedha za serikali zitakuwa kama zimebebwa kwenye wavu ambao unavuja kwenye matobo yake,” alisema Sitta.

Akihutubia kwenye mkutano huo, ambao unahudhuriwa na wajumbe kutoka nchi saba za Afrika, Sita alisema kuwa bunge la Tanzania lina kamati tatu ambazo zinafuatilia mfumo mzima wa matumizi ya fedha za serikali.

Alizitaja kuwa ni Kamati ya Hesabu za Serikali, Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa na Kamati ya Mashirika ya Umma. Alizielezea kuwa zimekuwa zikifanya uchunguzi wa kitaalamu pamoja na kushauri, ili kuepuka matumizi mabaya ya fedha.

Moja ya mambo yaliyosisimua kwenye mkutano huo ni wajumbe kutoka Uganda kumsifia Sitta kwa kumuelezea kuwa wanamtambua ameliwezesha bunge la Tanzania kukomaa kidemokrasia kwa kujadili mambo kwa uwazi.

Akitoa salamu za shukurani, mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya Bunge la Uganda, Nathan Nandala alisema kuwa mabadiliko aliyoyafanya Sitta ni makubwa katika kipindi kifupi chake cha uspika.

Sifa za Nandala zililenga katika ujasiri wa Bunge la Tanzania katika kujadili ripoti ya uchunguzi wa utoaji wa zabuni ya uzalishaji umeme wa dharura, iliyotolewa kwa kampuni tata ya Richmond Development Limited LLC, na kusababisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa pamoja na mawaziri wawili kujiuzulu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, John Cheyo (Bariadi Mashariki-UDP) alisema kuwa katika miaka ya karibuni serikali imeonyesha mafanikio katika kutumia fedha akiipa nguvu hoja yake kwa kutumia kigezo cha asilimia 70 ya halmashauri nchini kupata hati safi.

Lakini, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Dk. Wilbrod Slaa alitofautiana naye akisema kuwa madiwani wengi hawana elimu ya kutosha katika mambo ya fedha, jambo linalowafanya washindewe kuchambua taarifa za fedha.
 
Usanii mwingine bwana! Huyu Sitta yuko kimya kuhusu mapapa wa mafisadi ndani ya nchi yetu lakini anakuwa mkali kwa kuwavalia njuga mafisadi wa Afrika!! UPUUZI MTUPU!!!
 
Usanii mwingine bwana! Huyu Sitta yuko kimya kuhusu mapapa wa mafisadi ndani ya nchi yetu lakini anakuwa mkali kwa kuwavalia njuga mafisadi wa Afrika!! UPUUZI MTUPU!!!

Six anafanana na bosi wake Jk kukimbilia kusuruhisha matatizo ya nchi za nje wakati kwake kuna teketea! sijui wanataka sifa?
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom