Spika aokoa jahazi la serikali kuhusu hoja ya Mbunge Selelii

Ng'wanza Madaso

JF-Expert Member
Oct 21, 2008
2,268
333
Spika aokoa jahazi la serikali kuhusu hoja ya Mbunge Selelii

Na Exuper Kachenje, Dar

WIKI mbili baada ya Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii (CCM), kuwasilisha hoja kuituhumu Wizara ya Miundombinu kwa kuanza kutumia fedha zilizoko katika bajeti ya mwaka huu wa fedha (2009/10) kabla ya kuidhinishwa na Bunge, Spika wa Bunge, Samuel Sitta amesema licha ya udhaifu uliojitokeza, katiba ya nchi haikukuikwa.


Jana asubuhi baada ya kipindi cha maswali na majibu Spika Sitta alitoa mwongozo kuhusu hoja hiyo ya Selelii kuwa tatizo lililotokea ni Wizara ya Miundombinu kutumia majina mawili tofauti kwa Idara ya Barabara bila kulijulisha Bunge.


Ikionekana kana kwamba mbunge huyo angewekewa viunzi na kupata adhabu kwa tuhuma hizo, Spika Sitta alisema, kimsingi Selelii alikuwa sahihi kwa kuwa hoja yake ni ya msingi.


“Ila baada ya kupitia maelezo yote haya nashauri tu kwamba, fedha zilizotumika ni sahihi na ziliidhinishwa na Bunge, ingawa hoja ya Mheshimiwa Selelii ni ya msingi,” alisema Sitta.


Alibainisha kuwa mbunge huyo alisoma kitabu cha miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha wa 2009 ukurasa wa 489, kifungu 4489 kinachoonyesha kuwa miaka ya nyuma hakuna fedha zilizotengwa kwa ajili ujenzi wa barabara hiyo na kwamba hayo ni makosa ya uchapishaji.


“Kuhusu barabara ya Chalinze, Segera, Tanga, waheshimiwa wabunge hii ripoti nitaigawa kwenu mkaisome kwa sababu ni ndefu na inaelezea mambo mengi. Lakini kwa kifupi ni kwamba, kuanzia mwaka 2006, zimekuwa zikitengwa fedha za matengenezo ya barabara hii ya Chalinze-Segera,” alisisitiza.


Alibainisha kuwa katika mwaka 2007/08 jumla ya Sh10 bilioni zilitengwa na mchango mkubwa ukitokana na wahisani ambao ni Danida na Sh 17 bilioni zilitengwa katika mwaka 2008/09 ambapo jumla ya fedha za ndani zilizotengwa na kuidhinishwa na Bunge zilikuwa Sh50 bilioni na kueleza kilichotokea.


“Tatizo lililotokea ni kwamba, Wizara ya Miundombinu kulikuwa na idara inayoshughulikia barabara ikiitwa ‘Roads Division' kitengo cha barabara na baadaye wizara hiyo ilibadili `Roads Division` na kuuita 'Transport Infrastructure Division'. Kwa hiyo, miaka yote tuliyokuwa tunaidhinisha makadirio haya, tulikuwa tunaidhinisha kupitia eneo linaloitwa Roads Division,”alifahamisha Spika.


Alikumbusha kuwa mkutano wa 12 wa bajeti ulipitisha makadirio hayo na kufafanua, “Ni kwamba katika kitabu zilitokea Sh332,857,400,000, badala ya Sh428,857,400,000, zilizoidhinishwa, hivyo uamuzi wangu, pamoja na kwamba kulikuwa na utata baina ya fedha zilizopitishwa na zilizoonekana kwenye kitabu, hakuna kasoro yoyote ya uvunjaji wa sheria wala katiba.”


Spika Sitta alifafanua kwamba: “Matokeo yake vitabu vilivyoidhinishwa vya 2009/10 kwenye Idara ya Transport Infrastructure Division, ikaonekana kwa miaka iliyopita haikuwa na makadirio, hivyo haimaanishi kuwa Bunge halijaidhinisha fedha, bali ziliidhinishwa chini ya 'Roads Division'”.


Alikumbusha kuwa katika bajeti yake kwa mwaka 2007/08, ilitenga Sh 332,857,400,000, lakini fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa mwaka huo zilikuwa ni Sh428,857,400,000, kiasi kilichoongezwa kupitia mkutano huo wa dharura na kuidhinishwa na Serikali.


“Kwa kuwa utata huu unatokana na mabadiliko ya muundo, naishauri serikali ili tusirudie matatizo kama haya, kunapotokea mabadiliko ya muundo kama haya, hasa mabadiliko yanayotokana na kutengwa fedha kwa miradi mikubwa ni vema Bunge likafahamishwa na kupokea ili iwepo taarifa kamili na kuwa na hakika kwamba fedha zote zilizotengwa zimeidhinishwa na Bunge.


Waheshimiwa wabunge huo ndio uamuzi wangu hakuna utata wowote sasa,” alisema Spika.


Selelii alipoulizwa na Mwananchi iwapo ameridhika na maelezo ya Spika, alionyesha kutoridhika, lakini akasema, “Kwa vile kuna kipengele cha kanuni za Bunge kinachotaka mtu kuheshimu maelezo ya kiti cha Spika, mimi nimekubali kuridhika na maelezo ya Spika.”



Hata hivyo, alipobanwa na maswali mengi ya kumtaka afafanue juu ya kauli hiyo, aliwataka waandishi wa habari kuwa na subira kwa sababu leo wabunge watajadili bajeti ya Wizara ya Miundombinu, hivyo wawe na subira kwa sababu mengi yatawekwa wazi.

SOURCE: Mwananchi
 
Sitta anaiogopa serikali..ule ulikuwa mkwara tu...hatujapata bunge madhubuti hapa tanzania kwakweli
 
Back
Top Bottom