Soma Mkasa wa kusikitisha kutoka Moshi....

macho_mdiliko

JF-Expert Member
Mar 10, 2008
21,770
39,540
Wauguzi KCMC, Mawenzi wahojiwa kwa mauaji

WAUGUZI wawili, mmoja wa Hospitali ya Rufaa KCMC na mwingine wa Hospitali ya Mkoa Kilimanjaro, Mawenzi, wanahojiwa na polisi kwa tuhuma za kula njama na kupanga mauaji ya msichana mmoja, mkazi wa Kibosho.
Habari za uhakika zilizolifikia gazeti hili jana, zilisema ingawa mauaji hayo yanaaminika kutokea kati ya Desemba mwaka jana na Januari mwaka huu, lakini siri ya mauaji hayo imefichuka Julai mwaka huu.

Taarifa hizo zilidai, polisi wamekwishaandikia ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kufanya taratibu za kisheria kufukuliwa kwa miili ya wanawake watatu ili ifanyiwe vipimo vya vinasaba (DNA), kuwatambua.

Polisi wanaamini moja ya maiti hizo zilizookotwa maeneo tofauti Wilaya ya Moshi na Hai, inashukiwa ni ya mwanamke aitwaye Rufina Joseph, ambaye ametoweka miezi saba sasa. Maiti hizo zilizikwa na manispaa kwa kukosa ndugu.Wauguzi hao wawili walikamatwa Julai 6, mwaka huu na kuwekwa mahabusu kwa wiki moja hadi Julai 13, walipoachiwa kwa dhamana licha ya kesi za mauaji kutokuwa na dhamana hata kama iko hatua za awali za uchunguzi.

Chanzo kimoja kilidokeza kuwa, siri ya mauaji hayo ilifichuliwa na dereva teksi mmoja ambaye alifahamu mipango yote ya suala hilo, ambalo sasa linawaumiza vichwa wapelelezi wa polisi.

Sakata lilianza mwanzoni mwa mwaka 2010
Taarifa za uhakika zilisema mmoja wa washukiwa ambaye ni muuguzi Idara ya Utabibu KCMC (jina tunalo), alipata ‘dili’ ya Wazungu waliokuwa tayari kumtumia fedha, lakini sharti likiwa ni kuthibitisha kuwa na mtoto mchanga.
Kwa kuwa muuguzi huyo alikuwa hawezi kupata mtoto, alianza harakati za kutafuta mtoto mchanga hata ikibidi wa kununua na mipango hiyo akimshirikisha rafiki yake, ambaye ni muuguzi wa Wodi ya Wazazi Hospitali ya Mawenzi.

Wauguzi hao inadaiwa walikwenda kuzungumza na wazazi ambao walikuwa na watoto wachanga maeneo ya Uchira na Uru Moshi Vijijini, ikiwamo mama mmoja aliyekuwa amejifungua watoto mapacha, lakini waligoma kumpa mtoto.Katika kuhangaika huku na kule bila mafanikio, muuguzi huyo wa KCMC akishirikiana na dereva teksi aliyemwajiri, walipata taarifa kuwa yuko msichana mwenye mimba ya miezi minane eneo la Kibosho.

“Kwa hiyo yule muuguzi wa KCMC naye akawaarifu watumishi wenzake kuwa, ana mimba ya miezi minane sambamba na ya yule dada wa Kibosho, ili atakaposingizia amejifungua ifanane na yule wa Kibosho,” kimedokeza chanzo chetu.
Msichana huyo alipata mimba hiyo kwa bahati mbaya na wazazi wake walikuwa wakigombeza kutaja mhusika, ili aweze kubeba gharama za matunzo. hivyo kitendo cha kupata msamaria kilimpa faraja.

Inadaiwa wauguzi hao kwa kushirikiana na dereva teksi huyo walimghilibu dada huyo ambaye alikuwa njiapanda na kukubaliana kuwa baada ya kujifungua, muuguzi wa KCMC angemchukua mtoto na kumsaidia kumlea.
Baada ya makubaliano hayo, muuguzi huyo wa KCMC aliwaarifu wafanyakazi wenzake kuwa ni mjamzito mwenye mimba ya miezi minane na kwamba anakaribia kujifungua lakini asingejifungulia KCMC, bali Hospitali ya Kibosho.
Msichana huyo alijifungua Aprili mwaka jana kwa operesheni kwenye hospitali hiyo na kukaa siku nne, ndipo wauguzi hao walipoomba kwa maandishi aruhusiwe kurudi nyumbani.

Madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Kibosho walikubali ombi hilo na kukaa kwa siku moja kwa muuguzi wa Hospitali Mawenzi eneo la Soweto mjini Moshi, siku iliyofuata alihamishiwa nyumbani kwa yule wa KCMC.
Baada ya kufika huko na kukaa mwezi mmoja, muuguzi huyo wa KCMC alimshawishi msichana huyo kumwachia mtoto kwa ahadi kwamba akamtafutie kazi Dar es Salaam.

Inadaiwa kuwa mwanamke huyo alikubali na kumwacha mtoto wake mchanga kwa muuguzi huo wa KCMC, ili amsaidie kumlea na yeye kupelekwa Dar es Salaam ambako alitafutiwa kazi ya kuuza baa moja (jina la baa tunalo).

Katika kipindi chote hicho cha mwezi mmoja alichokaa na muuguzi huyo wa KCMC, mama wa mtoto alikuwa akitambulishwa kama mfanyakazi wa ndani.
Muuguzi KCMC alipongezwa kwa kujifungua salama
Wakati wote, muuguzi wa KCMC akawataarifu watumishi wenzake na majirani kuwa amefanikiwa kujifungua salama na kuwaonyesha mtoto na alipokea pongezi na zawadi kutoka sehemu mbalimbali.
Kubwa zaidi ni kuwa muuguzi huyo akaendelea kumnyonyesha mtoto kama wa kwake kuanzia Aprili hadi Desemba 2010, hakuna aliyeshuku kuwa mtoto huyo siyo wake.

Chanzo cha mgogoro wa mtoto
Desemba kama ilivyo ada kwa wenyeji wa Mkoa wa Kilimanjaro, mama wa mtoto alirejea Moshi kwa ajili ya Sikukuu ya Krismas na mwaka mpya.Taarifa za polisi zilidai kuwa mama wa mtoto alifika nyumbani kwa muuguzi huyo na kumwomba ampatie mwanaye, ili kwenda naye Kibosho kwa bibi yake kumsalimia, lakini muuguzi alimbadilikia na kumweleza wazi kuwa hakuwa na mtoto pale, jambo lililomfanya kuamini kuwa pengine ni utani, kwani hakuamini angegeukwa kiasi hicho kwa damu yake.

Inadaiwa kitendo cha mama wa mtoto kushikilia msimamo wa kutaka kuondoka na mtoto wake, kilimweka njiapanda muuguzi yule wa KCMC akijiuliza jinsi ya kujieleza kwa wafanyakazi wenzake na jamii.
Taarifa hizo zinadai siku moja kabla ya mama wa mtoto kutoweka katika mazingira ya kutatanisha, muuguzi yule wa KCMC na mama wa mtoto walionekana wakinywa pombe nyingi na vijana wasiofahamika mtaani walipokuwa wakiishi.

Kufichuka kwa siri ya mauaji
Kitendo cha muuguzi wa KCMC kuendelea kumnyonyesha mtoto yule licha ya taarifa za mama yake kurejea Moshi, kilimshitua dereva teksi ambayo alimhoji kulikoni, lakini muuguzi akamtaka kutofuatilia mambo ya watu.
Baada ya kuonekana akifuatilia sana huku akihoji alipo mama wa mtoto, muuguzi yule alimweleza dereva teksi kwamba amemtafutia kazi nyingine katika baa moja iliyopo Korogwe, mkoani Tanga.

Kutokana na mashaka aliyokuwa nayo, dereva yule alifuatilia hadi Tanga na kugundua kulikuwa hakuna baa yenye jina hilo alilotajiwa, ndipo alirejea Moshi na kumweleza muuguzi huyo kwamba baa aliyomtajia haipo.
Muuguzi yule alienda mbali na kumtaka dereva huyo kumkabidhi funguo za gari aliyokuwa akiendesha. Muuguzi huyo anamiliki teksi mbili.Kitendo hicho kinadaiwa kilimchukiza dereva yule ambaye baadaye aliamua kufichua siri ya tukio hilo kwa mama mzazi wa mtoto aitwaye, Magdalena Mwacha, ambaye baadaye alitoa taarifa polisi.

Mama mzazi asimulia mwanaye alivyotoweka
Akizungumza katika ofisi za Mwananchi Moshi wiki iliyopita, Magdalena alisema baada ya mwanaye kujifungua, alipewa taarifa na jirani yake kuwa asiende tena kumchukua Hospitali ya Kibosho kwani amechukuliwa na wauguzi hao.
“Nilisisitiza nataka nimwone mjukuu wangu, ndipo yule jirani aliponipeleka nyumbani kwa yule nurse (muuguzi) wa KCMC na kweli nilimkuta mjukuu wangu, lakini mwanangu sikumwona wakaniambia atarudi tu,” alisema na kuongeza:
”Baada ya kukaa hadi saa 12:30 jioni bila kumwona mwanangu, niliamua kurudi Kibosho lakini baada ya mwezi nilirudi kwa yule muuguzi na kumkuta akiwa na mjukuu wangu tu mama yake hakuwepo.”

Mama huyo alidai kuwa siku moja Desemba, mwanaye alimpigia simu kuwa angekuja likizo ya Krismas na siku aliyosafiri alimjulisha pia, lakini akamwambia kuwa angepitia mahali ingawa hakumwambia sehemu yenyewe.
“Baada ya kutomwona hadi Januari niliamua kutoa taarifa polisi, ambao waliwakamata wale wauguzi na kuandikisha maelezo yao na kuwaachia, huku wakiniambia niendelee kumtafuta mtoto wangu,” alisema.

Alisema Juni 29, mwaka huu alipokea simu kutoka kwa dereva teksi akimwambia aende kumwona ili wazungumze kuhusu kutoweka kwa mwanaye, aliitikia wito huo na kwenda Moshi mjini na kukutana na dereva huyo.
“Aliniambia kuwa Rufina alifika nyumbani kwa yule muuguzi wa KCMC Desemba akimtaka ampe mtoto wake, lakini alikataa na kumchukua na kwenda kumnyesha pombe na baadaye kukodisha watu wa kumuua,” alisema.

Kauli ya RPC Kilimanjaro
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Absolom Mwakyoma, alilithibitishia kuhojiwa kwa wauguzi hao na dereva teksi mmoja na kwamba, hivi sasa wako nje kwa dhamana ya polisi.“Ni kweli hilo jambo hilo lipo, lazima tuthibitishe kama kweli huyo mwanamke ni marehemu ili sasa tuweze kuunganisha ushahidi tulionao, njia pekee ni kufanya vipimo vya DNA ili tusikurupuke,” alisema Mwakyoma.

Kwa mujibu wa Mwakyoma, zipo maiti za wanawake watatu zilizookotwa ambazo utaratibu unafanyika ili zifukuliwe na kufanyiwa vipimo vya DNA, ili kuthibitisha kama upo mwili wa mwanamke huyo aliyetoweka."Kama tutathibitisha kuwa mwili ule ni wa Rufina, bado jukumu letu lingine litakuwa ni ku establish (kutafuta chanzo) kama sababu za kifo ili sasa tuweze kuunganisha hadithi hizo ulizozisikia,” alisema Mwakyoma.

From mwananchi
 
Aisee kama hiki kisa ni cha kweli basi dunia imefika ukingoni...
 
very sad. Nimekuwa nikisema mara zote wengi wa manesi wetu ni wauaji nikapingwa sana na baadhi ya madaktari waliomo humu JF. Oneni sasa mtu badala ya kufanyiwa maombi azae ananyanganya mtoto na kumuua mama yake. Mungu anaona na hakika mwisho wa kutenda ubaya wa huyu nesi na wenzake umefika.
 
Du imezidi waungwana at least haki itendeke this time. . .huyo nurse afuatiliwe kwa ukaribu ni hatari anaweza kupanga tukio jingine baya maana ni kama anamgongo wa mkubwa wa dola why atoke kwa dhamana while bado wanachunguza na ni case ya mauaji?
 
Duh.. hii inapita simulizi la sinema!!

Kuna mbili zilitokea Marekani, Mama aliyetaka mtoto aliamua kumuiba toka tumboni kwa kumkatakata mjamzito tumboni na kuondoka na mtoto yaani nilipoisikia hadi mwili ulisisimka kwa jinsi watu wanavyoweza kufanya unyama wa kutimiza walitakalo, haukupita muda mrefu nikasikia tena incident nyingine iliyoshabihiana na hiyo kama nakumbuka vizuri katika case zote mbili wajawazito walifariki baada ya kupoteza damu nyingi sana.
 
Inasikitisha,
Lakini nadhani Tanzania inabidi tuwe na utaratibu wa kuweza kuadopt watoto, kwani kuna haja maana kuna watu wanauwezo wa kulea watoto ila hawana watoto na kuna watu hawana uwezo wa kulea watoto ila wanao watoto. Hili suala inabidi liangaliwe kwa upana, pamoja na adhabu anayoweza kupata muuaji.
 
Inasikitisha,
Lakini nadhani Tanzania inabidi tuwe na utaratibu wa kuweza kuadopt watoto, kwani kuna haja maana kuna watu wanauwezo wa kulea watoto ila hawana watoto na kuna watu hawana uwezo wa kulea watoto ila wanao watoto. Hili suala inabidi liangaliwe kwa upana, pamoja na adhabu anayoweza kupata muuaji.
Mkuu... nadhani adoption sio mwiko Tz. Kwa mfano mtu ukienda kwenye vituo vya kulelea watoto yatima kwa nia ya ku-adopt hutanyimwa.
 
Mimi ndio maana nasema siku ikitokea vita nchi hii, itakuwa janga, sishangai sana ,
kwani nchi hii inawatu wenye roho ngumu kinoma, angalia tu:
1. Ishu ya vibaka wanapochomwa moto.
2. Vibaka wavyoua wakitaka kupora simu na boda boda.
3. Watu wanavyowatesa wafanyakazi wao wa ndani, watoto wa kufikia
4. Ufisadi uliopitiliza.
Na mengineyo, haya yote yanahitaji roho ya paka kuyatenda.
 
Hata wauguzi jamani! hii inaumiza sana sijui kwanini watu tunakosa tabia za kibinadamu.
 
mwandishi anaelezea hadi jinsi hao wanawake wawili walivyokuwa wanajibizana wakiwa peke yao, je hapa kweli hatudanganywi??
 
Hadithi hii ina maswali mengi. Polisi wanahangaika kwendapima maiti DNA kwanini wasipime DNA ya mtoto aliyeko na kulinganisha na ya Muuguzi na pia bibi alopotelewa na mwanaye. DNA ya mtoto na nurse zikikosa mahusiano ni moja kwa moja nurse anapaswa kusema mama wa mtoto yuko wapi. Pila DNA ya mtoto ikionyesha uhusiano na ya bibi ni wazi atakuwa mjukuu wake. Yatosha kumsweka ndani muuguzi mpaka ataje mama wa kweli wa mtoto
 
mwandishi anaelezea hadi jinsi hao wanawake wawili walivyokuwa wanajibizana wakiwa peke yao, je hapa kweli hatudanganywi??
Hata mimi nimeona kuna missing links nyingi ambazo mwandishi haja connect the dots.
1.Story ilianza na ‘dili' ya Wazungu' ili atumiwe pesa kwa shurti la kuwa na mtoto, how did it go maana mtoto si alipatikana.
2. Muuguzi ambaye hajawahi kuzaa, kajitia ana mimba, hayo maziwa ya kunyonyesha yatoke wapi?, japo nakubali ziwa likinyonywa sana hatimaye hutengeneza maziwa, lakini initial stage ni lazima vile vichocheo viwepo!.
3. Taarifa zote za kiofisi kwa muunguzi kuomba maternity ya uwongo si zipo?, taarifa za addmission, delivery na discharge pia si zipo, unless wauguzi wale waliandikisha majina ya mama bandia, hivyo paper work yote ikionyesha mtoto ni wa muuguzi na sio wa mama halisi.
4. Mama mzazi baada ya kuona mwanae ametoweka, mbona hajamdai mjukuu wake?.
5. Dereva teksi ndio kafichua siri baada ya kufutwa kazi?.
6. Polisi hawajasema mtoto ni wa nani, kama muuguzi anadai ni wa kwake, ilikuwa ni kazi ya polisi kupitia hiyo hiyo forensic yao kuestablish mama halisi wa mtoto, na wakikuta mwenye mtoto siye mama halisi, ingetosha kumfanya ni suspect.
Hiki kisa kinaonekana ni cha kweli bli bado kazi ya kuunganisha hizo missing links kibao.
 
Pasco nashukuru nawe umeyaona maswali kibao kwenye hadithi hiii. Bado mimi haijaniingia akilini eti hata binti mwenyewe alitafutiwa tu kazi ya bar DAR mapema akaishia na kumuacha mtoto akinyonyeshwa na muuguzi ambaye hakuwahi kuwa na mimba. Maziwa kayapata wapi muuguzi huyu bila uhusika wowote wa mimba?
Halafu binti siku zote kapiga tu simu mara moja kwa mamaye eti nakuja Krisimasi na mjukuu?!
Anafika nyumbani anaambiwa mtoto humpati na anaendelea kuishi safi tu mpaka mkakati wa kwenda mnywesha pombe unaandaliwa na kutekelezwa?
Wazungu walihitaji tu kujua ana mtoto na tayari ingeshafahamika mradi uliendelea vipi lakini kimya.
Huwezi kutangaza una mtoto ni wako kwa uma huku bibi mwenye mjukuu wake naye ajulishwa waziwazi kuwa mwanaye kajifungua salama na mtoto ni huyu atunzwa hapa naye awe na uhuru wa kutangaza kwa marafiki na ndugu kuwa muuguzi fulani ndo atulelea mjukuu halafu bado ibaki siri ya muuguzi.
Muuguzi anazuka tu ghafla jamani nina mimba ya miezi nane na wote wanamuelewa na kukubali bila mshangao. Inakuwa kama kasema jamani nimenunua mimba ya miezi nane? Kwa wazijuazo mimba, kwa wengi tangu mwezi wa 5 siyo ya kutangaza tena bali yaonekana kwa wengi. Bado nashangaa kama ni kweli
 
Back
Top Bottom