SMZ kubadili kanuni za usafiri majini

Kakke

JF-Expert Member
Dec 4, 2010
1,883
1,482
SMZ kubadili kanuni za usafiri majini
Tuesday, 17 April 2012 21:45

Aidan Mhando
WAZIRI wa Miundombinu na Mawasiliano wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hamard Masoud Hamard amesema Serikali inaandaa mpango wa kufanya marekebisho ya Kanuni za usafiri wa majini ili kutoa nafasi kwa Serikali kusimamia na kudhibiti upangaji wa njia unaofanywa na vyombo binafsi vya usafiri kiholela.

Waziri Hamard aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza katika kipindi cha dakika 45 kinachotangazwa na ITV, ambapo alibainisha mambo mbalimbali yanayofanyiwa kazi na Serikali ya Zanzibar katika masuala ya usafiri wa majini.

Alisema baada ya vyombo vingi vya usafiri vya majini hususani kwa vyombo binafsi ambapo wamiliki wake hutumia vyombo vyao kimasilahi zaidi bila kujali kwamba wananchi wanapata shida ya usafiri katika baadhi ya maeneo, Serikali imeamua kufanya marekebisho ya kanuni mbalimbali za usafiri wa majini ilikuhakikisha wanadhibiti hali hiyo.

“Kumekuwa na shida ya usafiri hasa katika eneo la Pemba ambapo wakati mmoja boti zinaweza kwenda katika eneo hilo bila kuwa na ratiba maalumu jambo ambalo wakati mwingine linasababisha ukosefu wa uasafiri kwa muda mrefu na kwamba wananchi wanalazimika kusubiri kwa muda mrefu jambo ambalo hatupendezwi nalo kama serikali,” alisema Hamard na kuongeza:

“Serikali ya Mapinduzi kwa kuliona jambo hilo tumeamua kuzipitia tena kanuni zetu za usafiri wa majini na kwamba tutazifanyia marekebisho ilikuhakikisha Serikali inapata nguvu ya kudhibiti hali hiyo,” alisema.
Aidha Waziri Hamard alifafanua kwamba Serikali inafanya mpango wa kununua meli kubwa ambayo itatumika kama sehemu ya kupunguza tatizo la usafiri wa majini Zanzibar.

“Kwa sasa tumebakiwa ma meli moja baada ya meli yetu nyingine kuwa imechakaa kwa kiasi kikubwa ambapo kwa kutambua umuhimu wa chombo hicho Serikali imeamua kuagiza meli nyingine mpya ambayo itachangia kuondoa matatizo ya usafiri,” alisema
 
Back
Top Bottom