Slaa kufyeka wizara, kufuta ukuu wa Mkoa
Slaa kufyeka wizara, kufuta ukuu wa Mkoa
Imeandikwa na Halima Mlacha; Tarehe: 26th August 2010
MGOMBEA Urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Wilbroad Slaa, amesema iwapo atashinda kiti cha urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, ataunda serikali tatu ikiwamo ya Tanganyika.
Mwanasiasa huyo pia amesema, atapunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri, Makatibu Wakuu na manaibu wao, na atafuta cheo cha ukuu wa mkoa.
Slaa alisema, cheo cha ukuu wa mkoa hakina maana kwa kuwa viongozi hao wanatoa ushauri tu, wapo wengi na wanatumia magari, nyumba na fedha za serikali kwa kazi hiyo.
Kwa mujibu wa Slaa , Baraza la Mawaziri kwa sasa lina mawaziri 45 ambao ni wengi kulinganisha na idadi ya watanzania.
Alisema, kuna nchi nzima ina wananchi milioni 45, na ametoa mfano kuwa, katika nchi ya Uingereza kuna wananchi milioni 300 na mawaziri 14.
Sioni kazi ya Manaibu Waziri wanakuwa wengi tu na kutumia magari ya gharama kubwa VX zenye thamani ya Sh milioni 200 bila kazi yoyote ya maana,
Alisema atapunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri na kufuta baadhi ya vyeo ili kupunguza matumizi makubwa ya Serikali ambayo robo tatu ya bajeti ya nchi hugharamia uendeshaji wa Serikali hali ambayo imekuwa ikididimiza zaidi nchi kiuchumi na ataanza kupunguza utitiri wa ofisi zisizo za lazima.
Tutaweka mfumo katika Serikali za mitaa na mikoa ambao utawafanya viongozi kuwajibika, tutatumia baraza la madiwani kuwafikia wananchi na kikubwa meya wa madiwani atachaguliwa na wananchi na si kama mfumo wa sasa uliopo, alisema.
Pia amesema, bado Katiba ya Tanzania imeonekana kuwa kikwazo kikubwa katika utendaji wa viongozi nchini hivyo serikali yake itaibadili Katiba hiyo na kutoa madaraka zaidi kwa wananchi na kufuata mfumo wa uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa zamani wa Zanzibar Abeid Amani Karume.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Habarileo Dar es Salaam jana, alisema kwa sasa hali ya muungano iliyopo ya kuwa na serikali mbili haijawa na ufumbuzi wa kutosha kwa kuwa, serikali moja ya umoja imeizidi ukubwa serikali nyingine hivyo inafaa kuwa na serikali ya Tanganyika ili kuleta usawa.
Sisi Chadema kama wapinzani hatutaki muungano uvunjike tunataka udumu, lakini hatuoni sababu ya kuwa na serikali mbili za nini? Sasa hapo muungano uko wapi, na hali hii ikiendelea hata kero za muungano haitokuwa rahisi kuzitatua, ndiyo maana sera yetu tutakayokuja nayo itakuwa na mfumo wa serikali tatu, alisema Dk Slaa.
Alisema katika Serikali hizo tatu mbili zitakuwa kubwa na moja ya umoja itakuwa ni Serikali ndogo ambayo hapo baadaye chama hicho kitakuja na fomula ya namna ya kuisaidia Serikali hiyo katika kushughulikia masuala ya muungano.
Alitoa mfano kuwa, hali ya sasa visiwani Zanzibar ya makubaliano ya Serikali ya Umoja na kubadilishwa kwa Katiba ya visiwani humo.
Kama Zanzibar ni nchi ya muungano na Katiba yao inatambua Serikali ya Umoja basi na Katiba ya Muungano ingebadilishwa na kuitambua serikali hiyo,
Alisema, iwapo Chadema kitashinda katika uchaguzi huo, wanafikiri kubadili mfumo wa uongozi uliopo kwa kuanza na Katiba na kuondoa mamlaka makubwa aliyopewa Rais.
Alisifu mfumo wa Mwalimu Julius Nyerere ambao ulishirikisha wananchi na ulijikita zaidi katika kuondoa maadui wakubwa ambao ni ujinga, umasikini na maradhi hali ambayo sasa imebadilika.
Kwa mujibu wa Slaa, ameongezeka adui mmoja, ambaye ni rushwa na akadai kwamba hali hiyo imesababishwa na uongozi mbovu.
Alisema kikubwa ambacho Chadema itazingatia ni mfumo mzuri wa uongozi ambao wamefanyiwa uchunguzi wa kina, mfumo ambao utatumia utajiri wa rasilimali za Tanzania kutunga sera, mipango na mikakati kwa kuisimamia ipasavyo ili kukuza uchum na kuiletea maendeleo nchi hiyo.
Katika uongozi wa Mwalimu Nyerere alijitihadi kutumia mfumo wake wa uongozi na kupeleka timu ya watanzania nje kupatiwa utaalamu wa kutengeneza magari na hadi sasa yapo magari yaliyotengenezwa Tanzania tena kupitia rasilimali yetu ya chuma, ila kwa sasa inasikitisha kuona mfumo wa Mwalimu kama vile Azimio la Arusha umefutwa, alisema.
Akizungumzia suala la elimu ya mgombea wake mwenza Said Mzee Said, ambaye ana elimu ya shule ya msingi, alisema haoni kama hilo ni tatizo.
Alisema, hata Katiba ya nchi inazungumzia wazi sifa za kiongozi kuwa ni umri, utaifa, awe na akili timamu na ajue Kiswahili au kingereza sifa ambazo mgombea huyo anazo.
Kwangu mimi sioni kama elimu ni kigezo kikubwa kwa kiongozi, wapo viongozi wengi tu hawakuwa na elimu kubwa na wameongoza vizuri kama vile Simba wa Vita (Rashid Kawawa) ambaye alikuwa Waziri Mkuu pamoja na Sokoine na wote hao wameacha historia nzuri juu ya uongozi wao, alisema.
Alisema iwapo katika uchaguzi huo atashindwa kwa haki atabaki kuwa mtanzania wa kawaida na kwamba, Januari mwakani atazunguka nchi nzima kuiandaa Chadema kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Lakini pia bado naweza kuwania nafasi ya Uspika kwani kwa mujibu wa Katiba Spika si lazima awe Mbunge,