Elections 2010 Slaa achukua fomu, hajathibitishwa

Slaa achukua fomu, hajathibitishwa
Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko; Tarehe: 10th August 2010 @ 08:35 Imesomwa na watu: 356; Jumla ya maoni: 1

MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbrod Slaa, amechukua fomu ya kugombea nafasi hiyo kabla chama chake hakijamthibitisha.

Slaa alichukua fomu jana katika Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dar es Salaam, amezunguka mikoa kadhaa nchini kusaka wadhamini, anatarajia kuthibitishwa kesho katika Mkutano Mkuu wa chama hicho.

Alikabidhiwa fomu hiyo jana na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Lewis Makame akishuhudiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Rajabu Kiravu. Dk Slaa alifuatana na viongozi wa juu wa chama hicho na wafuasi kadhaa ambao waliingia kimya kimya katika ofisi za NEC.

Akizungumza baada ya Slaa kuchukua fomu, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema kwa mujibu wa utaratibu ndani wa chama hicho, hawaangalii kura bali wanateua mgombea kutokana na utafiti ndani ya chama na matokeo ya utafiti huo ndiyo yanayowaongoza kumpata mgombea huyo.

Alisema baada ya utafiti wao wa kumpata mgombea, ndipo anathibitishwa na Mkutano Mkuu utakaopitisha pia Ilani ya chama ambayo itatoa mwelekeo wa watakachofanya ikiwa watashinda katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 31 mwaka huu.

Mbowe alipotakiwa kueleza ana uhakika gani kuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu watamthibitisha Slaa, alisema "usitukane mamba kabla hujavuka mto" na kuondoka, bila ufafanuzi.

Kwa mujibu wa ratiba ya Chadema iliyotolewa na Katibu wa Kamati ya Taifa ya Uchaguzi, John Mnyika, Kamati Kuu ya Chadema inatarajiwa kukutana leo na kuteua majina ya wagombea ubunge na kuandaa ajenda za Baraza Kuu za kesho na Mkutano Mkuu kufanyika kesho kutwa.

Kuhusu Slaa kuchukua fomu kabla ya kuidhinishwa, Mnyika alifafanua kuwa Nec hukabidhi fomu kwa mgombea aliyependekezwa na chama kuwania nafasi hiyo ya urais na kukumbushia kuwa Kamati Kuu ya Chadema iliyokutana Julai 20 mwaka huu, ilimpendekeza Slaa kuwa mgombea pekee.

Slaa alikuwa na mgombea mwenza wake, Said Mzee Said. Alisema malalamiko yanayotolewa na CCM kuwa chama hicho kimeanza kampeni mapema si ya kweli kwa kuwa yeye alikuwa akitafuta wadhamini na hivyo alilazimika kujitangaza.

"Sisi bwana hatufanyi kampeni, lakini katika kipindi hiki cha kutafuta wadhamini, chama chochote hakiachi kujitangaza, kwani kudhaminiwa ni lazima ujieleze ili watu wakuelewe na kukufadhili, hata wao CCM mbona katika utaratibu wao walijitangaza katika mikutano ya hadhara?" alihoji.

Akizungumzia suala hilo, Makame alisema Tume hiyo haijapata malalamiko rasmi kutoka chama chochote zaidi ya kusikia au kusoma katika vyombo vya habari, na kusema wao hawawajibiki mpaka hapo watakapotangaza rasmi muda wa kuanza kampeni Agosti 20 mwaka huu.

"Sisi hatujapata malalamiko rasmi kutoka chama chochote, ikiwa tutapata malalamiko hayo tutayafanyia kazi, ingawa sasa kabla ya kutangaza muda wa kampeni kuanza, ni vigumu kuwachukulia hatua," alisema Makame.

Alisema tayari vyama vyote 18 vimesaini maadili ya uchaguzi ili kutunza maadili katika uchaguzi wa mwaka huu, kwani wakati wa kuchukua fomu hupewa pia kitabu kinachoelezea maadili ya uchaguzi.

Wakati huo huo, Fahmi Dovutwa wa chama cha United People's Democratic Party (UPDP) akiwa na mgombea mwenza Hamad Mohamed Ibrahim, alichukua fomu za kugombea urais katika ofisi cha Tume hiyo.

source:HabariLeo | Slaa achukua fomu, hajathibitishwa

inahitaji hatua madhubuti ili kuimarisha demokrasia ndani ya chama hiki vinginevyo kinakaribisha ukosoaji usio wa lazima..... wengi wataona kuwa mkutano mkuu ni ruber stamp tu, kamat kuu ilikuwa na mtu wao tayari...

nawasilisha

Upumbafu wako tu
 
Back
Top Bottom