Siri zaanza kuvuja rushwa kamati za bunge

only83

JF-Expert Member
Oct 15, 2010
5,343
2,525
  • Mtandao wa wafanyabiashara wahusishwa, Kamati ya Maliasili, Mazingira yaguswa

Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira aliyejitambulisha kuwa ni mpinga vitendo vya rushwa, ameamua kuandika makala hii kueleza baadhi ya vitendo vya rushwa ndani ya Kamati hiyo. Hii ni sehemu ya makala ya mbunge huyo ambaye kwa sasa tunalihifadhi jina lake.


UTANGULIZI

Tarehe 28 Julai 2012, Bunge la Tanzania liliingia katika historia baada ya Spika Anne Makinda kutangaza kuivunja Kamati ya Nishati na Madini pamoja na kamati nyingine zinazotuhumiwa kwa rushwa.

Spika alifikia hatua hiyo baada ya kuwapo kwa harakati za wafanyabiashara wa sekta ya mafuta kufanya mipango kwa zaidi ya wiki mbili za kuwashawishi wabunge washinikishe kujiuzulu kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, na Katibu Mkuu Eliakim Maswi kwa kile kinachodaiwa kutoa zabuni kwa kampuni ya Puma Energy ya kuiuzia mafuta Tanesco kwa ajili ya mitambo ya umeme wa dharura ya IPTL. Harakati zililenga wabunge wengi wenye ushawishi bungeni, wakianzia na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini.

Kutokana na harakati hizo, Kamati ya Wabunge wa CCM ilikaa mapema wiki hiyo kumuhoji Waziri Muhongo.
Katika utetezi wake, Waziri Muhongo pamoja na Katibu Mkuu Maswi – kwa nyakati tofauti – walitoa shutuma nzito kwa wabunge kuwa wamehongwa na kampuni za mafuta, ili wazitetee na ziendelee kuiuzia mafuta mazito Tanesco pamoja na kushinikiza kurejeshwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, William Mhando, ambaye ni mshirika wa kampuni hizo.
Katika utetezi wake, Profesa Muhongo alieleza kwamba kumekuwa na kampeni hizo chafu dhidi yake na Katibu Mkuu Maswi, kutokana na uamuzi wake wa kuzinyima kampuni hizo zabuni ya kuuza mafuta ambayo zilikuwa zikiuza kwa bei ya juu kwa zaidi ya Sh bilioni 6 kwa mafuta ya matumizi ya mwezi mmoja ukilinganisha na bei ya Puma Energy.

Kutokana na hali hiyo, wabunge wengi waadilifu walichachamaa na wengine kukiri kuwapo kwa hali hiyo na hata kutoa ushuhuda kwamba hata wao wamepelekewa fedha wakazikataa. Mjadala kuhusu suala hilo uliendelea pia bungeni Julai 27 hadi 28 2012 ambako wabunge walishinikiza wabunge waliohongwa watajwe; na Kamati ya Nishati na Madini ivunjwe. Wabunge waliochangia kwa nguvu kuhusu suala hilo ni pamoja Kangi Lugora, Vita Kawawa, Joseph Selasini, David Kafulia na Ezekiel Maige.

Katika michango yao, wabunge hao waliitahadharisha Serikali kwa kutaka iwe makini katika uamuzi wake, kwani kumbe wakati mwingine wabunge wanapiga kelele kuhusu viongozi wa Serikali wakisukumwa na nguvu ya rushwa kutoka kwa wafanyabiashara walioathirika na uamuzi mzuri wa viongozi hao.


CHIMBUKO LA MCHEZO HUU MCHAFU

Kutokana na tabia iliyojengeka na inayoonekana ya Serikali kama mhimili wa dola kuonekana kuzidiwa nguvu na Bunge na hivyo kuwa ‘too submissive to the Parliament', Bunge limejikuta likitumia vibaya nafasi yake ya kuisimamia na kuishauri Serikali kwa kujiingiza kwenye masuala ya utawala na utendaji wa siku hadi siku wa Serikali (shughuli ambazo zinaendeshwa kwa mujibu wa sheria mbalimbali zilizopo), badala ya kuisimamia Serikali katika masuala makubwa ya kisera.

Katika hali hiyo, wabunge sasa wameanza kuwa wanashughulika na masuala madogo kama mtumishi kutolipwa haki zake za kitumishi, mfanyabiashara kukosa zabuni, mfanyabiashara kufutiwa leseni, na kadhalika; masuala ambayo ni ya mtu mmoja mmoja na yana sheria zake, na ambayo katika hali ya kawaida, watu hao wangepaswa kwenda mahakamani ambako ndiko tafsiri sahihi ya sheria inafanyika.

Kwa kugundua hali hiyo, wafanyabiashara wengi wanaoathirika na uamuzi wa watendaji serikalini, sasa hawaendi mahakamani kupinga uamuzi huo, badala yake wanakimbilia kwa wabunge ili Bunge lishinikize – ama uamuzi fulani wa watendaji serikalini utenguliwe au kiongozi fulani aondolewe.

Ingawa ni kweli kwamba kuna watumishi na viongozi wengi wanaokiuka misingi ya sheria katika uamuzi na utendaji kazi wao, matumizi ya Bunge katika mazingira fulani fulani hayana matokeo mazuri ya haki, kwani bungeni uamuzi haufuati misingi ya kuangalia vielelezo husika, bali misingi ya ‘wengi wamesema'.

Hivyo, wabunge wengi wakishinikiza waziri au kiongozi fulani aondolewe, hayahitajiki mazingira ya kutoa vielelezo vya bayana kuhusu makosa ya mhusika, bali hulazimika kuondoka. Hii ndiyo nguvu ya wengi ambayo sasa imeanza kutumika vibaya kwa mahasimu kufanyiana "lobbying" na kutoa rushwa kwa wabunge ili kushinikiza uamuzi huo.

Kwa upande mwingine mfumo wa uchaguzi na uendeshaji wa shughuli za kibunge nao umewasababisha wabunge wawe na hamu kubwa ya kujipatia fedha na hivyo kuwa "vulnerable" kwa rushwa.

Mfumo wa sasa wa uchaguzi ni wa gharama kubwa kwa wagombea, hivyo wagombea wengi hushinda kwa gharama kubwa. Aidha, wananchi nao wamekuwa wakiwatumia sana wabunge kama wafadhili au watatuzi wa kero binafsi za kimaisha badala ya kuwatumia kama wawakilishi pekee. Hali hii nayo inaongeza shinikizo kwa wabunge kutafuta fedha kwa ajili ya kuendesha maisha yao ya kisiasa na hasa kujipendekeza kwa wapigakura wao.

Kwa sheria za sasa, wabunge pia hulazimishwa kuacha kazi zao za kitumishi mara wanapochaguliwa kugombea ubunge. Hivyo, wabunge wengi ambao walikuwa watumishi kwenye taaluma mbalimbali, hulazimika kuingia kwenye biashara kama njia pekee ya kuendesha maisha. Eneo hili ambalo nalo wengi wao hawana muda wa kusimamia shughuli hizo na pia hawana uzoefu na weledi, haliwaletei mafanikio. Hivyo biashara nyingi za wabunge hukwama.

Biashara nyingi za wabunge huanzishwa kwa mitaji ya mikopo ya benki. Kwa mfano, mwaka 2011 benki zilikuwa zikiwakopesha wabunge hadi Sh milioni 200 ambazo hulipwa kutoka kwenye mshahara na marupurupu ya ubunge.
Katika mazingira hayo ambako wabunge hulazimika kuanzisha biashara kwa kuchukua mishahara yao yote, wabunge huishi miaka mitano bila mishahara wala marupurupu yanayoendana na maisha yao kwani huwa wamekopa mishahara yao yote.

Wabunge hulazimika kujitafutia njia nyingine za kujipatia kipato ikiwa ni pamoja na kudai nyongeza ya posho, kudai kufanyiwa semina na mashirika na taasisi za serikali, kudai kupatiwa ziara za kiserikali na kibunge, kudai kuteuliwa kwenye bodi mbalimbali za mashirika ya umma na hata kudai na kupokea rushwa kutoka kwa viongozi wa mashirika na wafanyabiashara kwa lengo la kuwatetea kwenye shughuli zao.

Huu ndiyo msingi wa yanayotokea sasa bungeni. Tatizo la Kamati ya Nishati na Madini si la kamati moja, bali karibu kamati zote zinazosimamia sekta nyeti kama Nishati na Madini; Serikali za Mitaa; Mashirika ya Umma; Maliasili na hata Miundombinu.

Uhusiano mbaya kati ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na wafanyabiashara

Katika kipindi cha mwaka 2011 na 2012, eneo jingine ambalo limegubikwa na misuguano kutokana mabadiliko ya kiutendaji ni Maliasili hasa Sekta ya Wanyamapori.

Katika kipindi hicho, kumekuwa na matukio ya ukiukwaji wa sheria na utoroshwaji wa wanyama hai nje ya nchi kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Novemba 2010 na ugawaji upya wa vitalu vya uwindaji wa kitalii.
Katika utekelezaji wa Sheria Namba 5 ya mwaka 2009 ambayo - pamoja na mambo mengine – imeelekeza yafutayo kwa lengo la kuongeza tija na mapato ya serikali:-

1. Kuongeza idadi ya kampuni za kizalendo na kupunguza za kigeni. Sheria imeelekeza kwamba kampuni za kigeni zisizidi asilimia 15 ya kampuni zote zilizogawiwa vitalu. Hatua hii inapaswa kufikiwa katika mazingira ambayo tasnia hii inamilikiwa na wageni kwa zaidi ya asilimia 80; na kampuni nyingi za kigeni ndizo zenye nguvu ya kimitaji, masoko na uzoefu ukilinganisha na kampuni za kizalendo ambazo nyingi ni ngeni.

2. Kupunguza idadi ya vitalu vinavyoweza kugawiwa kwa kampuni moja. Kabla ya sheria hii hapakuwa na ukomo wa idadi ya vitalu kwa kampuni, na hivyo kampuni nyingi za kigeni zenye nguvu na uzoefu zilikuwa na vitalu vingi, nyingine hadi vitalu 18. Sheria imeweka ukomo wa vitalu vitano kwa kampuni.

3. Kugawa upya vitalu vikubwa ili kupata vitalu vingi. Agizo hili linakuja wakati kuna kampuni kubwa za kigeni zenye vitalu vikubwa vinavyofikia hadi km 24,000, hivyo, kampuni nyingi kupinga kugawanywa kwa vitalu ‘vyao' na pale vilipogawanywa, kampuni hizo hazikupenda vitalu hivyo au sehemu yake kugawiwa kwa waombaji wengine kwa kile kinachodaiwa kuwa ‘zimewekeza sana katika maeneo hayo'.

Hivyo, baada ya ugawaji vitalu kufanyika, kampuni nyingi za kigeni ziliathirika na hivyo kuzifanya zilalamike. Imeelezwa na vyombo vya habari kwamba kampuni kadhaa zilifikia hadi kulalamika Ikulu, japo Ikulu ilikanusha kuingilia mchakato wa ugawaji vitalu na hivyo kuwaelekeza wenye malalamiko wote waende wizarani.

Kwa upande mwingine, tukio la wanyamapori hai kutoroshwa kupitia KIA lilisababisha kuchukuliwa kwa hatua zifuatazo:

1. Wafanyabiashara watuhumiwa kufikishwa mahakamani Moshi mwezi Mei 2011 kwa kesi ya uhujumu uchumi. Kesi hiyo, yenye watuhumiwa sita inaendelea. Mtuhumiwa mmojawapo ni Mpakistani Ahmed Kamrani ambaye anaaminika kuwa na nguvu kubwa za kifedha.

2. Watumishi walioonekana kuzembea au kutuhumiwa kujihusisha na biashara hiyo walisimamishwa kazi. Jumla ya watumishi watatu akiwamo Mkurugenzi wa Wanyamapori walisimamishwa kazi Agosti 18, 2011

3. Biashara ya wanyamapori hai nje ya nchi ilifungwa kwa tamko la Waziri Mkuu Bungeni Agosti 18, 2011.
Kutokana na uamuzi huo, wafanyabiashara – hasa wawindaji wa kigeni na wale wanaojihusisha na usafirishaji wanyamapori hai nje ya nchi – walianza kampeni ya kuupinga. Katika kampeni zao, walifika kwa viongozi wa juu serikalini ikiwamo Ikulu na kwa Waziri Mkuu bila mafanikio, ndipo njia ya Kamati ya Bunge ilipotumika.

Ufuatao ni muhtasari wa jitihadi za wafanyabiashara hao pamoja mikutano waliyofanya kwa viongozi wa Kamati na wakati mwingine Kamati ya Ardhi, Maliasiali na Mazingira:

Kwa kuzingatia yaliyojitokeza kwenye Kamati ya Nishati na Madini, hakika uhusiano huu baina ya viongozi wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira pamoja na mikutano baina ya wafanyabiashara na Kamati, unatia shaka. Posho nono zilitolewa kwenye vikao vyote, na kwa kweli hali hiyo, kwa mujibu wa Sheria ya Rushwa, inaashiria kuwapo vitendo vya rushwa.


HITIMISHO

Wakati Spika akivunja Kamati ya Nishati na Madini na kuahidi kuvunja Kamati nyingine, Kamati ya Maliasili na Mazingira ni miongoni mwa kamati zenye kutiliwa shaka na kutuhumiwa kwa rushwa.

Kamati hii imeshakuwa na tuhuma siku nyingi. (Rejea maelezo ya aliyekuwa Mbunge wa Kwela, Dk. Chrisant Mzindakaya) wakati akihitimisha hoja yake ya Azimio la Bunge kuhusu uwindaji wa kitalii na kutungwa kwa Sheria mpya ya Wanyamapori).

Aidha, uchunguzi wa kimaadili na rushwa unatakiwa kufanywa na Takukuru kwa kutumia rejea za mikutano hiyo na kujiridhia uhalali na kuzingatiwa kwa maadili kwa wajumbe na viongozi wa Kamati hiyo. Aidha, ni vema sasa Takukuru na vyombo vingine vya usalama kujipanga na kuwa "proactive". Ni lazima vijipenyeze kwenye Kamati hizi ili kujua kinachoendelea huko.

Aidha ni vema vyombo hivi viwe vinabaini matukio haya yenye kutia shaka na kuchukua hatua badala ya kusubiri mijadala ya bungeni kwani, kama ilivyobainika sasa, wabunge wengi wanachangia kwa malengo maalumu yanayotokana na ushawishi wa rushwa kutoka kwa wafanyabiashara waathirika wa uamuzi wa viongozi wachapakazi serikalini.

Aidha, Serikali, na hasa Waziri Mkuu, atumie vyombo vya uchunguzi mapema kwenye kila jambo na kutumia taarifa ya vyombo hivyo katika kujibu hoja za wabunge, badala ya kila wakati kukubali shinikizo la wabunge ‘waliohongwa', kwani kwa kufanya hivyo, viongozi wengi wazuri wataumizwa na serikali haitakuwa imara. Badala yake itakuwa ikiteua viongozi kila wakati.

Uwezekano mwingine ni kutokea kwa viongozi wasiokuwa na uamuzi, jambo ambalo litakuwa ni kikwazo kwa utekelezaji wa shughuli za serikali na maendeleo kwa ujumla.

Source: Wote pamoja.com
 
Mkuu, mbona "siri" zenyewe zilizovuja hazijaandikwa? Umeisoma kweli hii taarifa au umeinakili tu na kuweka hapa haraka haraka? Yaliyoandikwa hapa ndiyo yaliyoandiokwa na vyombo vya habari wakati ule, wewe unaleta tena kama siri?
 
Matumaini ya watanzania yalikuwa huko bungeni kwa wawakilishi wao sasa na wao wana "collude" na watumishi wa serikali na wafanyabiashara mmh kazi tunayo. Tanzania bila rushwa sijui kama itawezekana kwa hii generation yetu.
 
Hii inaonekana kama vile ni taarifa ya waziri mmoja aliyeenguliwa sasa anataka kulipiza kisasi kwa kamati anayodhani ilimyang'anya ulaji!! Kijana hizo ulizokwiba zinakutosha endelea na biashara yako ya malori unakopata $20,000 kwa mwezi!! Mtoto acha kupiga mayowe.
 
Back
Top Bottom