Sijui ya jeshini mie - Dk. Mwinyi

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,011
[h=1]Sijui ya jeshini mie - Dk. Mwinyi[/h]
picture-9.jpg

Na Alfred Lucas - Imechapwa 19 October 2011


WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, hajui “kinachoendelea” eneo la kambi ya jeshi ya usafirishaji-Kunduchi (KTC), MwanaHALISI limegundua.
Waziri Dk. Mwinyi aliliambia gazeti hili kwamba hafahamu kinachoendelea katika eneo lenye machimbo ya kokoto Kunduchi-Mtongani, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Wakazi wa eneo la Kunduchi wanadai kuwa askari wa kambi hiyo, wamekuwa kwenye ‘operesheni maalum’ ya kuwatimua kutoka eneo ambako yamekuwa makazi yao ya miaka mingi.
Diwani wa kata ya Kunduchi, Janeth Rethe aliliambia gazeti hili juzi kuwa hadi kufikia Ijumaa iliyopita, watu watano walikuwa wameshinikizwa kuhama eneo hilo.

Amesema askari waliofika kwenya makazi ya raia, wakiwa katika makundi, wamewajeruhi raia watano. Diwani amesema waliokumbwa na kadhia hiyo wamepigwa na kuchubuka mikono, miguu na usoni na nyumba 62 zimebomolewa.
Waziri Mwinyi alipoulizwa juu ya kadhia hiyo, alisema hajui kinachoendelea na kwamba mwandishi aulize kwenye kambi husika.

Hasa waziri aliulizwa juu ya taarifa za askari wanaodaiwa kubomoa nyumba za raia na kuwapiga.
Alisema, “…bwana eeh! Wewe piga simu makao makuu ya jeshi bwana; mimi sina taarifa hizo. Fuatilia hukohuko,” kisha alikata simu.
Diwani Rethe amedai kuwa eneo la makazi ya raia na kule ambako ni machimbo ya kokoto “panatakiwa na wakubwa jeshini.”

Hakueleza waziwazi na kwa uhakika ni askari gani hasa wanataka eneo hilo ambako wananchi tayari wamejenga nyumba za kudumu.
Diwani amesema juhudi zake na wenzake kukutana na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo, “angalau kumuuliza kulikoni hazijaweza kufanikiwa.”
Rethe ametoa wito kwa serikali kuwafidia wakazi wa kata yake ambao amesema kwa zaidi ya miaka 10 sasa wamefanya eneo hilo kuwa makazi yao ya kudumu.

“Hata kama wanataka kulichukua eneo hili na kuligawa kwa watu wao, basi ni vema serikali ikafuata taratibu ya kutoa fidia. Maana hawa wanaotaka kuondolewa hapa, ni binadamu pia. Serikali inapaswa kulinda raia wake,” anasema diwani huyo kwa sauti ya uchungu.
Anasema, “Pamoja na kwamba eneo hili liko nje kabisa ya kambi ya jeshi, lakini tunaona juhudi za kutuhamisha kwa nguvu na kuharibiwa mali zetu.”

Mwenyekiti wa kamati ya mipango miji wa manispaa ya Kinondoni, Tarimba Abbas ameliambia MwanaHALISI, “Nimelisikia hilo, bali lipo juu ya mamlaka yangu.”
Alisema, “Kwa sasa suala hili lipo mikononi mwa mkuu wa mkoa, halmashauri na jeshi lenyewe. Ukitaka kupata taarifa zaidi wasiliana na mkuu wa mkoa au mkurugenzi wa manispaa.”

Taarifa zinasema ubomoaji nyumba za wakazi wa Kunduchi-Mtongani ulianza 22 Julai mwaka huu.
Imefahamika kuwa bomoabomoa imefuatia hatua ya mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni.
Tarehe 14 Julai mwaka huu, mkurugenzi wa manispaa aliandika waraka kwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa Kunduchi, akiagiza kuhama kwa wakazi hao kwa madai kuwa wako ndani ya eneo la jeshi na wanapasua mawe kwa kutumia baruti.

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Kunduchi Mtongani, Richard Rusisye ambaye alihojiwa kwa njia ya simu kuhusiana na barua ya mkurugenzi, alisema, “Kinachofanyika sasa kiko nje ya uwezo wangu.”
Rusisye ndiye tarehe 20 Julai mwaka huu aliandika barua kwa mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni kupinga kubomolewa kwa nyumba hizo.

Katika barua yake hiyo kwa mkurugenzi, yenye Kumb. Na. SM/KMT/No172/11, Rusisye anasema, “Wananchi hawamo ndani ya eneo la jeshi kama inavyodaiwa. Wapo nje ya beacon (alama za mipaka) ya jeshi.”
Rusisye alikuwa anajibu barua ya mkurugenzi wa manispaa ambayo iliagiza kuondolewa kwa aliowaita “wavamizi wachimba kokoto eneo linalomilikiwa na jeshi ifikapo 30 Julai 2011.”

Akiandika kwa njia ya msisitizo, Rusisye anasema, “Kwanza, notisi yako haikutaja majina ya walengwa…Huelezi watu hawa watapelekwa wapi baada ya kuondolewa hapa.”
Anasema, “Katika azimio la serikali ya mtaa, tulikubaliana watu hawa wasichimbe tena mawe kwa kutumia baruti bali watumie eneo hilo kwa kuishi tu. Hivyo ndivyo wanavyofanya sasa.”

Tayari kuna kesi Na. 90 ya mwaka 2009 katika mahakama kuu kitengo cha ardhi ambapo wakazi wa Kunduchi-Mtongani wanapinga kuhamishwa. Kesi hiyo bado haijaamuliwa.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yussuf Mwenda amesema, anachofahamu yeye ni kwamba nyumba zinazobomolewa ni zile zilizoko ndani ya eneo la jeshi.
Mkuu wa mkoa, Said Meck Sadick, wala msemaji wa jeshi, hawakupatikana baada ya simu kuita bila kupokelewa.
Lakini mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana alipoulizwa iwapo anafahamu lolote kuhusu suala hili, alikata simu. Mwandishi alipiga tena na tena, lakini simu haikupokelewa.
 
Back
Top Bottom