Siasa zinazotishia wawekezaji, ndiyo zipi tena?

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,007
Siasa zinazotishia wawekezaji kupunguzwa
Mwandishi Maalumu
Daily News; Friday,February 20, 2009 @19:13

Serikali imeazimia kupunguza misimamo ya kisiasa yenye hisia za kutishia wawekezaji. Ingawa haikufahamika ni misimamo gani, lakini taarifa iliyotolewa juzi, ilionyesha kuwa hayo yaliafikiwa katika mkutano wa kutathmini utendaji wa Serikali kati ya Rais Jakaya Kikwete na uongozi wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko.

Mkutano huo uliozihusisha pia taasisi za wizara hiyo, ulifanyika juzi kwa saa tisa mfululizo, ikiwa ni sehemu ya mikutano ya Rais aliyoifanya wiki hii kwa nyakati tofauti na Wizara za Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na taasisi zake, na ya Elimu na Mafunzo na taasisi zake.

“Mkutano umefikia makubaliano muhimu … kuhakikisha kuwa msimamo wa Serikali unatabirika na kupunguza misimamo ya kisiasa inayojenga hisia za kutishia wawekezaji,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo. Iliazimiwa kwamba zichukuliwe hatua za haraka kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuhudumia kwa ufanisi na ubora zaidi uwekezaji nchini kwa maofisa wa Serikali kupunguza urasimu kwa kufanya uamuzi wa haraka.

Katika mkutano huo, Rais Kikwete alitangaza kuwa katika Bajeti ya Serikali ya mwaka ujao wa fedha, itatoa asilimia moja ya Pato la Taifa kwa ajili ya utafiti, badala ya kiasi cha asilimia 0.3 za sasa. Kwa wiki hii, Rais Kikwete amemaliza mikutano yake hiyo baada ya kuwa amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na taasisi zake, na Wizara ya Elimu na Mafunzo na taasisi zake kabla ya mkutano wa juzi.

Taarifa hiyo ilitokana na maazimio ya mkutano huo uliotaka zifanywe jitihada kubwa zaidi kuimarisha eneo la utafiti nchini. Masuala mengine yaliyoazimiwa ni kwamba hatua za haraka zichukuliwe kuvutia wawezekaji katika eneo la kusindika mazao ya kilimo na vyakula, ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda vya matunda na mboga, na kusindika bidhaa za nyama.

Vile vile kuchukua kuwahamasisha Watanzania kuingia katika eneo la kunenepesha ng’ombe kama njia ya kuhudumia sekta ya viwanda vya kusindika bidhaa za nyama. Wakati huo huo, walikubaliana kuwa idara za viwanda na biashara ziimarishwe kwa nia ya kuzipa uwezo mkubwa zaidi wa kuhudumia mchakato wa kuanzishwa viwanda nchini na kuimarisha biashara.
 
Back
Top Bottom