Siasa za tanzania

nvbongo

New Member
Sep 28, 2010
3
0
Uchaguzi mkuu unakaribia kwa kasi ya ajabu kwa Watanzania huku kila chama na mwanasiasa akivutia ngoma kwake. Kama ukiwasikia wanasiasa wetu hao kwa umakini basi unaweza ukaamini wanaweza wakaleta mabadiliko makubwa pindi tutakapowapa dhamana ya kutuongoza katika maeneo yetu mbali mbali, iwe kata kwa diwani, jimbo kwa mbunge na nchi kwa Rais.
Ninachouliza kwa sasa ni wagombea wangapi bila kujali itikadi yao ya chama wapo tayari kutetea maslahi ya umma na sio maslahi yao binafsi. Ili kujua hilo nimejaribu kuona vitendo vinavyofanyika katika kila chama na hasa vyama vya upinzani ambavyo ndio vinavyotegemea kutoa changamoto kwa chama tawala (CCM)

Kabla sijaenda kwenye vyama vya upinzani, ninaona ni bora nianzie chama Tawala kwa kujadili vitu ambavyo vinanifanya nichanganyikiwe na siasa za hapa kwetu. Mfano wa kwanza ni suala la kijana Hussein Bashe, ambaye alienguliwa na vikao vya chama kuwa hafai kugombea kwa tiketi ya CCM kwa sababu sio raia halali wa Tanzania. Na hilo mpaka waandishi wa habari walielezwa bila uwoga wowote na John Chiligati, Katibu mwenezi wa CCM na pia Yusuph Makamba ambaye ni Katibu Mkuu wa CCM. Sasa baada ya wiki kadhaa kupita Waziri Masha ametuambia yeye kama mtu wa mwisho mwenye msimamo kuhusu suala hili wa kutumia nafasi yake ya Uwaziri wa mambo ya Ndani anatangaza Bashe ni raia halali wa Tanzania. Inasikitisha kuona haki ya mtanzania inapotea tena mbele ya taifa zima na limefanywa kimakosa bila vikao vya chama kupata maoni ya Waziri wa Mambo ya Ndani anayetoka chama tawala. Na mtanzania wa kawaida kama mimi ategemee nini katika suala la kupata haki kama Bashe kafanyiwa hivyo mbele ya umma. Ningefurahi sasa Rais Jakaya Kikwete iwapo atapofanikiwa kuingia Ikulu tena basi ampe hata nafasi ya kuteuliwa ya ubunge kwani hata ushindi aliopata Bashe ulithibitisha anakubalika miongoni mwa Wana Nzega, lakini pia ninamsifu Bashe kwa ukomavu wa kisiasa alionyesha kwa kukubali maamuzi ya chama ingawa yamemkandamiza, tofauti na wanasiasa wengine ambao nitawajadili hapo baadae.

Suala la pili ambalo Chama Tawala inabidi liangalie kwa umakini ni kutokuwa na Double Standard, nikimaanisha misimamo tofauti katika suala moja la msingi. Suala hilo ni rushwa au kutumia dhamana ya cheo vibaya. Sasa hapo ataingia Fredrick Mwakalebela ambaye katokea TFF ( Shirkisho la mpira nchini)na kajidumbukiza katika medani ya siasa. Mwakalebela alimbwaga Mama Monica Mbega lakini akaja kuenguliwa kwenye vikao vya chama kwa sababu alifunguliwa kesi mahakamani na TAKUKURU kuhusu utumiaji wa rushwa kwenye mchakato wa kura za maoni. Swali ambalo linawatatiza makada wengi wa CCM Iringa na pia wadau wa siasa nchini, iweje waheshimwa Andrew Chenge na Basil Mramba waachwe, huku Chenge akitajwa kwenye sakata la rada na Mramba akiwa amefunguliwa mashtaka ya kutumia madaraka yake vibaya. Haki ipo wapi kama wengine wanaachwa na wengine wanaenguliwa.

Naona kwa hayo mawili ninataka niiache CCM na niende kwenye Upinzani na ningependa kuchukua vyama viwili vikubwa vinayotoa upinzani kwa CCM ambavyo ni CUF na CHADEMA. Nianze na CHADEMA ambayo inaonekana kutoa upinzani mkubwa kwa CCM kwa jinsi wadau wanavyoangalia upepo wa kisiasa nchini. Lakini inasikitisha kuona CHADEMA inaweza ikageuka kuwa CCM B hata kabla hawajaingia pale kwenye anuani namba moja nchini MAGOGONI (Ikulu). Kitendo cha CHADEMA kusubiri kura za maoni ziishe halafu wenyewe wachague wagombea wao ni jambo la kushangaza sana, Je CHADEMA hawapo watu makini wa kujaza nafasi za wagombea mpaka wasubiri CCM wamalize mchakato wao.?
Nitaanza na wanasiasa ambao CHADEMA imewachukua ambao mimi ninawawekea viulizo vinavyonifanya nichanganyikiwe zaidi na Siasa za Tanzania.

JOHN SHIBUDA: Ninataka nimuulize bwana Shibuda swali moja, Je CCM imekuwa mbaya baada ya yeye kuangushwa kwenye kura za Maoni, au baada ya yeye kuenguliwa kwenye vikao vya chama rasmi, Ndugu Shibuda akajua CCM ni chama cha Mafisadi. Je ni Shibuda huyo huyo aliyemchangia Kikwete kwenye mbio zake za kuongeza muhula mwingine wa kukaa Ikulu katika shamrashamra zilizofanyika pale Dodoma. Nimuulize swali lingine Bwana Shibuda, Je iwapo angeshinda au angepitishwa na CCM kuwa mgombea katika nafasi ya ubunge angesema nini, angekataa.
Sasa Shibuda anatetea maslahi yake kwa kuhama vyama au maslahi ya watu. Hilo ninawaachia umma wajibu vizuri na wananchi jimbo la Maswa ambao watapiga kura kama Shibuda anawafaa au la?

Mwanasiasa mwingine ambaye ningependa kumzungumzia ni Ndugu Fred Mpendazoe. Inasikitisha kuona mwanasiasa mmoja anaweza akabadilisha vyama vingi katika kipindi cha muda mfupi hivyo. Alitoka CCM akaenda CCJ, ambacho alisema kitakuwa na nguvu kubwa ya kuleta mabadiliko ndani ya uwanja wa kisiasa lakini juhudi hizo zikagonga mwamba, (Je alikuwa hajajiweka vizuri katika suala la kuipatia CCJ usajili wa kudumu), Baada ya hapo akaenda CHADEMA kutokana na CCJ kukosa usajili wa kudumu. Nataka nimuulize Mpendazoe maswali machache pia, Je kwa nini hakuenda kugombea Kishapu alikomaliza muda wake wa ubunge? Swali lingine ni kuwa je amehamia CHADEMA ili apate nafasi ya kugombea ubunge na je kama CCM wakishinda kuingia Magogoni (Ikulu) na JK akiamua kumpa ubunge wa kuteuliwa , anaweza akarudi CCM? Hayo yote ni maswali ambayo majibu yake ni kazi kuyapata, kilichobaki ni kutafakari kila mtu na majibu yake.

Arcado Ntagazwa, Waziri wa zamani wa serikali ya CCM na mwanachama mpya wa CHADEMA naye anaingia kwenye orodha. Hivi pamoja na kukaa miaka yote CCM hakuweza kutambua kuwa chama tawala kina harufu ya ufisadi na rushwa, au kwa sababu alikuwa yupo kwenye nafasi nyeti z, na baada ya kupigwa chini kwenye kura za maoni za kutaka ubunge kule Muhambwe akaona na yeye aanze kudandia treni la kupigia kelele ufisadi huenda akabahatisha kupata nafasi kwa njia nyingine. CHADEMA kina viongozi ambao wameonyesha matumaini kama Slaa na Zitto Kabwe lakini je kuwachukua makada kama Shibuda na Ntagazwa kunabadilisha upepo wa siasa za chama chao.

Chama cha mwisho ni CUF (Civic United Front), ambacho kinaonekana zaidi kuwa na nia ya kuwepo kwenye siasa za visiwani kuliko huku Bara. Ingawa kimefanya vizuri katika chaguzi za Serikali ya mitaa lakini kimeshindwa kupata hata kiti kimoja cha ubunge kwenye uchaguzi mkuu uliopitaupande wa Bara na kinaonekana kushindwa kuwa na wanasiasa nyota upande wa Bara, kama ilivyo visiwani ambako kuna Ismail Jussa Ladhu, Juma Duni Haji, Hamad Rashid na wengineo wengi. Na Je CUF na CHADEMA kwa nini wasiweze kuwa na mgombea mmoja katika majimbo mbalimbali na kuungana hili pia ni jambo la kujiuliza kwa vyama hivyo viwili. Lengo kubwa la upinzani ni kuiondoa CCM madarakani na inaonekana kuwa kazi ngumu kadri siku zinavyoenda. Na bila kuungana itazidi kuongeza ugumu wa kuingia Magogoni kwa upinzani katika miaka ya karibuni kutoka sasa. Iwapo CUF ikishindwa kuchukua hata kiti kimoja cha ubunge upande wa pili wa Muungano (Bara), Je itamaanisha nini kwa mustakabali wake kama moja ya vyama vikuu vya upinzani nchini Tanzania.

Hivi karibuni CUF ilimsimamisha mgombea katika jimbo la Zitto Kabwe, je huku ni kuua upinzani au kusaidia upinzani. CCM ndio imekumbatia mafisadi, sasa je na CUF wanafanya nini kumbania Zitto ambaye kaonyesha kufichua uozo kwenye sekta ya madini kwa kiasi kikubwa. Mimi ninazidi kuchanganyikiwa kuangalia Siasa za pande zote mbili zimekaa kujali maslahi ya watu wachache kuliko ya watu wengi.
Baba wa Taifa wa India Gandhi alisema “ BE THE CHANGE YOU WANT TO SEE”, hivyo natafakari naona sisi wananchi tuanze kubadilika kwa kuacha kula cha juu na kutoa cha juu kwenye sehemu za kazi, na hivyo hata viongozi tutakaowatoa hapo baadae watakuwa waadilifu kuliko hao tuliokua nao.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom