Siasa za Tanzania ni kwa Wasomi au Matajiri?

KIPATO kikubwa cha Mbunge kwa mwezi, wakati anaingia bungeni na akimaliza muda wake,
kimetajwa kupunguza mchango wa wasomi na wataalamu katika ujenzi wa Taifa na kuzalisha wajasiriamali wengi wa kisiasa.


Akizungumza na gazeti hili wiki hii, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk.
Prosper Ngowi alisema ukubwa wa kipato cha Mbunge umesababisha wataalamu ambao
wangetoa mchango mkubwa katika taaluma zao, kuzitelekeza na kukimbilia u bunge.

"Haina maana kuwa Bunge letu tukufu halihitaji wataalamu. Lakini ni ukweli kuwa pengine mtu mwenye taaluma kama ya utafiti na utabibu anaweza kutoa mchango mkubwa zaidi kwa umma kwa kufundisha, kutafiti na kutibu kuliko kukaa bungeni.

"Lakini kwa kuwa kifedha Bunge linalipa zaidi, watu wanashawishika na ni haki kushawishika kuacha taaluma na kazi ambazo mchango wao kwa Taifa ungekuwa mkubwa sana," alisema Dk. Ngowi.

Kwa sasa kipato cha Mbunge kinakadiriwa kufika Sh milioni 7 kwa mwezi, anapata mkopo wa Sh milioni 90 kwa ajili ya gari anapoingia bungeni na anapata kiinua mgongo wakati Bunge
linapovunjwa kwa ajili ya uchaguzi.

Hoja hiyo iliungwa mkono na Profesa wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine, Mwesiga Baregu aliyesema mishahara mikubwa ya wabunge ni kichocheo kwa wataalamu kuacha fani zao wakiwa bado wanahitajika na jamii kwa utaalamu zaidi na kukimbilia kwenye ubunge.

Akitoa mfano wakati akiwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na taarifa
alizonazo mpaka sasa, Baregu alisema, "mshahara wa Profesa anayefundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka jana (2010) ulikuwa ni kati ya Sh milioni 2 hadi Sh milioni 2.5 na mwaka huu sidhani kama unazidi Sh milioni 2.9 na hapo ni kila kitu."

Dk. Ngowi kwa upande wake alisema pia si haki kwa mbunge kukopeshwa fedha za mlipa kodi wakati na wao ni watumishi wa umma na sehemu ya walipa kodi.

"Kwa kuwa Serikali haina fedha za kumkopesha kila mlipa kodi kama wabunge wanavyokopeshwa basi hakuna haki ya mgawanyo (distributive justice) kwa wachache kujipatia fedha hizi," alisema Dk. Ngowi.

Dk. Ngowi alipendekeza pia wabunge wasilipwe mishahara sawa bali mishahara
itofautiane kulingana na kiwango cha elimu, uzoefu, ujuzi na ufanisi wa mbunge
husika.

"Kama wafanyakazi katika sekta ya umma na binafsi wanalipwa kutokana na viwango vya elimu, uzoefu na ujuzi ni vema iwe hivyo pia bungeni," alisema Dk. Ngowi

Kutokana na hali hiyo, Dk. Ngowi alipendekeza kuundwe chombo huru kichunguze stahili halali za wabunge na kupinga marekebisho ya stahili hizo kufanywa na Bunge.

"Tatizo la ulipanaji huu mkubwa bungeni ni kuwa waheshimiwa ndiyo watunga
sheria. Unapokuwa mwamuzi (referee) na mchezaji kwa wakati huo huo hakuna
utawala bora. Ni bora kuwa na chombo huru kiamue stahili za waheshimiwa ni
zipi," alisema.

Mfanyabiashara ndogo wa Mbezi Luis, Nassor Abdallah alielezea kushangaa wabunge wanaoshabikia posho kwa madai kuwa wanaweka mbele maslahi yao na si ya wananchi.

Kwa upande wake, Gema Mmari, mkazi wa Sinza, Dar es Salaam aliiomba Serikali kuchukua hatua mara moja kupunguza kama si kuondoa kabisa posho za wabunge kwa kuwa wanaendelea kuweka pengo kati ya walionacho na wasionacho nchini.

Mjadala wa kipato cha wabunge umeibuka baada ya mjadala wa posho ulioamshwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto aliyekataa kulipwa posho za vikao huku Mbunge wa Bumbuli, January Makamba akisema ni suala la kitaifa na lipo katika Mpango wa Taifa wa
miaka mitano.
Source: Habari leo 20/06/2011
 
Back
Top Bottom