Sheria ya maadili ya viongozi irekebishwe

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,299
33,082
Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma imetangaza kuwa inaaza kuhakiki mali na madeni ya viongozi wa umma 60 kama walivyowasilisha matamko yao kuhusu rasilimali na madeni kwa mujibu wa kifungu cha 9 na 11 cha Sheria
ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na.13 ya Mwaka 1995, uhakiki huo utafanyika nchini kote.

Kama alivyosema Kamishna wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Salome Kaganda, uhakiki huo unafanyika ukiwa ni utararibu wa kawaida kubainisha kilichotangazwa kwenye fomu na hali halisi ya mali na madeni ya viongozi hao ilivyo. Kadhalika, aliwataka wananchi wenye taarifa zozote wanaodhani zinaweza kusaidia Tume kujua zaidi kuhusu mali za viongozi waziwasilishe katika ofisi zao.

Tume hii iliundwa baada ya kutokea kwa ombwe la taratibu za kimaadili na kisheria juu ya umiliki wa mali na madeni kwa viongozi wa umma hasa kutokana na mageuzi ya kiuchumi na kisiasa ambayo yaliikumba nchi katika miaka ya mwisho ya 80 na mwanzoni mwa tisini, hususan baada ya kuuawa kwa Azimio la Arusha ambalo lilikuwa limeanisha miiko ya uongozi.

Madhumuni makuu ya kutungwa kwa sheria hii ni kuhakikisha kwamba viongozi wa umma hawatumii ofisi zao kwa maslahi binafsi, ndiyo maana kabla ya kiongozi yeyote wa umma wa ngazi zilizoanishwa kwa mujibu wa sheria hiyo kuanza kutumikia ofisi husika anawajibika kutoa tamko la mali na madeni yake kwa Kamishna wa Tume ya Maadili.

Kimsingi sheria hii inalenga kuwalinda viongozi pia kwamba mwenye mali zake asije kutuhumiwa kwamba alizipata kwa kutumia ofisi ya umma ambayo mapato yake halali katika ofisi hiyo hayamwezeshi kuwa nazo, lakini pia kusaidia kulinda ofisi za umma zisitumike vibaya.

Sheria hii inalazimisha pia kutangazwa kwa mali ambazo kiongozi husika anamiliki na zile za mwenza wake, kwa sababu katika mazingira ya kawaida, kuna uwezekano mkubwa wa kutumia jina la mwenza kujinufaisha.

Hatua hii ni ya pili kubwa kuwahi kuchukuliwa na Tume hii baada ya ile ya mwaka jana ya kuwaita viongozi ambao kisheria walipaswa kutangaza mali zao na kuziwasilisha katika Tume hiyo, lakini hawakufanya hivyo. Wapo waliopata karipio na kukumbushwa kuzingatia sheria hiyo.

Kwa hiyo tunaposikia sasa Tume inasambaa nchini kote kuhakiki au kukagua mali za viongozi ambazo zipo kwenye matamko yao ya mali na madeni, tunafarijika kwamba kidogo kidogo Tume hii inaamka na kuanza kutekeleza majukumu yake ambayo tangu mwaka 1995 takribani miaka 17 sasa haijawahi kuifanya kwa ufanisi huo.

Ni kwa maana hiyo tunapongeza hatua hizi. Tungependa kuona Tume ikipiga hatua zaidi katika kusimamia sheria hii si tu kwa kuwaita viongozi husika waliokiuka sheria hii, bali pia kuwa wazi zaidi kwa kushirikisha umma katika usimamizi bora wa sheria hii.

Tunajua pamoja na nia njema ya sheria hii, bado ina udhaifu mkubwa hasa katika kipengele cha kufanya mali na madeni ya viongozi yanayotangazwa kwenye fomu husika kuwa siri. Hali hii kwa hakika ndiyo imekuwa chimbuko la kuficha vitendo vyote vya udanganyifu vinavyofanywa na viongozi wa umma wakiwa chini ya kiapo.

Kwa mfano, chini ya sheria hii ingawa mwananchi yeyote anaruhusiwa kuomba kibali kwa Kamishna wa Tume ya Maadili cha kusoma fomu za kutangaza mali na madeni za kiongozi yeyote baada ya kuandika barua na kueleza sababu za kufanya hivyo, kisha kulipa ada ya kufanya hivyo endapo atakubaliwa na Kamishna, chochote atachokuta ndani ya fomu hizo haruhusiwi kusema kokote isipokuwa kwa Kamishna tu.

Hata vyombo vya habari haviruhusiwi kusema lolote juu chochote ambacho kimekutwa kwenye fomu za kiongozi yeyote. Kwa hali hii sheria hii badala ya kujenga uwazi na uwajibikaji, imejikita zaidi katika usiri ambao haujengi na kukuza hali ya kuwawajibisha viongozi ili wasidanganye katika kujaza fomu hizo.

Itakumbukwa kwamba kuna kiongozi mmoja aligundulika kuwa alikuwa amedanganya kwenye fomu zake baada ya makachero wa nchi moja kumfanyia uchunguzi wa mali zake kufutia kugundulika kuwa na akiba ya fedha nyingi za kigeni alizokuwa amehifadhi nje ya nchi. Kiongozi huyo aliyekuwa amekalia ofisi kubwa ya umma alifanya hayo kwa kuwa alijua si rahisi watu kujua kilichomo ndani ya fomu zake kwa Tume ya Maadili.

Kutokana na hali hii basi sisi tunaamini kwamba ili kazi za Tume hii ziwe na maana na kwa kweli iweze kusaidia kujenga uwajibikaji kwa viongozi wanaokabidhiwa ofisi za umma, ni lazima sasa sheria hii ifanyiwe marekebisho na kuruhusu uwazi zaidi kwa yale yanayotangazwa ndani ya fomu za matamko ya mali, kwa kufanya hivyo ni rahisi kushirikisha umma kutoa taarifa za udanganyifu unaofanywa na baadhi ya viongozi wanaotumia ofisi za umma kama uchochoro wa kujilimbikizia mali.
Bila kufanya hivyo, tunaendelea kushuhudia baadhi ya viongozi wa umma wakitumia vibaya ofisi zao, lakini bila kuchukuliwa hatua zozote kwa kuwa hakuna wa kumfunga paka kengele.



CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom