Sheria ya Maadili ya Uongozi wa Umma ifanyiwe marekebisho

Sumasuma

JF-Expert Member
Jun 23, 2011
342
110
JANA gazeti hili lilichapisha habari inayohusu taarifa ya Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuwa imeanza mchakato wa kuhakiki mali za viongozi hao nchi nzima, ikianzia na viongozi 60.

Katika orodha ya viongozi hao 60 watakaohakikiwa katika mchakato utakaoanza Februari 20, mwaka huu, wamo mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya, mameya wa halmashauri za wilaya, manispaa na majiji, wabunge, madiwani na wakurugenzi wa taasisi mbalimbali za umma.

Akizungumzia jijini Dar es Salaam juzi, Kamishna wa Tume ya Maadili, jaji Mstaafu Salome Kaganda alisema uhakiki huo unalenga kujenga jamii bora ya Watanzania hasa viongozi ili kuwafanya waishi kwa kufuata misingi ya uadilifu iliyowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Uongozi wa Umma.

Pamoja na hayo, kamishna huyo aliwaomba wananchi kuisaidia tume hiyo kwa kutoa taarifa zinazosaidia kugundua mali za zilizofichwa zinazodhaniwa kuwa za viongozi wanaoguswa na sheria hiyo.

Tumefarijika na hatua iliyofikiwa na tume hiyo na hatimaye kutangaza kuwa kuna viongozi waliowasilisha orodha ya mali zao, ingawa wengi walifanya hivyo baada ya kutishwa kuwa wachukulia hatua watakaoshindwa kufanya hivyo ndani ya muda uliowekwa.

Ni jambo la kufurahisha kuwa Tume imeamua kutangaza wazi waliotoa taarifa zao. Pia tunawapongeza viongozi waliopata ujasiri wa kuanika mali zao ingawa hatuna uhakika kama wameandika kila kitu kwa vile taarifa hizo ni za siri.
Zaidi ya hapo, tunaounga mkono mwaliko wa tume kwa wananchi kusaidia kutoa taarifa wanazojua kuhusu mali zinazodhaniwa kuwa za vigogo ambazo zinaweza kuwa zimefichwa, ili kukwepa maswali ya kutoa maelezo ya jinsi walivyozipata.

Hata hivyo, tunapata mashaka kuhusu uwazi na ukweli wa mchakato huo kwa sababu sheria hiyo haitoi kibali cha taarifa za viongozi hao kuanikwa hadharani ili jamii ijue na iweze kusema hadharani kama kweli ndivyo zilivyo au zimefichwa.

Kwa tafsiri rahisi ya sheria hiyo, taarifa hizo ni siri hazistahili kuanikwa kwani, hata wanaoruhusiwa kuangalia wanatakiwa kufanya hivyo katika ofisi za tume na kuzitunza moyoni bila kutangaza kwa vile ni siri.

Tunakubali kuwa taarifa binafsi za mtu ni siri, lakini usiri huu unatakiwa kuwa na mipaka kwani suala la mali za mtu siyo siri kwa sababu zinaonekana wazi. Mtu akiwa na nyumba, magari, mashamba, migodi ya madini, mifugo na mengineyo ni vitu vinavyoonekana hivyo siyo siri. Inakuwaje siri wakati wapo watu wanaozijua? Je, tunaficha ili watu wasishangae wingi wa mali za kiongozi kulingana na kipato chake na mfumo wa maisha yake, au kubaini mali alizoficha?

Kamishna amewaomba wananchi wasaidie kutoa taarifa je, taarifa hizo zitatangazwa, au zitatunzwa kwa usiri uleule wa kuwa siri isiyotakiwa kuanikwa hadharani?

Kwa ujumla tunasema, hii ina upungufu unaotakiwa kufanyiwa marekebisho kama kweli nia yake ni kujenga jamii ya viongozi waadilifu. Udhaifu wa sheria hii unaonekana wakati wa kutaja mali mtu anaingia na anapotoka madarakani kutokana na kutawaliwa na usiri mkubwa. Kibaya zaidi ni kwamba, kiongozi huyo anapoingia madarakani anajaza fomu ya mali alizonazo ambayo ni siri yake na Tume, lakini napotoka madarakani haelezi mali zake zimeongezeka au kupungua kwa kiasi gani?

Hii ni ishara tosha kuwa viongozi wetu wanapotoka madarakani wanakuwa na mali nyingi zaidi ikilinganishwa na mapato yao halali yanayotokana na mishahara na marupurupu wanayopata kwa mujibu wa sheria ya ajira zao.

Sisi tunaamini kuwa, mtu anapoamua kuwa kiongozi wa umma hana sababu ya kuficha mali zake ili kudhihirisha uadilifu wake kwa vile anatakiwa kuwa mfano wa kuigwa kwa anaowaongoza na wananchi kwa ujumla.

Kwa ujumla, kiongozi safi, mkweli, asiyependa udhalimu na kupata mali za aibu, hawezi kuogopa kutangaza mali zake hadharani kwani hiyo ni fahari kwake na watu watamuunga mkono. Sasa inakuweje iwe siri kiasi hicho?

Ni kwa mantiki hiyo basi, tunashauri kuwa vyombo vinavyohusika na hasa Bunge letu, bila kujali masilahi ya wabunge ambao pia wanaguswa sheria hiyo, lione umuhimu wa kuiboresha ili iende na wakati kwa kuweka mazingira ya uwazi zaidi.
:A S 465:
 
Kwa viongozi wanaotaka maslahi yao binafsi hawawezi kufanya kitu kama hicho
 
Wakitaka tuwaamini waanze na Raisi na mawaziri wake ndo washuke chini, pia tuone nini matunda ya kazi hiyo na si kukaa kimya baada ya wao kunyakua padiem.
 
Back
Top Bottom