"Kafata Nini Nchini?"
Nawauliza wajuzi, myajuayo ya ndani
Alipofika majuzi, akenda hadi chumbani
Kama vile paka jizi, akivizia machoni
Kafata nini nchini, kichaka huyo mwajua?
Nawauliza magamba, kichaka kafata nini?
Kafika huku atamba, akipepesa machoni
Kakenua kama mamba, udenda u mdomoni
Kafata nini nchini, semeni niwe sambamba
Ama magwanda mwajua?, kilomleta nchini
Kafika mwachekelea, na ninyi mpo sirini?
Magwanda mwachemshia, ama mwajua kunani?
Kafata nini nchini, magwanda naulizia
Si bure miye nahisi, kufika kwake nchini
Avizia kama fisi, mzoga u kigamboni?
Nasaka mwenye nyepesi, atoe hayo ya ndani
Kafata nini nchini, tujulisheni na sisi
Kaditama wa tamati, kalamu naweka chini
Wengine wasema ati, dili la kweli madini!
Alishawapa visheti, ati sasa taabani
Kafata nini nchini, tetesi nyingi baruti!
Choveki