Shahidi amweka pembeni Liyumba

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,956
22,148
Liyumba(14).jpg

Amatus Liyumba.

Shahidi wa sita katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, amedai mahakamani kuwa mabadiliko ya mradi wa majengo pacha ulifanywa na menejimenti ya BoT na si mtu mmoja.

Manase Shayo (75), ambaye taaluma yake ni mhandisi, alidai kuwa mkataba wa mabadiliko ya usanifu na ubunifu wa mradi huo ulifanyika kwa njia ya barua kati ya kampuni yake ya Design and Services na BoT na kwamba Liyumba alisaini mkataba huo kwa niaba ya menejimenti.

Liyumba katika kesi hiyo anashitakiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia serikali hasara ya sh. bilioni 221.1.

Akiongea mbele ya jopo la mahakimu watatu; Edson Mkasimongwa, Lameck lacha na Benedict Muingwe huku akiongozwa na wakili wa serikali, Prosper Mwangamila, shahidi huyo alidai kuwa BoT iliamua kufanya mabadiliko ya mradi huo baada ya idadi ya wafanyakazi kuongezeka na kuwepo kwa ukosefu wa ofisi kwa watumishi.

Aidha alidai kuwa mkataba wa mradi huo ulikuwa na thamani ya zaidi ya Dola milioni 73 za Marekani ambapo maelekezo yote ya utekelezaji wa mradi huo yalikuwa yanafanywa na kurugenzi ya utumishi na utawala ambayo ilikuwa inaratibu mradi huo.

Katika kesi hiyo ambayo Liyumba anakana mashitaka, anadaiwa kupindisha mkataba wa BoT kuhusu mradi wa ujenzi wa maghorofa pacha na hivyo kuongeza kiasi cha fedha zilizokuwa zikihitajika katika ujenzi na kuisababishia serikiali hasara.
 
Back
Top Bottom