Shahada za kura 2010 kuchapishwa nchini

Josh Michael

JF-Expert Member
Jun 12, 2009
2,523
77
Na Sadick Mtulya


SERIKALI imetangaza rasmi kuwa kuanzia uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba, 2010 itaanza kuchapisha nyaraka na karatasi za kura nchini kwa ajili ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kupatikana kwa mitambo mipya na ya kisasa yenye uwezo wa kuweka alama za siri, namba na rangi katika karatasi za kura kwa usalama mkubwa.

Kazi hiyo itatekelezwa kupitia Idara ya Mpiga Chapa Mkuu ambayo iko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Ununuaji wa mitambo hiyo ni mpango wa serikali wa kutaka kuimarisha idara hiyo tangu mwaka jana, ambapo serikali ilitoa zaidi ya Sh 1.7 bilioni na mwaka huu imetenga zaidi ya Sh 1 bilioni, ili kutekeleza mpango huo.

Pia ilielezwa kwamba mpango huo unalenga kuondoa utegemezi wa kuchapisha karatasi hizo nje ya nchi .

“Kwa sasa tayari umepatikana mtambo ambao utakuwa na uwezo wa kuweka alama za siri, namba na rangi katika karatasi za kura kwa usalama mkubwa. Na wakati huo huo upo uwezekano wa kuhakiki alama za siri zitakazowekwa,” alisema Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu(Sera na Mipango) Philip Marmo.

Marmo aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam mara baada ya kukagua mitambo ya zamani pamoja na huo mpya katika Idara ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali.

Waziri huyo alifafanua kuwa mpango huo unaendelea kufanywa kwa ushirikiano wa Idara ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi(Nec).

Marmo alisema kutokana na hatua hiyo, serikali itakuwa imeondoa matatizo yaliyojitokeza katika chaguzi za miaka ya nyuma yakiwemo ya kukosewa kwa majina ya baadhi ya watu na kuilazimu serikali kutumia fedha nyingi kufanya marekebisho madogo.

“Pia itasaidia sana katika udhibiti wa siri za nyaraka hizo katika mikondo mingi na kuokoa pato la taifa, hivyo utaona zipo faida nyingi sana kwa uwekezaji huu unaofanywa na serikali,” alisema Marmo.

Waziri huyo alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuiboresha Idara ya Mchapaji Mkuu wa Serikali, ili iweze kuendesha shughuli na udhibiti wa nyaraka za siri kiujumla.

Alisema kwa kuanzia idara hiyo imeboreshewa kwa kupatiwa mgawo maalum wa bajeti ya maendeleo na kwa kila mwaka watakuwa wakipata mtambo mmoja au zaidi na kwamba, hivi sasa mitambo mipya saba iko bandarini na mingine inapakiwa kuja nchini.

“Serikali tumeanza mkakati huo na ndio maana hivi sasa tayari tumekwisha leta mtambo mmoja na mingine saba ipo bandarini na mingine inapakiwa huko kwa watengenezaji nchini Ujerumani.

“Hivyo serikali ina matumaini kuwa kabla ya bajeti ijayo, idara hii itakuwa na mabadiliko makubwa kabisa ambayo yanaweza pengine kuhitajika kwa zoezi la kupunguza watendaji wa baadhi ya sehemu za mifumo ya zamani isiyohitajika,” alisema.

Waziri huyo pia alizungumzia mikakati ya kuimarisha idara hiyo kwamba ni pamoja na kujenga ofisi mpya na makao makuu mapya mjini Dodoma na mchakato umekwishaanza huku ukiambatana na hatua ya kumpata mtaalamu wa masuala ya uanzishaji wa kiwanda cha uchapishaji nyaraka za kawaida na siri.

“Hata hivyo katika makao hayo mapya, kutakuwepo pia chuo cha uchapishaji, karakana ya marekebisho ya mitambo yetu na pia viwanja vya kumbukumbu ya uchapishaji wa kale na asili vikiwa ni vivutio kwa wageni na pia sehemu ya mapumziko,” alisema

Pia serikali imeanzisha mpango maalum wa kupata wataalamu zaidi na waliobobea katika fani ya uchapishaji ikiwemo kuendelea na ajira ya watumishi watakaomudu uendeshaji wa mitambo ya kisasa na uendeshaji wa vifaa vya elektroniki.

Katika hatua nyingine, jana hiyo, Marmo aliagiza Wizara, Idara za serikali, taasisi zake pamoja na watendaji wote katika Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuanzia sasa kuhakikisha nyaraka zote zinachapwa kwenye idara hiyo.

Sambamba na agizo hilo, alizitaka Wizara, na Idara ya halmashauri zote nchini kurejesha nyaraka zote za serikali pamoja na nyenzo zake kama mihuri kwa Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, ili ziandikwe kwenye daftari maalumu.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya serikali kwa sasa kutaka kuhakikisha kuwa inakuwa na taarifa ya nyaraka zake zinazochapishwa kwa Mpigachapa Mkuu wa Serikali na pia nyaraka zake zote zitakazokuwa na ulazima wa kuchapishwa nje ya idara hiyo, ziandikwe kwenye daftari maalumu la mzunguko wa nyaraka za serikali.

“Mtindo huu wa kufanyia usaili na kuwekwa kwenye rekodi za nyaraka za serikali unatumika pia na nchi zilizoendelea na zenye mafanikio makubwa ya kiuchumi na kiulinzi, hivyo ninamuagiza Mpigachapa Mkuu wa Serikali kufungua regista hiyo kama hakuwanayo,” alisema Marmo.

Akizungumzia utendaji kazi katika idara hiyo, Marmo aliwataka wafanyakazi hao kufuata maadili ya kazi na kwamba, wafanyakazi waache mifarakano, wizi wa nyaraka ili kuimarisha utendaji kazi.

Alisema serikali haitawavumilia watumishi wanaochafua utulivu maeneo ya kazi.
Awali, Mpiga Chapa Mkuu, Casian Chibogoyo alimshukuru waziri kwa kufika na kuahidi kuwachukulia hatua mara moja wafanyakazi watakaojaribu kuiba nyaraka na kusababisha mifarakano kazini.
 
Back
Top Bottom