Serikali : Wananchi wote wenye sifa jijini Dar es salaam tutawaandikisha

Mwakaboko King

JF-Expert Member
Apr 22, 2015
1,099
207
Serikali imesema zoezi la uandikishaji wa wananchi katika Daftari la Kudumu la wapiga kura kwa kutumia mfumo wa BVR katika jiji la Dar es salaam litafanyika kama ilivyopangwa kuanzia Julai 16 hadi 25 mwezi huu kwa mafanikio makubwa kutokana na maandalizi mazuri yaliyofanywa na Tume ya Taifa ya uchaguzi kwa kushirikiana na Manispaa za mkoa huo.

Akizungumza wakati ufunguzi wa Mafunzo ya siku 2 ya wasimamizi wa zoezi jijini Dar es salaam, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala Bw.Raymond Mushi amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wasimamizi wa Manispaa hizo ili waweze kufanikisha zoezi la uandikishaji wa wananchi katika daftari la kudumu la wapiga kura katika jiji la Dar es salaam na kuzuia makosa yaliyojitokeza wakati wa uandikishaji katika maeneo mengine nchini.

Amewataka wasimamizi hao kufanya kazi kwa viwango na weledi wa hali ya juu wakati wa zoezi hilo ili kuzuia malalamiko kutoka kwa wananchi kwa kuhakikisha kuwa kila raia mwenye sifa anaandikishwa katika daftari hilo.

Amesema wananchi wote watakaofika kwenye vituo kujiandikisha wahakikishe kuwa wana taarifa muhimu kuhusu uraia wao pia wahakikishe kuwa wanafuata taratibu zilizowekwa na Tume ili waweze kuandikishwa.

"Natoa wito kwa wananchi wote waliokidhi viwango vya kupiga kura na wale watakaofikisha umri wa kupiga kura ifikapo 25 Oktoba 2015 wajitokeze kwa wingi maana wote wataandikishwa"Amesisitiza.

Aidha, amewataka wasimamizi hao kutoa ufafanuzi na elimu inayostahili kwa wananchi pale inapobidi wakati wa ukusanyaji wa taarifa zao na kuepuka kutumia lugha ya kuudhi ili kazi hiyo iwe rahisi na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika kujiandikrsha na kuepuka vitendo vya vurugu na siasa zinazoweza kuleta machafuko katika vituo vya uandikishaji,

Pia Ametoa wito kwa baadhi ya wanasiasa watakaofika kujiandikisha kwenye daftari la kudumu kuepuka kuingilia zoezi hilo kwa kuwa wao sio watumishi wa Tume ya uchaguzi.

"Kuna maeneo nchini baadhi ya wanasiasa wamekuwa chanzo cha kusababisha vurugu kwenye vituo vya uandikishaji, wao kama raia wanalo jukumu la kufika kujiandikisha na kuangalia watu wanaojiandikisha kama sehemu ya haki na wajibu wao kufuatilia ufanisi wa zoezi hilo na sio kuingilia kazi za wataalam wa Tume"

Kwa upande wake Afisa Mwandamizi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Joseph Mally amesema kuwa Mafunzo hayo ya siku 2 yanayohusisha wasimaizi 36 wa uchaguzi ngazi ya jimbo kwa manispaa zote tatu Ilala, Kinondoni na Temeke ambao nao watatoa mafunzo hayo kwa wasimamizi wa Kata 36, ujazaji wa Fomu na matumizi ya mashine za BVR.

Amesema wao kama Tume ya Uchaguzi watahakikisha kuwa wanatembelea vituo vyote vya uandikishaji ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zitakazojitokeza.

Ameeleza kuwa kwa kuzingatia wingi wa idadi ya watu katika jiji la Dar es salaam kutakuwa na mashine 3500 zitakazofanya kazi katika vituo 1000 huku kukiwa na wataalam zaidi ya 600 waliopatiwa mafunzo kwa lengo la kukamilisha kazi hiyo na kukabiliana na changamoto zilizojitokeza katika maeneo mengine.

"Kwa upande wa Tume tunaendelea kujipanga ili kuhakikisha kuwa changamoto zilizotokea katika maeneo mengine hazitokei, tunatoa wito kwa wananchi watakaofika kwenye vituo kuandikishwa wawe wamekidhi vigezo vilivyowekwa kulingana na vielelezo vya uraia, na umri" Amesema.

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo kutoka Manispaa za Temeke, Ilala na Kinondoni wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa mafunzo hayo wamesema kuwa mafunzo hayo ya siku 2 yanawajengea uwezo wa kuelewa namna ya kuandikisha wapiga kura, ujazaji wa fomu ,uelewa wa sifa za mtu anayestahili kuandikishwa na matumizi ya mashine za BVR.
 
Back
Top Bottom