Serikali: `Mvua za Lowassa` haziwezekani

mundele

Member
Jun 5, 2009
45
1
Serikali imesema ilitupilia mbali mpango wa kuzalisha mvua kwa kutumia teknolojia ya Mfalme wa Thailand uliokuwa umeombwa na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, alipotembelea nchi hiyo mwaka 2006 kutokana na gharama kubwa za teknolojia hiyo.
Hatua hiyo ilitangazwa bungeni jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Philip Marmo.
Marmo, alisema kama mradi huo ungetekelezwa ungeigharimu serikali kiasi cha sh. bilioni 14.5.
Alisema baada ya kufanya majadiliano na Serikali ya Thailand, ilionekana kuwa zingehitajika ndege mbili za kukodi kwa siku saba kwa ajili ya kupeleka kemikali za kurutubisha mawingu, gharama za kutoa mizigo bandarini na kuisafirisha hadi kwenye kituo cha majaribio, gharama za kukodi maghala ya kuhifadhi kemikali na posho na malazi kwa wataalam ambao wangetekeleza kazi hiyo.
Marmo aliyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Chake Chake kupitia Chama Cha Wananchi (CUF), Fatma Mussa Maghimbi, aliyetaka kujua mpango huo wa serikali umefikia wapi.
Tanzania ilikumbwa na ukame mwaka 2006 na kuilazimisha serikali kutangaza mgawo wa umeme baada ya mabwawa ya kuzalisha umeme kukauka.
Katika jitihada za kupata nishati mbadala, Lowassa alifanya ziara Thailand ambapo alishauriana na wakuu wa nchi hiyo kuangalia uwezekano wa Tanzania kutumia teknolojia hiyo.
CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom