Serikali kuunda tume mpya ya mipango

Kasheshe

JF-Expert Member
Jun 29, 2007
4,694
787
Mambo ya kujadili haya hapa! Kujadili watu imetosha sasa tujadili hoja!

Na Boniface Meena, Bagamoyo:


SERIKALI imeanza mchakato wa kuunda tume mpya ya mipango ili kiwe chombo kikuu cha kutoa dira na mwelekeo wa maendeleo ya nchi baada ya Rais Kikwete kuunganisha Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji na Wizara ya Fedha na uchumi.

Katika maandalizi ya mchakato huo wadau mbalimbali wa uchumi nchini walikutana Bagamoyo jana katika warsha ya siku moja kujadili namna tume hiyo itafanya kazi vipi.

Akifungua warsha hiyo Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo alisema warsha hiyo imekutanisha wadau mbalimbali ili kuelezana majukumu ya tume hiyo mpya.

"Lengo ni kupata mawazo ya wadau mbalimbali ili kujua nini hasa tume ya mipango ifanye katika kuleta maendeleo na kukuza uchumi wa nchi yetu," alisema Luhanjo.

Alisema wadau hao ambao wako nje ya serikali wanaweza kutoa ushauri zaidi utakaoiwezesha tume kufanya kazi kwa ufanisi.

"Nia hasa ni kuondoa umasikini kwani ndiyo changamoto kubwa inayoikabili nchi yetu," alisema Luhanjo.

Alisema kuamua kushirikisha wadau hao ni kutokana na tume ya kwanza kuwa ya kiserikali zaidi na hivi sasa serikali imeamua kuifanya iwe tume huru na shirikishi.

"Kazi za tume zitakuwa ni za kufikiri zaidi na kufanya utafiti na siyo kuwa na utafiti wa ndani tu bali hata nje ya nchi," alisema Luhanjo.

Alisema tume hiyo itahusika kusaidia sekta zote za serikali hasa katika suala la mipango.

Naye Gavana wa Benki Kuu Beno Ndulu alisema kuanzishwa kwa tume hiyo kutasaidia kwani serikali imekuwa ikifanya kazi bila mipango kwa muda mrefu na huu ni wakati mzuri kuwa na chombo kitakachoshirikisha wananchi ili kusaidia kufikia malengo.

Alisema tume hiyo itakuwa huru na kuweza kufanya tathmini ya mipango bila kuwa na vikwazo vya kiutendaji kutokana na kushirikisha wadau wa nje ya serikali.

Naye Profesa Samuel Wangwe alisema tume hiyo itatakiwa kuweka kipaumbele chenye dira na maendeleo ili maendeleo yaonekane hasa kwa kutumia rasilimali zilizopo hapa nchini akitolea mfano madini.

Alisema kushirikisha wadau ni vizuri lakini mipango iwe na mikakati ambayo itaweza kufikia malengo na sio kushirikisha wadau kwaajili ya mipango tu halafu utekelezaji ukawa duni.
 
Ameunganisha wizara tangu februari, yaani miezi sita yote ndio kwanza serikali imeanza mchakato... kweli tuna safari ndefu
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom