Serikali ilichakachua ushauri wa jaji mkuu?

mzambia

JF-Expert Member
Dec 31, 2010
885
60
Daniel Mjema
SAKATA la kutohojiwa kwa matokeo ya urais limechukua sura mpya baada ya kubainika kuwa, Mahakama ilikwisha agiza kuundwa kwa sheria itakayoruhusu kuchunguzwa kwa matokeo hayo na ikataka ianze kutumika katika uchaguzi mkuu wa vyama vingi wa mwaka 1995.

Agizo hilo lilitolewa Januari 3, 1995 na jopo la majaji watatu, Jaji Robert Kisanga, Jaji Lameck Mfalila wakiongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Marehemu Francis Nyalali wakati walipokuwa wakitoa hukumu ya rufaa iliyowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) dhidi ya Dk Walid Kaborou aliyeshinda kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kigoma mjini mwaka 1994.

Uchaguzi huo ulifanyika mwanzoni mwa mwaka 1994, baada ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Rajabu Mbano (CCM)

Katika uchaguzi huo, Azim Premji (CCM) alishinda, lakini Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Tabora chini ya Jaji Lawrence Mchome ikatengua ushindi wake.

Suala hili limebainika wakati Rais Jakaya Kikwete juzi alitangaza kuunda tume ya kuratibu mchakato wa kuundwa kwa katiba mpya ambayo itakwenda sawa na mabadiliko ya kichumi na kisiasa yaliyopatikana kwa miaka 50 ya uhuru.

Alisema jukumu la msingi la Tume hiyo litakuwa ni kuongoza na kuratibu mchakato utakaowashirikisha wananchi wote vikiwemo vyama vya siasa, wanasiasa, wafanyabiashara, asasi za kiraia, mashirika ya dini, wanataaluma na makundi mbalimbali ya watu wote, katika kutoa maoni "wayatakayo kuhusu Katiba ya nchi yao".

Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili umebaini kuwa agizo la Majaji hao halikufuatwa na badala yake serikali ikawasilisha muswada mwingine bungeni wa marekebisho ya katiba ili matokeo ya urais yasihojiwe na chombo chochote.

"Kutokuwepo kwa kifungu cha sheria kinachoruhusu kuhoji na kuchunguza kwa matokeo ya urais katika uchaguzi unaoshirikisha vyama vingi inashangaza na kutokuwepo kwake ni mwanzo wa kukaribisha vurugu,'' inaeleza sehemu ya hukumu iliyotolewa na majaji hao.

Hukumu hiyo ambayo gazeti hili imeiona, ukurasa namba 176 wa taarifa za sheria au Tanzania Law Reports (TLR), ya mwaka 1996, ilishauri kufanyika kwa mabadiliko ya sheria ya uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu 1995.

"Jambo la mwisho tunalotaka kulisisitiza hapa hasa kuhusiana na uchaguzi mkuu wa rais na wabunge (1995) ni kuwepo kwa upungufu katika sheria ya uchaguzi hasa katika uchaguzi wa urais,

"Hatuoni kifungu chochote kinachozungumzia kuhoji matokeo ya urais, hatuelewi kwa nini upungufu huu haukurekebishwa katika marekebisho ya sheria hiyo ya mwaka 1985 na yaliyofanywa mwaka 1992,'' walihoji majaji hao.

Wakaongeza: "Sehemu ya VII inayohusika na kubatilisha matokeo ya ubunge haikutumiwa kwenye matokeo ya urais, kusahaulika huku kunashangaza."

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, Majaji hao waliagiza kufanyika kwa marekebisho ya sheria hiyo ili kuruhusu kuhojiwa matokeo ya urais kabla ya uchaguzi mkuu wa urais mwaka 1995 utakaohusisha vyama vingi.

Uchunguzi umebaini badala ya serikali kufanyia kazi ushauri huo, mwaka 2005 iliamua kuifanyia marekebisho Katiba ya Tanzania ya 1977 na kulifanya suala la kutohojiwa matokeo ya urais kuwa la kikatiba.

Badala ya kurekebisha sheria ya uchaguzi, serikali ikaingiza kwenye katiba ibara ya 41 (7), lengo likiwa ni kuhakikisha hukumu ya jopo hilo la majaji haitumiwi na mawakili kama mwongozo (authority) wa maamuzi ya mahakama.

Ibara hiyo inasomeka "Iwapo mgombea ametangazwa na Tume ya uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa Rais kwa mujibu wa ibara hii, basi hakuna mahakama yeyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.''

Tayari wadau mbalimbali wakiwemo Wanasheria na Majaji wamependekeza kuandikwa kwa katiba mpya walisema kifungu hicho cha Katiba kama hakitafanyiwa marekebisho huenda kikawa kiini cha umwagaji damu nchini.

¡§Kama kweli tuna demokrasia kwa nini tunafunga milango ya kuhojiwa kwa matokeo ya Urais? tunatakiwa tuwe mfano ifikapo 2015 tuwe na katiba mpyaÿ sio hata mtu akifunga goli kwa mkono linahesabiwa ni goli¡¨alisema wakili mmoja.

Novemba mwaka jana wabunge wa Chadema walisusia hotuba ya Rais Kikwete bungeni wakipinga mchakato wa matokeo ya urais katika uchaguzi mkuu haukuwa mzuri.

Pia walitaka kuundwa kwa katiba mpya, tume huru ya uchaguzi na kutaka matokeo ya urais yawezi kuhojiwa.

Wadau mbalimbali wamekuwa wakipaza sauti wakitaka kuwepo kwa katiba mpya na katika kauli ya hivi karibuni kabisa, mwanasiasa mkongwe nchini, Peter Kisumo aliitaka CCM isiogope kuongoza mabadiliko ya katiba.

Katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 31, 2010 ambao unalalamikiwa na Chadema, mgombea wa chama hicho, Dk Wilbroad Slaa alipata kura 2,271,941 nyuma ya Rais Jakaya Kikwete aliyeibuka mshindi kwa kura 5,276,827.

Wadau wanapendekeza ili kudumisha amani na mshikamano, katiba irekebishwe ili kuwepo na kipindi cha mpito kabla ya Rais kuapishwa ili matokeo yaliyompa ushindi yaweze kuhojiwa endapo kuna malalamiko kutoka kwa wagombea.

SOSI: MWANANCHI

WAZO LANGU:
KATIBA MPYA TU HAKUNA KINGINE
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom