Elections 2010 Seif: Nitatimiza Ndoto Ya Karume

X-PASTER

JF-Expert Member
Feb 12, 2007
11,610
1,809
Seif: Nitatimiza Ndoto Ya Karume

Salim Said

KATIBU mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad ametangaza vipaumbele 10 katika uongozi wake iwapo atachaguliwa kuwa rais wa Zanzibar, akisema kuwa anakusudia kuifikisha Zanzibar kule alikokusudia muasisi wa taifa hilo, Hayati Abeid Aman Karume.

Katika taarifa yake ya shukrani kwa wanachama wa CUF iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, Maalim Seif alisema kuwa mambo hayo kumi yatakuwa chachu muhimu katika kuhakikisha kuwa Zanzibar inafikia kule ambako Hayati Karume alikusudia.

“Mambo haya pia yatakuwa msingi wa ilani ya uchaguzi ya CUF kwa upande wa Zanzibar,” alisema Maalim Seif.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni kuyaendeleza maridhiano ya kisiasa waliyoyaasisi pamoja na Rais Karume ambayo alisema ni njia sahihi ya kujenga umoja wa kweli miongoni mwa Wazanzibari, kuendeleza amani na utulivu uliopo kwa kufuata misingi ya ukweli na mapatano; kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na kuimarisha Muungano.

“La nne ni kujenga uchumi imara kwa kuzingatia mfumo wa soko huria unaotoa fursa ya ushiriki kwa wananchi wote utakaoratibiwa vyema na serikali, ili kuhakikisha wananchi wanafaidika na fursa hizo na kunyanyua hali zao za maisha katika hali ya neema na tija kwa wote,” alisema Seif.

Alisema serikali yake itaimarisha nidhamu ya utendaji kazi serikalini na ubora wa huduma zinazotolewa na watumishi wa umma, kwa kusimamia ipasavyo kanuni za kazi, kuwapatia mafunzo ya kazi na kuwaongezea mishahara wafanyakazi, ili wafanye kazi zao kwa ufanisi na kuwa mfano kwa umma.

Maalim Seif alisema serikali yake itafuata mfumo wa uchumi wa soko huria, kuirudisha Zanzibar katika hadhi yake ya kituo kikuu cha biashara na huduma katika eneo lote la Afrika Mashariki, kuvutia uwekezaji mkubwa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuimarisha bandari na viwanja vya ndege.

Alitaja mambo mengine kuwa ni kuendeleza kilimo na kukirejeshea hadhi yake; kuweka msukumo maalum katika kuinua viwango vya elimu katika shule zetu za msingi, sekondari hadi vyuo vikuu, kuinua na kuimarisha huduma za afya katika hospitali, zahanati na vituo vya afya na kurejesha maadili mema ya Wazanzibari kwa kuhuisha mila, silka na utamaduni wetu na kuwarejeshea wazanzibari hadhi na fahari yao iliyotokana.

Alisema ana uhakika kuwa CUF itaibuka mshindi katika uchaguzi huo baada ya mazingira ya uchaguzi kurekebishwa.

“Maridhiano ya Wazanzibari yaliyoanzishwa na rais wa Zanzibar ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Amani Abeid Karume, na mimi Novemba 5, 2009, yamebadilisha kabisa sura na mahusiano ya kisiasa baina ya wananchi wa Zanzibar na hasa wafuasi wa CUF na CCM,” alisema Maalim Seif.

Alisema kuna uwezekano wa uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa uliopangwa kufanyika Oktoba 2010, kufanyika katika mazingira ya uhuru, haki na uwazi.

“Rais Karume amekuwa akisisitiza mara kadhaa kwamba hilo ndilo lengo lake na la serikali yake kuona uchaguzi wa mwaka huu unakuwa huru na wa haki, ambao utawafanya washindani wote waridhike na kusiwepo na malalamiko yoyote ukiondoa yale yanayotokana na makosa ya kibinadamu,” alisema Maalim Seif.

Maalim Seif, ambaye amegombea nafasi hiyo mara tatu bila ya mafanikio, alisisitiza kuwa “imani yangu ni kwamba Rais Karume ataisimamia kauli hiyo kwa vitendo”.

“Hivyo basi, naamini katika mazingira hayo na tukishirikiana wanachama wote wa CUF kufanya kampeni kabambe za kisasa na za kistaarabu, hapana sababu kwa nini tusishinde uchaguzi huu na kuiongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,” alisema maalim Seif.

Alisema utofauti mwingine wa mazingira ya uchaguzi wa mwaka huu ni kwamba, matokeo yake yataifanya Zanzibar kuanzisha muundo mpya wa serikali ya umoja wa kitaifa.

“Najua kuwa hili litategemea maamuzi ya wananchi katika kura ya maoni itakayofanyika Zanzibar Julai 31, 2010, lakini mimi naamini kabisa Wazanzibari wamechoshwa na hali ya magomvi, chuki na uhasama, iliyodumu kwa miaka 50 sasa, hivyo basi kwa umoja wao na kwa asilimia kubwa sana watapiga kura ya ndio kuridhia muundo huo mpya wa serikali,” alisema Maalim Seif.

Maalim Seif alitaja mambo 10 ambayo yatakuwa msingi wa uongozi wake iwapo atafanikiwa kuingia ikulu ya Zanzibar katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
 

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom