Saratani ya tezi la kibofu inatibika

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,315
33,108
”CHEMBECHEMBE za uhai katika tezi la kibofu zinapoanza kukua bila kufuata utaratibu na mfumo wa mwili-zinaasi na kutengeneza viumbe vidogo vidogo, hapo mtu anakuwa amepata saratani ya tezi ya kibofu…” anasema Mchungaji Canon Dk. Emmanuel Kandusi.

Dk Kandusi ambaye ni mwathirika wa satarani ya tezi la kibofu, Mratibu wa Kampeni ya Tanzania 50 Plus Campaign anathibitisha, “Ndugu yangu mimi ni mwathirika wa saratani ya tezi ya kibofu, kimelea cha saratani kilianza kukua katika tezi akiwa na umri wa miaka 50 (1997), miaka kumi baadaye dalili za mwanzo zilijitokeza.”

Mwathirika wa saratani anawaonya wanaume wote wenye umri wa kuanzia miaka 50 na kuendelea kujitokeza kupima ili kubaini kama wana saratani ya tezi la kibofu kwa lengo la kupatiwa matibabu.

Wakati wa uzinduzi wa vipeperushi vya saratani ya tezi la kibofu vya Taasisi ya Tanzania 50 Plus Campaign, Daktari Mshauri wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Pascience Kibatala, alitoa mwito kwa wanaume wiki iliyopita Dar es Salaam kuwa waachane na imani potofu kuwa saratani ya tezi ya kibofu ni ugonjwa wa wazee.

Saratani ya tezi la kibofu huwapata wanaume tu wenye umri wa miaka 50 na zaidi, utafiti unaonyesha kuwa satarani hii imeshika nafasi ya pili katika kusababisha vifo kwa wanaume wakati inayoongoza ni saratani ya mapafu.

“Magonjwa ya saratani yameongezeka kwa kiasi kikubwa nchini. Kati ya wagonjwa wote, asilimia kumi ndio waliopatiwa matibabu na kwa saratani ya tezi ya kibofu, hatuna takwimu kamili, lakini madaktari wameona kuna ongezeko la wagonjwa wanaoenda hospitalini wakiwa wamechelewa na wengine wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa huo,” alisema Dk. Kabatala.

Saratani hiyo hutambuliwa na kugunduliwa katika hatua ya kwanza hadi ya nne. Katika hatua ya kwanza na ya pili, ikigunduliwa matibabu yanakuwa rahisi, katika hali hiyo waathirika wa saratani hiyo wanatakiwa kuwahi hospitalini kupata matibabu.

Watu wanaochelewa kwenda hospitalini kwa sababu ya kuona haya wakidhani wamepata maambukizi ya magonjwa ya zinaa kama kisonono, wanakosea.

Wanatakiwa kujua kuwa mara zinapoanza kujitokeza dalili wajue mara nyingi saratani hii huwa tayari imo mwilini mwa mwathirika kwa zaidi ya miaka saba au minane. Wanaume wasihofu kwenda kuchunguza afya zao kwa hofu ya kwanza wameambukizwa magonjwa ya zinaa, kwani dalili zake zinafanana na zile za magonjwa ya kuambukiza ya zinaa.

Wapo wanaume wanaohusisha saratani hiyo na kuugua kutakosababishwa na mambo ya kishirikina kama kulogwa, dhana ambayo ni potofu, lakini pia wasihofu kwenda hospitalini kwa kudhani kuwa wameugua ugonjwa wa hatari wa mabusha au wa wanywa gongo.

Wapo wanaouchukulia ugonjwa wa saratani ya tezi la kibofu kama ni ‘gonjwa la utu uzima,’ kana kwamba saratani hiyo ni haki ya mzee kuugua, jambo ambalo linawafanya watu wengi wachelewe kwenda hospitalini kuchunguza afya zao, kumbe wanaweza kuwa wanaumwa.

Matokeo ya kusambaza dhana hizo potofu, kumechangia watu wengi kwenda kwa waganga vichochoroni na kujitafutia tiba isiyo na msaada.

Baadaye wanajikuta wamezidiwa ndipo wanahaha kwenda hospitalini wakiwa tayari wamechelewa, au wakati mwingine ugonjwa unakuwa katika hatua za mwisho na wanapoteza maisha, wakati wangeyaokoa.

Vifo vinavyotokana na kuchelewa kutibiwa saratani ya tezi la kibofu, vinasababishwa na ukosefu wa elimu kuhusu ugonjwa huo wa saratani hususani saratani ya tezi la kibofu.

Tanzania 50 Plus Campaign imeamua kuondoa ugonjwa huo kwa kutoa elimu kwa kutumia vyombo vya habari lakini pia kwa kuchapicha vipeperushi.

Imelenga kutoa elimu juu ya ugonjwa huo, unaotesa na kuua wanaume wengi wenye takribani miaka 50 na kuendelea.

“Okoa maisha, unga mkono kampeni za taasisi hii,” anasema mratibu wake Dk. Kandusi. Saratani haina mipaka ya nchi, Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Afrika Kusini, Desmond Tutu, Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela na Dk. Emmanuel Kandusi ni waathirika wa ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa Dk. Kibatala, wanaume wengi hawaendi hospitali kwa sababu wanahisi kuwa wana magonjwa ya zinaa, kwani dalili za saratani hiyo zinafanana na dalili za magonjwa ya zinaa.

Wengine hawaendi kwa sababu wana imani za kishirikina na wanaamini kwamba wanaoumwa ni wazee tu na watu wanaotumia gongo.

Kutokana na dhana hiyo, inayotokana na kukosa elimu, wanaume wengi huenda kwa waganga na matokeo yake, hupelekwa hospitali wakiwa wamechelewa na wengine kufa kwa sababu ya kukosa matibabu.

Dk. Kabatala anaiomba Tanzania 50 Plus Campaign kushirikiana na taasisi nyingine katika kutoa elimu kuhusu ugonjwa huo.

Hata kama tayari wamechagua wilaya ya Kongwa kuwa mradi darasa, ambapo wazee watafanyiwa uchunguzi, watakaopatikana kwa kushirikiana na ndugu wa wagonjwa watapatiwa matibabu.

Daktari Mwandamizi wa taasisi hiyo, Jerome Nkiramweni anasema saratani ya tezi la kibofu, huwapata wanaume wenye umri wa miaka 50, ugonjwa ambao hutokana na chembe za tezi la kibofu zinapoanza kukua bila kufuata utaratibu wa mfumo wa mwili na hivyo kutengeneza uvimbe mdogo.

Baadhi ya dalili za ugonjwa huo, ni kwenda haja ndogo mara kwa mara kunakoambatana na maumivu au kutoa damu, kunakuwa na maumivu ya kiuno au kwenye mapaja hasa mguu wa kushoto, lakini pia unawasha wakati wa haja ndogo, pamoja na kukosa hamu ya kula na kupungua uzito.

Ugonjwa huo unaweza kukaa mwilini kati ya miaka saba hadi 10 na ndipo dalili zake huanza kujitokeza wazi. Kutokana na haja ya kutoa elimu ya ugonjwa huo kwa umma, Tanzania 50 Plus Campaign, kwa ufadhili wa Global Campaign Against Poverty (GCAP)- Tanzania Alliance-SAHRINGON (T), imetengeneza vipeperushi kwa Kiswahili na Kiingereza, vinaelezea saratani ya tezi la kibofu ni ugonjwa gani.

Vipeperushi hivyo vinaonyesha namna ugonjwa huo unavyoanza na namna ulivyo hatarishi, lakini pia unabainisha dalili zake, namna uchunguzi unavyofanyika pamoja na tiba zake, lakini pia vinaonyesha ushuhuda wa waathirika wa saratani.

Mwanamume mwenye umri wa miaka takribani 50 na kuendelea, anatakiwa kwenda hospitalini kumwona daktari ili achunguze afya yake lakini pia kufanya uchunguzi wa tezi za kibofu, badala ya kuamini kuwa haumwi.

Kwa madaktari, vipeperushi hivyo vinawakumbusha kuwa mara wanapowapata wagonjwa wenye umri wa miaka 50 na kuendelea, wawashauri kuwa pamoja na kupata matibabu za maradhi mengine, wafanye uchunguzi wa saratani ya tezi la kibofu.

Dk Kandusi anasema alianza kusumbuliwa na ugonjwa huo mwaka 1997 lakini mpaka juzi, miaka takribani 10, dalili za mwanzo za ugonjwa zilianza kujitokeza. Mwaka jana alizidiwa, lakini kwa msaada wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, alikwenda Hospitali ya Indraprastha Apollo nchini India, huko uchunguzi wa kina ulifanyika na jopo la madaktari, akachagua upasuaji badala ya sindano ambayo ni zaidi ya Sh 650,000, anaishi kwa kidonge aina ya bicalutimide gramu 50 kila siku na ataendelea kwa miaka miwili.

Dk Kandusi anasema, “Mimi nimerudi na nawapeni ushuhuda… “Nisingependa wanaume wengine wapate mateso ninayopata kutokana na kuchelewa kugundua ugonjwa…” Wazee wasisubiri hadi dalili zinajitokeza, wanatakiwa kuweka kipaumbele tabia ya uchunguzi wa afya kwa ujumla na wanapofikia umri wa miaka 50 na kuendelea, uchunguzi wao ujumuishe uchunguzi wa tezi ya kibofu angalau mara moja kwa mwaka.

Dalili za mwanamume mwenye saratani ya tezi za kibofu, anakuwa dhaifu katika kujisaidia haja ndogo na unapotaka mkojo unakatizwa, lakini pia mwathirika wa ugonjwa huo anashindwa kukojoa na kushindwa kuanza kupata haja ndogo. Mtu anakuwa katika hali ngumu anashindwa kupata haja ndogo na wakati mwingine hasa usiku haja inatoka yenyewe, anaweza kukojoa kitandani.

Kampeni ya Tanzania 50 Plus Campaign inaenda sambamba na Sera za Afya pamoja na Mpango wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umasikini (Mkukuta) na Millennium Development Goal (MDG) VI, ambayo inatoa fursa shirikishi kwa asasi zisizo za kiserikali katika masuala ya afya, kitaifa na kimataifa.

Wizara ya Afya inapongeza Kampeni ya Tanzania 50 Plus Campaign kuwa itaendelea kutoa ushirikiano ili kuelimisha umma wa Tanzania kuhusu madhara ya saratani ya tezi la kibofu kwani ‘ikigundulika mapema ni rahisi kutibika.’

http://www.habarileo.co.tz/makala/?n=3633
 
MziziMkavu said:
Dalili za mwanamume mwenye saratani ya tezi za kibofu, anakuwa dhaifu katika kujisaidia haja ndogo na unapotaka mkojo unakatizwa, lakini pia mwathirika wa ugonjwa huo anashindwa kukojoa na kushindwa kuanza kupata haja ndogo. Mtu anakuwa katika hali ngumu anashindwa kupata haja ndogo na wakati mwingine hasa usiku haja inatoka yenyewe, anaweza kukojoa kitandani.

Ahsante kwa kutupatia hizo dalili, kazi kwetu
 
asante saana kwa elimu iliyo bora kwetu sisi na familia zetu. Wengine wazee wetu wamefikia umri huu 50+ kwahiyo ni bora tukirudi krisimasi tuwajulishe habari hii muhimu! Lakini sijaona sehemu wazee WANAWAKE wamezungumziwa au ni kwa wanaume pekee?
 
Back
Top Bottom