Salam za Mheshimiwa Balozi Maajar katika Kusherehekea Sikukuu

M

MegaPyne

Guest
Salam za Mheshimiwa Balozi Mwanaidi Sinare Maajar katika Kusherehekea Sikukuu ya Eid El-Hadji, Noeli Na Mwaka Mpya 2008


Ndugu Watanzania wenzangu na wote wenye mapenzi na nchi yetu mlioko hapa Uingereza na Jamhuri ya Ireland.

Tumejaaliwa kupata fursa ya kusherehekea sikukuu ya Idd El-hadji huku tukisubiria sikukuu ya Noeli na Mwaka Mpya.

Kwa niaba ya Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwa niaba ya wafanyakazi wenzangu katika Ubalozi wa Tanzania London, na kwa niaba yangu binafsi napenda kushirikiana nanyi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kufikia kipindi hiki muhimu.

Katika kipindi cha mwaka mmoja Ubalozi wenu umekuwa ukijitahidi kuwajibika kibalozi na kushirikiana kwa namna mbalimbali na Watanzania walio katika eneo letu la uwakilishi.

Katika kipindi hiki pia tumejitahidi kupigania kuimarisha mshikamano wa Watanzania na hatimaye kufanikiwa kuunda upya Jumuiya ya Watanzania baada ya kuwa kimya kwa muda. Ni matumaini yetu kuwa Watanzania watailinda na kuiinua Jumuiya yao kwa mafanikio yao na Taifa letu kwa ujumla.

Watanzania tuna sifa kubwa ya kuheshimiana, kuvumiliana na kushikamana bila kujali itikadi zetu za kisiasa, imani zetu za dini au kabila au rangi. Ni matumaini yetu tutaendelea kudumisha mshikamano wetu siku zote tukifanya kazi kwa bidii ili tuchume ugenini na kuweza kuijenga nchi yetu.

Katika kusherehekea sikukuu hizi muhimu natumaini tutakuwa na fursa nzuri ya kutembeleana na kuimarisha mshikamano kati yetu.

Nawapeni nyote mkono wa Eid El Hadji, mkono wa sikukuu ya Noeli na kuwatakia kheri ya Mwaka Mpya ujao.

Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania.


Balozi Mwanaidi Maajar
 
Back
Top Bottom