Sakata La Mgomo Wa Madaktari; Tafsiri Yangu

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246
Ndugu zangu,

Mgomo wa madaktari wetu ni habari kubwa. Umeingia sasa kwenye wiki ya pili. Hata kama
ungekuwa ni wa siku mbili, bado ungesababisha madhara makubwa kwa nchi. Kwamba
sasa una zaidi ya siku kumi na nne ni balaa kubwa kwa nchi yetu.

Tafsiri yangu;

Uliopo ni mgogoro kati ya madaktari na Serikali. Na kwenye mgogoro kama huu, siku zote,
wenye kuathirika zaidi ni wananchi walio wengi.

Ni ukweli, kuwa karibu kila Mtanzania anayeamka asubuhi, ama ni mgonjwa au ana ndugu,
jamaa au rafiki aliye mgonjwa.

Hivyo basi, kuna mamilioni ya Watanzania wenye kutaabika kila siku na maradhi ya aina mbali mbali. Ni
Watanzania wenye kutegemea sana huduma ya tiba inayotolewa na madaktari wetu. Na katika nchi
zetu hizi, daktari ni rafiki muhimu sana wa mwananchi.

Ni jambo baya sana, pale Serikali inapoingia kwenye mgogoro na madaktari. Inapoingia
kwenye mgogoro na marafiki wa wananchi. Hakuna mahali popote duniani wananchi
wakatokea kuwachukia madaktari.

Hivyo basi, ni balaa pia pale Serikali inaposhindwa kumaliza tofauti zake na madaktari wa
wananchi kwa njia ya mazungumzo na hata kufikia hatua ya madaktari kugoma.

Katika nchi zetu hizi, mganga wa tiba aliyesomeshwa kwa fedha za walipa kodi na kwa miaka
mingi anahitajika sana. Mganga wa tiba msaidizi anahitajika sana. Na hata kama angelikuwapo
Msaidizi wa Mganga Msaidizi wa tiba , naye angehitajika sana. Vivyo hivyo kwa wakunga wakuu
na wasaidizi, wauguzi wakuu na wasaidizi wao. Wote hao wanahitajika sana.

Na katika nchi zetu hizi, Serikali hazipaswi kufikia hatua ya kuwatisha na hata kuwafukuza kazi
madaktari. Hilo la mwisho lifanyike tu pale ambapo njia nyingine zote za kumaliza tofauti na
kusuluhisha migogoro na madaktari zitakapokuwa zimeshindikana. Na kwanini ishindakane?

Tufanye nini sasa?

Taarifa kwamba Kamati ya kudumu ya Bunge inayohusika na masuala ya huduma za jamii
imepanga kukutana na madaktari wetu ni hatua njema na ya busara. Maana, katika mgogoro
huu taarifa zimekuwa zaidi za upande mmoja; upande wa Serikali. Ni wakati sasa pande zote
mbili zikasikilizwa na Kamati hiyo ya Bunge. Ndio, ni wakati pia hata madaktari wetu wakapewa
nafasi tuwasikie.

Huu si wakati wa kufanya ’ propaganda’ za kisiasa kwenye masuala ya afya za wananchi.
Na hata pale Waziri wa Afya alipokaririwa jana Bungeni akitamka kuwa hali ya huduma za
mahospitalini zimerejea katika hali yake ya kawaida ni mfano wa ’ Propaganda’ za kisiasa
ambazo Watanzania hatuzihitaji kwa sasa.

Hivi ni hali gani hiyo iliyorejea kwenye kawaida yake
kwenye hospitali zetu baada ya mgomo huu wa madaktari unaoendelea sasa? Kwamba askari
wetu wa Jeshi la Wananchi wamelazimika kwenda kutibu wagonjwa Muhimbili hiyo haiwezi
kuwa ni ’ Hali ya kawaida’. Kwamba madaktari wameripoti lakini hawaonekani mawodini hiyo
haiwezi kuwa ’ hali ya kawaida’. Na kama ni kawaida, hivi ni nini tafsiri ya ’ kawaida’?

Hapa kuna ukweli unaopaswa kusemwa, na si kitu kingine bali ni ukweli. Watanzania tunataka
kujua; ni kwanini watendaji wa Wizara husika wameshindwa kulitatua suala la madaktari wetu
na hata kutufikisha hapa tulipo?

Yumkini, kulikuwa na hali ya kuyapuuzia madai ya madaktari
katika hatua za awali. Yawezekana pia watendaji wa Wizara hawakuwa karibu na wawakilishi
wa madaktari hao ili kutoa fursa ya kuongea na kutafuta ufumbuzi wa tatizo. Labda ndio maana
tumefika mahali sasa mgogoro umekomaa na wahusika kuonyesha hali ya kutunishiana misuli.
Kuna mahali kosa limefanyika. Ni wapi?

Ndio hapa, kuwa hata kama Kamati ya Bunge itafaulu kusuluhisha mgogoro huu, bado
Watanzania tutahitaji iundwe Tume huru itakayochunguza namna watendaji wa wizara husika
walivyolishughulikia suala hili kwa upande wao.

Tume hiyo itusaidie kuupata ukweli mzima ili kama taifa, tujifunze. Na wakati tume kama hiyo
itakapokuwa ikifanya kazi yake, itakuwa ni busara, kwa watendaji wakuu wa wizara husika
wajiweke pembeni kwa maana ya kujiuzulu ili kupisha uchunguzi huo.

Kama Tume itabaini kuwa hakukuwa na mapungufu makubwa katika utendaji wao na hususan walivyolishughulikia suala
hili la mgogoro na madaktari, basi, itajulikana hivyo, na wana nafasi ya kurudi tena kwenye
nafasi za utendaji Serikalini. Inahusu umma kurudisha imani yake kwa Serikali yao. Ndio maana
ya umuhimu wa wahusika kupisha pembeni kuruhusu uchunguzi ufanyike. Maana, haitakuwa
busara kuliacha suala hili likapita kama yanavyopita mengine ilihali limegharimu maisha ya
Watanzania.

Na kubwa zaidi kwa sasa, ni kwa pande zote katika mgogoro huu kutambua; kuwa kwa sasa
mvutano unaoendelea hautatoa mshindi, ni kwa vile, katika kilichotokea na kinachoendelea
kufanyika sasa, sote, kama taifa, tumeshindwa.

Huu ni wakati wa kutanguliza busara na hekima. Tufanye yote, lakini, njia mujarab ya kutanzua
mgogoro huu uliopo sasa ni mazungumzo katika mazingira ya kuheshimiana, basi.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

Maggid Mjengwa,

Dar es Salaam,
Jumamosi, Februari 4, 2012
Mjengwa Blog::Habari,Picha,Matangazo
 
Mimi hilo la bwana mponda kusema kuwa huduma za afya zimerudi katika hali ya kawaida kwenye hospitali za rufaa ndo limenishtua. Mimi nipo kcmc, mainterns wanaendelea na mgomo na tangu j4 madaktari wakazi(residents) nao walianza mgomo, hali ni mbaya sana kwa kweli. Juzi malasusa alikuja kuongea na madaktari but hawakumsikiliza. Madaktari bingwa wameelemewa sana na wanasema kama mpaka j3 hali itakuwa hivyo hivyo watashindwa kuendelea na kazi
 
Yaani hawa viongozi wetu wanatufanya sisi hatuoni yanayoendelea mahospitalini, tutakuwa wajinga mpaka lini, Tanzania is gone with Mwalimu.
 
Yaani hawa viongozi wetu wanatufanya sisi hatuoni yanayoendelea mahospitalini, tutakuwa wajinga mpaka lini, Tanzania is gone with Mwalimu.
Mwalimu hayupo sisi tuliopo tuna nafasi gani ya kuibadili hii nchi?
 
Back
Top Bottom