Said Mwema - Kuwa shemeji ya Rais ni leseni?

Well, kwa waandishi wa habari wanachojaribu kupigia kelele kwa sasa ni kauli ya "mkuki kwa nguruwe, kwa binadamu mchungu". Ndugu zanguni hakuna binadamu atakayesalimika anapoachia uovu upite naye amekaa kimya kwa sababu yoyote ile. Iwe ni maslahi toka kwa watawala waliopo au iwe ni chuki binafsi dhidi ya anayefanyiwa unyama. Nionacho mimi mkuki huu kule Morogoro alipigwa nguruwe ndiyo maana waandishi hawakupiga kelele kiasi hiki huku wakijua ukweli wa mambo. Lakini kwa Nyololo kapigwa binadamu ndiyo maana kelele ni nyingi. Tumezoea kuona waandishi wakipokea vijibahasha kwenye mikutano (press conference) kisha aidha kunyamazia ukweli fulani au kuupindisha sababu ya vibahasha hivyo. Walidhani watasalimika wakiendelea kukaa kimya. Sasa leo wanyamazishaji wametafuta wa kunyamaziha hawamuoni wamewageukia "washikaji" wa siku zote. Sasa huu ni wito kwa waandishi kutonyamazia ukweli wauonapo bila ya kujali nani anaonewa, vinginevyo tunawaweka waandishi kwenye kundi moja na watawala dhalimu
 
Me nikisikia Chagonja mwili unasisimka,hakuna polisi anayenipa hasira kama Chango-njaa.
 
Imeandikwa na Lula wa Ndali Mwananzela kwenye gazeti la Raia Mwema toleo la 256

INGEKUWA kwenye nchi ambayo ina utawala wa sheria na haki za kiraia na zile za kibinadamu hushikiliwa kama tunu, basi, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema na Kamanda wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Kamishna Paul Chagonja wangekuwa wameshaondolewa kwenye nyadhifa zao, kutiwa pingu na tayari wanatumikia vifungo virefu jela. Bahati mbaya katika nchi kama ya kwetu utawala wa sheria unawafuata watawala walio juu ya sheria. Ndugu zangu, matukio ya mauaji ya mara kwa mara hasa katika mazingira ya kisasa yanavyozidi kutokea najikuta nafikia hitimisho la kuudhi kuwa uongozi wa Jeshi la Polisi ambao umeshindwa, unalindwa na wanaoulinda wananufaika na vitendo vya ukiukwaji wa haki za raia na haki za binadamu.

Kwa mara nyingine taifa letu limeanza wiki hii na habari ya kushtua ya kifo cha kijana mmoja mjini Morogoro ambaye taarifa za


awali zimedai kuwa, alikuwa ni muuza magazeti ambaye hakuwa sehemu ya maandamano lakini alijikuta anapatwa na mauti baada ya kupigwa na silaha (haijulikani kama ni risasi au bomu la machozi). Lakini hili limetokea tena katika mazingira ya kisiasa zaidi na kuwa ni sehemu ya mlolongo wa matukio ya aina hii ambayo taifa limeyashuhudia kwa miezi kadhaa sasa kama si miaka. Nitawakumbusha wasahaulifu.

Mwezi Juni, mwaka jana huko Mara Jeshi la Polisi lilituhumiwa kumuua mwananchi aliyekuwa nyumbani kwake na mkewe kwa kumdhania kuwa ni jambazi. Askari wa Kituo cha Mugumu (Serengeti) walifika nyumbani kwa Nyitamboka Mwita (28), usiku wa manane na kumuamuru atoke ndani. Kilichofuatia baada ya hapo hakijulikani sana lakini moja linalojulikana ni kuwa dakika chache baadaye Mwita alikuwa ameuawa kwa kupigwa risasi ya mgongoni. Hilo lilikuwa tukio la nne la mauaji ya wananchi kufanywa na polisi wa kituo hicho katika kipindi cha muda mfupi tu.

Mwezi Januari, mwaka 2011 huko Mbarali Mbeya Jeshi la Polisi hilo hilo lilihusika na mauaji ya raia wawili ambao walikuwa ni miongoni mwa wananchi waliokuwa wamesimama kupinga kupita kwa lori lenye uzito mkubwa kwenye eneo lililokatazwa malori mazito kupita.

Nani atasahau tukio la Februari mwaka huu huko Songea, Jeshi la Polisi lilijikuta kwenye kashfa nyingine ya mauaji ya raia wanne ambao kosa lao lilikuwa kuandamana dhidi ya Mkuu wa Mkoa na dhidi ya uongozi wa polisi wa mkoa. Tukio hili likawafunua viongozi uchwara ambao kwa haraka wakadai ati watafanya uchunguzi na kuahidi kuwa tukio kama “hilo lisitokee tena”. Hata mwaka haujaisha limetokea na siwezi kushangaa linaweza kutokea tena huko Iringa!

Na hapa hatujagusia kabisa yale mauaji ambapo yamedaiwa kuwa “polisi yaua majambazi” kiasi kwamba tuhuma tu kuwa mtu ni jambazi zinatosha kabisa kupitisha hukumu ya kifo. Na hapa hatujagusa maeneo mengine ambapo watu wamefia mikononi mwa polisi tena wengine wakiwa chini ya ulinzi! Hatujagusa wengine ambao wanapigwa tu wanapokuwa mikononi mwa polisi na kuja kufa baadaye kutokana na majeraha yao.

Na hapa sijagusa mauaji yale yaliyotokea Arusha au yale ya Mbeya! Tukio hili la Morogoro haliwezi kuwa la mwisho na halitakuwa la mwisho kwa kadiri ya kwamba Said Mwema, Charles Chagonja na uongozi wa juu wa jeshi la polisi bado unabakia ule ule, wenye fikra zile zile za kibabe na ambalo linaamini liko kwa ajili ya kuwalinda watawala wasichukiwe!

Swali linalonisumbua (naweza kuhisi jibu lake hata hivyo) ni kuwa ni kina nani wanawalinda viongozi hawa wa polisi kiasi kwamba wanaweza kuacha ubovu uendelee kutokea na wao kuendelea kupiga saluti bila kujali matokeo. Imekuwaje – naendelea kujiuliza- jeshi ambalo linajitapa kuwa ni la ‘usalama’ wa raia kugeuzwa kuwa ni jeshi la ‘uhasama na raia”. Hivi ni kweli kina Chagonja na Mwema hawajui kuwa haki ya kuandamana kuipinga serikali au hata kupinga jambo fulani katika hali ya amani ni haki ya msingi kama vile kupiga kura? Ni lini watatambua kuwa wananchi kuandamana katika mkutano wa kisiasa ni jambo zuri na la kawaida? Hivi ni kweli katika upeo wao wa fikra wao na watendaji wao wa chini hawana uwezo wa kutoa ulinzi tu kidogo kuhakikisha kuwa maandamano yanakuwa katika njia zilizokubaliwa na yanakuwa salama? Mbona inaonekana jeshi lina polisi wengi wa kuvunja maandamano kuliko wanaohitajika kulinda maandamano?

Lazima kuna watu wanawalinda hawa. Upande mmoja naamini ni wakubwa serikalini ambao wanawatumia hawa kama mabosi wa kikoloni walivyotumia jeshi la mkoloni. Matokeo yake maofisa hawa wa polisi hawajioni kuwa wanatumikia wananchi na wanawajibika kwa wananchi bali wanajitahidi kujitafutia ujiko mbele ya wakubwa zao ambao ni wanasiasa. Ni ulinzi huu unazama zaidi hasa tunapokuja kugundua kuwa kumekuwapo na ujamaa au udugu kati ya Mkuu wa Jeshi la Polisi na Rais Kikwete (wanaitana mashemeji). Je, inawezekana ni huu ushemeji ambao unafanya hata kumuuliza Mwema kwa nini inatokea, haiwezekani? Je, inawezekana ni huu ugumu kiasi kwamba hata wabunge wameshindwa kutaka awajibishwe au kuwajibika kwani wanajua watamchongea vipi shemeji ya Rais?

Lakini pia wengine ambao wanalinda uongozi huu mbovu wa Jeshi la Polisi ni viongozi wenyewe wa upinzani. Hawa kina Mbowe na wengine wamekuwa watumishi wa kwenda kuzika mashabiki na wanachama wao huku wakiahidi “haki ya Mungu” nyingi! Ni lini watatambua kuwa tatizo ni uongozi wa Jeshi la Polisi? Uongozi ambao umejikita katika kukandamiza haki za kiraia ili kuwafurahisha watawala walioshindwa? Ni lini kina Mbowe na wale ambao wanajiona ni viongozi wa upinzani watafunga safari kwenda kwa Said Mwema na Chagonja na kumpa ujumbe usio na utata kuwa hawatovumilia tena Jeshi la Polisi kuua wananchi katika mikutano yao na kuwa ikitokea tena basi hapatakalika? Je, inawezekana ni upole huu wa vitendo ndiyo umewapa nguvu kina Chagonja na walio chini yao? Nani atawafokea?

Ndugu zangu sisi wenyewe wananchi ndiyo tunawalinda pia kwa sababu licha ya kuwa tunaona wanavyofanya dhidi ya ndugu zetu tunafikiri kuwa haiwezi kututokea sisi wenyewe au jamaa zetu hivyo tunaamua kuwa washirika wa ukimya. Hatutaki kusema.

Binafsi nasema – na Mungu awe shahidi yangu – Said Mwema na Chagonja wanatakiwa watu wa kwanza kutiwa pingu kwa matumizi mabaya ya madaraka na wanastahili kushtakiwa kwenye Mahakama ya Uhalifu wa Kivita kule The Hague, Uholanzi. Kwani chini yao wananchi wetu wengi wameuawa huku wao wakiendelea kula na kunywa vitamu vya jeshi. Wakitabasamu mbele ya saluti na kucheua mbele ya vimulimuli!

Ni matumaini yangu kuwa kuna mtu atawaambia hawa kuwa vitendo vyao vinahesabiwa na siku moja watasimama kujibu na kulipa. Kama Gaddafi alianguka na kulipa na Saddam na wauaji wake wote waliondolewa na kulipa hata hawa –na wale wanaowalinda- watakuja kuondoka tu. Na hawatoondoka bila kwanza kulipa gharama ya ubovu wao wa kiuongozi. Tuwaapie mbele ya haki ya Mungu kuwa siku moja watalipa tu vitendo viovu vinavyotokea chini yao na wao wakivitetea.

Watalipa kwani damu za ndugu zetu zinalia ardhini zikidai haki “mnidaie mnidaie” kama vile damu ya Habili aliyeuawa na yule muuaji wa kwanza Kaini na hazitonyamaza hata kama ni kizazi kingine. Watalipa tu, walahi watalipa. Hata katika mikono ya wajukuu wetu watalipa. Mungu atupe nguvu siku moja tuwalipishe.

---

Sehemu ya pili, Imeandikwa na Lula wa Ndali Mwananzela kwenye gazeti la Raia Mwema toleo la 257


VIONGOZI wa Polisi bado ni wale wale, wakilindwa na watu wale wale, na wakiendelea kutenda vile vile na mikononi mwao damu ya Watanzania ikiendelea kumwagika.

Nilipoandika makala yangu wiki iliyopita iliyohoji ni nani anawalinda viongozi wa juu wa Polisi ambao chini yao mauaji ya kinyama ya wananchi yametokea sikutarajia kuwa ukweli wake ungeendelea kuthibitika tena na kurekodiwa mbele ya macho ya mamilioni ya Watanzania.

Mauaji ya mwandishi wa kujitegemea na Mwenyekiti wa Chama cha Wandishi wa Habari tawi la Iringa Daudi Mwangosi yameligusa Taifa letu wakati bado maswali ya mauaji ya kijana muuza magazeti kule Morogoro yakiwa hayajapata majibu.

Kilichoshtua zaidi si tu kuwa ameuawa katika mazingira ya kisiasa lakini zaidi ni jinsi gani aliuawa. Kwamba mtu anaweza kulipuliwa hadharani na mwili wake kuachwa wazi kana kwamba ni mnyama inatosha kabisa kuudhi!

Lakini ni jeshi hili hili – kama watu wanakumbuka – ambalo maofisa wake walichukua miili ya maiti kule Nyamongo na kuiacha barabarani kwenye majeneza baada ya kujaribu kulazimisha familia zao ziwachukue? Ni kitu gani kinaendelea hapa? Inawezekana vipi mauaji haya yanaendelea kutokea na viongozi wa juu wa jeshi hili bado wanakalia viti vyao?

Kinachonishangaza zaidi ni ukimya wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje inayoongozwa na Edward Lowassa. Nilitarajia baada ya tukio la Songea la Februari, Lowassa na kamati yake wangeamua kukutana na uongozi wa jeshi kujua ni nini kinaendelea, lakini hakufanya hivyo.

Baada ya tukio la Morogoro nilitarajia labda kamati hii, ambayo ni sauti ya wananchi kwenye masuala ya usalama, ingejaribu kukutana na uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wa Polisi ili kuweza kuona jinsi gani nchi inaweza ikavumilia shughuli za kisiasa bila kulazimisha Polisi kutumia nguvu. Sasa kwa tukio hili la mauaji ya Mwangosi sitarajii kama Lowassa anaweza kuongoza kamati yake kwenda kutafuta ukweli.

Hili linanifanya nijiulize maswali mengi kama Lowassa na timu yake ya kamati wanajali maisha ya Watanzania au la. Kama wanajali ni kwanini wako kimya?

Ni kwanini wakati kamati nyingine zimeenda kutembelea wizara, ofisi na hata maeneo ya mbali na Dar es Salaam, na hata yenyewe majuzi ilikaa sana nje ya nchi wakati Bunge likiendelea, ili kuweza kufuatilia, kamati hii hata mara moja haijaenda kukutana na polisi na uongozi wa CHADEMA, haijajaribu?

Inawezekana vipi hata kukemea Polisi hawakemei na hata kuhoji hawahoji? Au ndiyo wanaamini serikali iko sahihi kuua wananchi wake na wao kwa vile ni sehemu ya watawala hao basi wanatoa baraka zao kwa ukimya wao?

Ni nani anawalinda? Je, yawezekana vyombo vya habari ambavyo leo vinaonekana vimeshtuka vimekuwa kimya muda mrefu na havijafanya kampeni ya kutosha kuonyesha uovu wa serikali? Je, vyombo vya habari havijaamua kukaa kimya na kuendelea kuripoti kuhusu kina Mwema, Chagonja na makamanda wengine licha ya kuhusishwa kwao na uongozi mbovu wa jeshi la Polisi? Leo wandishi hawa hawa wanashtuka kwa sababu mwenzetu kauawa? Walipokufa vijana kule Songea chini ya Kamanda huyu huyu wa Iringa waandishi hawakuona? Si Polisi waliua Arusha na Mbeya? Si hawa hawa wanatuhumiwa kuua Tarime? Kwanini vyombo vya habari vinafikiria Mwema na Chagonja wanastahili kuendelea kuongoza Jeshi?

Inashangaza hadi leo hii hakuna gazeti au chombo hata kimoja cha habari ambacho kwenye tahariri yake kimetaka viongozi hawa wawajibike! Kwanini? Wanaogopa? Wanawalinda?

Binafsi naamini kwa kadiri tunavyoendelea kushuhudia mauaji ya namna hii na kwa kadiri wanasiasa, wananchi na vijana wetu wana vyoendelea kukaa kimya ndivyo nao vile vile wanavyoamini kuwa wanaweza kufanya lolote kwa yeyote.

Si walimbeba mzobemzobe Freeman Mbowe na kumuweka kwenye ndege ya Jeshi? Si hawa hawa waliwapiga virungu viongozi wa CHADEMA pale Arusha na kumwaga damu ya Bi. Josephine Slaa na dunia ikaona lakini tukawaacha? Yawezekana ni njama hii ya ukimya ya watu wa vyombo vya habari leo vimeleta kuku kuatamia!?

Lakini ni nani hasa anawalinda?

Yawezekana ni wanasiasa wa chama tawala ambao wanaamini Polisi inawalinda wao na serikali yao. Ndiyo maana huwezi kuona wanasiasa wa chama tawala wakisimama na kutetea haki ya CHADEMA kuandamana au kupinga?

Yawezekana ukimya wao ni kwa sababu wanajua kuwa Polisi wanawafanyia kile ambacho wao wenyewe hawawezi kukifanya? Kwamba kwa kadiri ya kwamba wanaonyanyaswa, kutawanywa na kuuawa ni wale wanaohusiana na CHADEMA basi wao watu wa CCM wako salama na hivyo wanakaa pembeni na kusema “mkome”!?

Je, yawezekana kuna mtu wa juu zaidi ambaye ananufaika na unyanyasaji na uvunjaji wa haki za binadamu unaofanywa na Polisi? Je, mtu huyo inawezekana ananufaika kwa sababu anajua kuwa jeshi linamlinda na kulinda sifa ya serikali yake?

Je, yawezekana ni hawa wanaotoa maagizo ya kuzuia mikutano ya CHADEMA wakijua kabisa kuwa CHADEMA watadai haki hiyo na wao wataamuru Polisi wafanye ‘kazi’?

Maana ukiangalia sana utaona kuwa Polisi hawakuwa na sababu yoyote ya kiakili ya kujaribu kuwatawanya mashabiki na wanachama wa CHADEMA pale Nyololo.

Katika kulewa ulanzi wao wa madaraka, Polisi waliamua tu bila kujali lolote kutumia nguvu kubwa kuwatawanya watu ambao hawakuwa tishio kwa namna yoyote ile.

Mlolongo wa mauaji ya raia mikononi mwa Polisi iwe katika mazingira ya kisiasa au wakati wanapokuwa chini ya ulinzi wa Polisi unahitaji kutufanya tujiulize swali. Kwanini watendaji wakuu wa Polisi hawaguswi. Kwanini wanaosimamia mafunzo na operesheni wakiongozwa na Paul Chagonja hawaonyoshewi kidole? Wanaogopwa? Wanalindwa?

Na nani?




Source: Mwema, Chagonja, Ni Nani anawalinda? Na kwa nini? - wavuti
 
Me nikisikia Chagonja mwili unasisimka,hakuna polisi anayenipa hasira kama Chango-njaa.

Nenda ofisini kwani kaazime bomu la machozi nasikia ukijitambulia kwamba unatoka jamiiforums anakupa bila shida.
 
mwandishi amejiuliza swali la upande mmoja tu kwani chadema wanalindwa na nani?

acha kujifanya hujui, chadema ndio waathirika wa mauaji kwenye mikutano yao, halafa unauliza chadema wanalindwa na nani.?
 
Back
Top Bottom