Safari ya mwisho ya Hanga uwanja wa ndege wa Dar es salaam

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,908
30,249
Nimegundua kitu kimoja katika tabia za watu wanaoishi kwa hofu ya kusema kweli wakiogopa labda wenye mamlaka wanaweza wakawadhuru. Wataujua ukweli lakini hawatausema hadi wasikie mtu mwingine kazungumza ukweli ule.

Katika hali kama hiyo na wao watatoka huko walikujificha na kuingiza maneno mawili matatu ya kusadikisha ukweli ule. Binafsi nina mifano ya watu wakubwa tu katika nchi hii ambao baada ya kunisikia nikuzungumza au kuandika mambo ambayo kabla ya mimi kuyasema ilikuwa mwiko kusemwa basi na wao watayazungumza wengine kwa faragha kwa jamaa zao na wakati mwingine hadharani ingawa hii si mara nyingi kusadikisha ukweli ule.

Sasa watu hawa wanapozungumza ile ithibati ya jambo lile huwa imekamilika. Ingekuwa si kuhofia kuwaudhi watu hawa ambao waliniunga mkono kwa yale niliyoandika au kusema ningelitaja majina yao na habari zenyewe walizothibitisha. Lakini kwa kuwa mazungumzo yetu yalikuwa ya faragha nina wajibu wa kuheshimu usiri ule.

Siku moja niko msikitini akanijia mtu mzima mmoja akaniambia kuwa ana sahib wake kanisikia nikifanya kipindi katika radio kuhusu historia ya Zanzibar na nimemtaja Abdulla Kassim Hanga. Huyu bwana akanambia kuwa huyo sahib wake alikuwa akijuana na Hanga toka utoto wao Zanzibar na ana jambo angependa kunieleza kuhusu kifo cha Hanga.

Yule bwana alifika msikitini petu siku ya pili na tukajulishwa. Huyu bwana ni mtu mzima kiasi cha miaka 80. Nilimkaribisha nyumbani na tukakaa kwa ajili ya mazungumzo yetu. Rafiki yake yeye alisema atabaki msikitini kumsubiri. Baada ya mazungumzo mafupi ya hili na lile tulianza mazungumzo yetu.

Mimi nilimuomba nifanye, ‘’recording,’’ ya mazungumzo yetu lakini alikataa akasema hapana haja ya kuyanasa mazungumzo yetu katika chombo. Sikupata tabu nilimwelewa. Nikamuomba nimpige picha hali kadhalika alikataa na nilimwelewa na hata nilipotaka anipe jina la kampuni aliyokuwa meneja wa shirika la ndege na ndiyo hiyo kuwa sababu ya yeye kuwa pale Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam siku Hanga aliporudi safari yake ya mwisho akitokea Cairo pia hakupenda kuniambia.

Nami nilimwelewa kwa yote hayo. Baada ya haya nikawa tayari nishamwelewa mapshaji wangu habari sasa kilichobaki ilikuwa kwangu mimi kumtoa hofu atulie ili aniahdithie kisa kile vizuri.

Huyu bwana anasema:

‘’Mimi nilikuwa meneja wa kampuni moja ya ndege hapa Dar es Salaam na kila ndege yetu ikija Dar es Salaam mimi nilikuwa uwanjani kuipokea. Siku ile wakati niko pale uwanjani majira ya mchana nikamuona mkewe Hanga, Bi. Mkubwa, pale uwanjani. Nikamfuata kumsalimia na nikamuuliza mbona yuko pale.

Jibu alilonipa Bi. Mkubwa ni kuwa, ‘’Kassim anakuja na Egypt Air nimekuja kumpokea.’’ Mimi nilishtuka sana kupita kiasi kwa sababu hapa mjini Dar es Salaam sisi jamaa kutoka siku zile Zanzibar tulikuwa tunafuatilia kwa karibu na tunapata taarifa ya kila jambo lililokuwa linatokea Zanzibar khasa katika mambo ya kamatakamata na mauaji.

Taarifa ambazo zilizokuwa zikizunguka katika duru zetu kuhusu Hanga zilikuwa zinatisha kwa hiyo niliamini Hanga yeye ingawa alikuwa nje ya nchi bila shaka jamaa na marafiki zake watakuwa wameshamtahadharisha. Ndege ilipotua nilikwenda hadi chini ya ngazi kumpokea Hanga huku akili yangu ikenda mbio vipi nimpate Hanga faragha lau kama kwa muda mchache nimfahamishe kuwa maisha yake yapo hatarini. Wakati tunatembea kutoka nje ya jengo nilimkaribisha chakula cha mchana kabla hajakwenda kwake.

Tulikaa kwenye ‘’restaurant,’’ pale uwanjani tukala na baada ya kula nilipata faragha na Hanga. Sikuuma maneno yangu nilimweleza Hanga yote yaliyokuwa yakisemwa kuhusu yeye kule Zanzibar kama nilivyozipokea. Nikamwambia, ‘’Abdulla nakusihi ndugu yangu usiingie hata mjini rudi na ndege hii hii hali si nzuri kwako.’’

Hanga alinikatalia. Ilikuwa Qadar ya Allah. Hakika jitihada ya binadamu haiwezi kufuta aliloandika Allah. Tukaagana lakini aliniacha na moyo mzito sana. Nikamsindikiza Hanga na mkewe Bi. Mkubwa hadi kwenye gari wakaondoka kuelekea mjini. Hapo hapo nikampigia simu Ali Nabwa wakati ule yeye akifanya kazi Tanganyika Standard.

Nilikutana na Nabwa jioni ile na tulimtafuta Hanga kote hatukumpata. Nabwa alikuwa anafanyakazi Tanganyika Standard kwa hiyo alipiga, ‘’stop press,’’ ameagiza gazeti lisichapwe lisubiri habari kubwa ya Hanga kurejea nchini. Usiku tukampata Hanga Oyster Bay nadhani kwenye nyumba iliyokuwa ya Kambona.

Baada ya mazungumzo tuliamua twende kwa Maalim Muhammad Matar Magomeni tukafanye dua. Tulifika kwa Maalim Matar na tuliomba dua pale kuomba salama ya Hanga. Siku ya pili habari kubwa ya Tanganyika Standard ilikuwa kurejea kwa Hanga nchini. Habari hii ilikuwa katika ukurasa wake wa mbele.

Haukuchukua muda Hanga akatiwa mbaroni na akapelekwa Ukonga Prison na kutoka hapo akarejeshwa Zanzibar baada ya kufedheheshwa katika ule mkutano mashuhuri uliohutubiwa na Nyerere pale Mnazi Mmoja. Baada ya mkutano ule Hanga akarejeshwa Zanzibar na huo ndiyo ukawa mwisho wake.’’
***
Napenda kuongeza kitu. Ingawa kichwa cha habari kinaeleza kuwa hii ilikuwa safari ya mwisho ya Hanga. Ukweli ni kuwa ilikuwa safari yake ya mwisho akitokea nje ya nchi. Safari yake ya mwisho ilikuwa alipopita tena uwanjani pale wakati akirejeshwa Zanzibar kukabiliana na mauti.

Atakae kusoma habari zaidi za historia ya Zanzibar atapata habari hizo katika kitabu cha Dr. Harith Ghassany, ''Kwaheri Uhuru Kwaheri Ukoloni,'' kitabu kinapatikana:

Ibn Hazm Bookshop Msikiti wa Mtoro na Manyema
Tanzania Publishing House, Samora Avenue
Elite Bookshop Mbezi Samaki


HN3zyUwRMm7qCKqDFCI4TgEeJnYI0Fujb9HiDaLXSTdhayhkx7rPj-z3Ze-G7iJIRQf24FVXrN8DnZDp6xvzvy116vuFZ1Zc-fAOUk9NrqErvLG5u2TbsQwNdU1UmLPv-QPtGtd_Aiemwfb4BSBs9fjk5o-xE1_mZ1pri5s9DAy45aOWjKwOSAyLKqGbULUr350z6rYpofpPkC-p2ifGeQiH7utPW4YDxfFHiMQU-xQgiUf5DFDpHoLlWJvydfqAtQn7sghwLNtCTd9C65GqWZO3QzRTz4dRZrv8Bc97dntP6u0lF820XLAuDpC18JvluowdPzmv1nhXh12eSJ8Ph83ZghzOOHwc88ibPZ_EvgC_VWymDdIPvP5qDUoZa5eTmd753gVfg_Z-nT1H1FV9qvEmzEXQvML4B_YXpjH5u4mR2oyH8kx2jDNkSsglnvEc6d3hTp2l-YhGwBjksJRswOgzhtG6ud6OIGIPAfutaKM-IN0xI93gkXvHZP-GbsAcAiR9WsNGtAXmBZDuUKvUCWLnG7NzxH9QqQewdukFzCQrM88dqC3V5kFkSfHcZ6Hx6-3QSaKcSZj43vX8-rnlGViqYng-gMxVkKJbspHsFQ98VDBh=w831-h623-no
 
Kwa heri mkoloni,,,,,,, kwa heri uhuru,,,,,, Kisa cha kweli kabisa kilichotokea Tanzania na kufukiwa Ardhini na wenye macho kufumba macho wasione, kuziba masikio wasisikie na kuziba mdomo wasiseme.
 
Back
Top Bottom