Sababu tano kipigo cha Stars

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
KIPIGO cha mabao 5-1 ilichokipata timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ juzi kutoka kwa Misri ‘Pharaos’ kimetokana na sababu tano za msingi, huku kikiwa kimemchanganya Kocha Mkuu, Mdenish Jan Poulsen.

Moja ya sababu iliyotajwa na Kocha Poulsen ni kwamba Stars ilifungwa na timu bora Afrika.

“Tumecheza na timu bora, huwezi ukalinganisha nafasi ya 116 tuliyopo Tanzania na wao wapo katika 20 bora za dunia, pia ndiyo namba moja Afrika. Misri ni timu nzuri, imecheza vizuri, ni mabingwa mara tatu mfululizo Afrika, vijana wangu walipambana vilivyo, lakini walikutana na timu bora, naamini michezo ijayo tutaimarika,” alisema Poulsen.

Kocha huyo alisema, makosa machache waliyoyafanya wachezaji wake, yalitumiwa vizuri na wapinzani wao kufunga na hiyo ilitokana na kucheza bila kuelewana dakika 20 za mwanzo.

Sababu ya pili inayoelezwa na wadau wa soka nchini ni pamoja na ushindi wa Stars kwenye michuano ya Chalenji iliyomalizika nchini mwezi uliopita.

“Ushindi wao kwenye Kombe la Chalenje, nao umewachongea Stars, hivyo Misri ilikamia kwa kuweka wachezaji wake wote maarufu, wakijua inacheza na bingwa wa CECAFA mwaka huu,” alisema mmoja wa wadau wa soka nchini.

Sababu ya tatu ni kutoelewana kwa timu nzima, hasa safu ya ulinzi pamoja na kipa namba moja nchini, Juma Kaseja, ambao juzi walicheza chini ya kiwango.

Kuna wakati Kaseja alitaka kupigana na Nadir Haroub ‘Canavaro’ baada ya beki huyo kujifunga bao la tatu akiwa katika harakati za kuokoa, jambo lililopunguza kuelewana zaidi.

Kaseja mwenyewe ambaye umaarufu wake nchini uliongezeka wakati wa michuano ya Chalenji, alishindwa kucheza mipira kadhaa ya krosi iliyochangia kipigo hicho, kutokana na kupungua kwa umakini wa mabeki wa pembeni.

Sababu ya nne ni washambuliaji wa kati na pembeni, ambao walizidiwa ujanja na wachezaji wa Misri walioonekana kuwa na miili mikubwa ikilinganishwa na wa Stars
Sababu ya tano ya kichapo cha Stars, imetolewa na Nahodha wa Stars, Shadrack Nsajigwa, ambaye alisema kuwa hali ya baridi kali ya Misri, iliwachanganya kiasi Fulani, hasa kipindi cha kwanza, lakini baadaye walichangamka wakati tayari mambo yameharibika.

Aliwaomba Watanzania wasikatishwe tamaa na matokeo hayo na kukumbusha kuwa, hata michuano ya Chalenji iliyomalizika mwezi uliopita jijini Dar es Salaam timu ya taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ ilianza kwa kufungwa bao 1-0 na Zambia, lakini ikaja kuibuka bingwa.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Misri, Hassan Shehata, aliisifu Stars na kusema inahitaji marekebisho kidogo, lakini itakuwa nzuri.

Alisema, mpira ambao Stars ilicheza kipindi cha pili, kama ingecheza hivyo kipindi cha kwanza, mchezo ungekuwa mgumu kwao na kusisitiza kuwa timu yake licha ya kupata ushindi mnono, lakini ilikabiliana na upinzani mkubwa.

Naye nahodha wa Misri, Wael Goma alisema michuano hiyo ya soka kwa nchi za Bonde la Mto Nile ni migumu na kwamba Tanzania si timu ya kubezwa, kwani ina wachezaji wenye miili midogo, lakini wana vipaji.

Stars juzi ilikubali kipigo hicho, ambapo bao la kwanza lilifungwa na Said Khamdi, dakika ya nne, kisha dakika 10 baadaye Mohammed Aboutrika alifunga la pili na dakika tisa baadaye beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akajifunga.

Bao la nne lilifungwa na Said Khamdi dakika ya 57, wakati lile la mwisho lilifungwa na Ahmed Ally dakika ya 74 na la Stars lilifungwa na mchezaji aliyetokea benchi Rashid Gumbo dakika ya 77.

Kesho Stars itacheza na Burundi ambayo nayo juzi ilifungwa mabao 3-1 na Uganda, hivyo ili Stars iweke hai matumaini ya kufuzu nusu fainali italazimika kushinda na kusubiri mchezo wa mwisho dhidi ya Uganda.
 
nakubaliana na sababu hii tu
Moja ya sababu iliyotajwa na Kocha Poulsen ni kwamba Stars ilifungwa na timu bora Afrika.
"Tumecheza na timu bora, huwezi ukalinganisha nafasi ya 116 tuliyopo Tanzania na wao wapo katika 20 bora za dunia, pia ndiyo namba moja Afrika. Misri ni timu nzuri, imecheza vizuri, ni mabingwa mara tatu mfululizo Afrika, vijana wangu walipambana vilivyo, lakini walikutana na timu bora, naamini michezo ijayo tutaimarika," alisema Poulsen
 
nakubaliana na sababu hii tu
Moja ya sababu iliyotajwa na Kocha Poulsen ni kwamba Stars ilifungwa na timu bora Afrika.
"Tumecheza na timu bora, huwezi ukalinganisha nafasi ya 116 tuliyopo Tanzania na wao wapo katika 20 bora za dunia, pia ndiyo namba moja Afrika. Misri ni timu nzuri, imecheza vizuri, ni mabingwa mara tatu mfululizo Afrika, vijana wangu walipambana vilivyo, lakini walikutana na timu bora, naamini michezo ijayo tutaimarika," alisema Poulsen

Ni kweli tumezidiwa kimchezo, visingizio vingine ni kawaida yetu wabongo kila tunapofanya vibaya. Si zamani sana, Egypt hawa hawa tuliwahi kuwaomba friendly wakatufunga 5 sijui tulishasahau?
 
Back
Top Bottom