Rushwa Yaombwa Kumtoa Rumande!

X-PASTER

JF-Expert Member
Feb 12, 2007
11,610
1,809
Rushwa yaombwa kumtoa rumande mchungaji

2009-03-08 11:37:55
Na Thobias Mwanakatwe, Mbeya

Sakata la Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Evangelistic Church, Cosmas Mwasenga anayetuhumiwa kukutwa na viungo vya albino limeingia katika sura mpya.

Inadaiwa kuwa amejitokeza mtu mmoja na kwenda nyumbani kwa Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Zebadia Mwakatage, akimuomba ampe rushwa ya Sh. 150,000 ili akawashawishi polisi wanaopeleleza kesi hiyo wamwachie huru mchungaji wake.

Mtu huyo (jina tunalo) mkazi wa Mwanjelwa jijini Mbeya alifika nyumbani kwa Askofu Mwakatage na kumuomba kiasi hicho cha fedha Machi 4, mwaka huu akidai ametumwa na polisi wanaopeleleza kesi hiyo na kumhakikishia kuwa kama atatoa fedha hizo Mchungaji Mwasenga (mtuhumiwa) ataachiwa huru.

Kufuatia tukio hilo, Mwandishi wa habari hizi baada ya kupata taarifa hizo alifika nyumbani kwa Askofu Mwakatage eneo la Simike na kujitambulisha kuwa yeye ni mtoto wa Askofu Mwakatage na ndipo mahojiano yalianza kati ya mtu huyo na mwandishi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi (aliyejifanya mtoto wa Askofu Mwakatage) mtu huyo alisema yeye ametumwa na askari watatu na kuwataja majina (majina tunayahifadhi) kwamba kama anataka mchungaji wake aachiwe huru atoe Sh. 150,000 kwa sababu ameonewa kwa kuhusishwa na tukio la kukamatwa na viungo vya albino.

Katika hali ya kushangaza Afisa mmoja wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) alipopigiwa simu kwa ajili ya kujulishwa kuhusu tukio hilo, alipofika eneo la tukio alikataa kumkamata mtu huyo kwa madai kuwa ni raia wa kawaida lakini angekuwa polisi angemkamata.

Afisa huyo licha ya kufika karibu na eneo la tukio Simike nyumbani kwa Askofu Mwakatage akiwa katika gari la Takukuru, baada ya kuelezwa mkasa ulivyo aliamua kuondoka zake na hivyo kumuacha mtoa taarifa solemba asijue la kufanya.

Mtu huyo mwenye umri kati ya miaka 50 na 60 ambaye alikuwa amevalia kinadhifu shari, suruali, tai na mkononi akiwa ameshikilia begi dogo, alisema alitumwa na askari hao ambao kimsingi hawakubaliani na jinsi mazingira yalivyo ya kukamatwa kwa mchungaji huyo.

Alisema amekuwa akishirikiana na polisi katika mipango ya kupanga mikakati ya kuwakamata wahalifu na yeye kunufaika kwa kupewa mgawo wa fedha za uchunguzi zinazotolewa na Jeshi la Polisi kwa askari wake na kwamba tangu ameanza kazi hiyo amefanikiwa hata kujenga nyumba yake eneo la Mwanjelwa.

Aliongeza kuwa tukio la kukamatwa mchungaji wa kanisa la Pentekoste Evangelistic Church, Cosmas Mwasenga yeye binafsi limemsikitisha na kwamba mbali na kazi ya uchungaji amekuwa akijishughulisha na kazi ya uhunzi wa kufua vyuma.

Mtu huyo alisema baadhi ya polisi ambao wamekerwa na kitendo cha kukamatwa mchungaji huyo hivi sasa wanafanya mikakati ya kuwashawishi wananchi wa kijiji cha Idiwili kilichopo kata ya Iyula wilayani Mbozi anakotoka mchungaji Mwasenga (mtuhumiwa) ili waandamane kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kushinikiza haki itendeke dhidi ya mchungaji huyo.

Habari kutoka kijijini hapo zinaeleza kuwa mchungaji huyo ambaye kazi yake inayompatia kipato ni ya uhunzi inadaiwa alipelekewa silaha tatu na watu wasiojulikana wanaodhaniwa kuwa majambazi na kumtaka azikate vitako.

Waliongeza kuwa hata hivyo mchungaji huyo hakuifanya kazi hiyo na ndipo watu hao waliporejea nyumbani kwake na kumuuliza kwanini hajafanya kazi waliyomtuma na kuanza kumtisha ambapo baada ya siku mbili wakashitukia akikamatwa na kuhusishwa na biashara ya viungo vya albino.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Zelothe Stephen, akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu alisema hajapata taarifa za tukio na kwamba atahakikisha mtu huyo anakamatwa.

Hivi karibuni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Zelothe Stephen, akizungumza na waandishi wa habari alisema mchungaji Mwasenga pamoja na mwenzake Luseshelo Mwashilindi walikamatwa na viungo vya binadamu vinavyosadikiwa kuwa vya albino ambavyo walikutwa wakiviuza kwa Sh. milioni 30.

Alisema walikamatwa Februari 13, mwaka huu baada ya polisi kupata taarifa kuwa kuna watu wanauza viungo vya albino na hivyo polisi kuweka mtego uliofanikisha wakakamatwa.

Alisema Februari 12 mwaka huu polisi walipata taarifa kutoka kwa raia wema kwamba kuna kikundi cha watu katika mji wa Mlowo wilayani Mbozi wana viungo vya bindamu vinavyodhaniwa kuwa vya albino ambao walikuwa wakiwatafuta wateja wa kuvinunua.

Kamanda Stephen alisema watu hao walizagaa kutafuta wateja wa kununua viungo hivyo hadi katika maeneo ya Mwanjelwa na Makungulu Jijini Mbeya na ndipo polisi walipoweka mtego wa kumtafuta mtu wa kuvinunua ambapo alipotafutwa muuzaji walikubaliana kwa bei ya Sh.Milioni 30 na kwamba vitu hivyo vilikuwa vimehifadhiwa nyumbani kwake mjini Mlowo.

Alisema hata hivyo kwa kuwa kiasi hicho cha pesa kilikuwa kikubwa, mnunuzi alimuomba muuzaji ampe muda wa kutafuta pesa zaidi ili kufikia kiwango hicho anachohitaji na ndipo siku iliyofuata Februari 13 polisi walifanya maandalizi ambapo walifika nyumbani kwa Luseshelo Mwashilindi ambaye alitoa vipande viwili vya binadamu na papo hapo akatiwa mbaroni.

Alisema polisi walifanya upekuzi nyumbani kwa mtuhumiwa huyo ambapo alikutwa na viungo vya biaadamu anayedhaniwa kuwa ya albino,dawa ya bindamu aina ya Penincilim, maji ya kuchanganyia dawa pamoja na koti jeusi ambapo alipohojiwa zaidi alidai alikuwa akishirikiana na Mchungaji wa kanisa la Pentekoste Idiwili, Mchungaji Mwasenga.

* SOURCE: Nipashe
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom