Rushwa ya barabarani inavyoitafuna Njombe

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
266
• Rushwa ya barabarani ni wastani wa milioni 900 kwa mwaka
• Pesa hii inaweza kusomesha watoto 4,500, kununua mifuko
13,000 ya mbolea, na mabati ya nyumba 2,500.
Rushwa imekithiri sana katika jamii yetu kiasi kwamba hata tunasahau ni kiasi gani ina madhara makubwa! Kwanza Jamii imeamua kufanya hesabu ndogo ni kiasi gani rushwa inawagharimu wananchi wa Njombe.

Ni vigumu kujua jinsi rushwa inavyofanyika katika sekta zote za jamii. Kuna rushwa katika utoaji wa huduma za afya, elimu, na katika vyombo vya sheria. Hapa tumeamua kuangalia kwa wastani kiwango cha rushwa katika sekta moja: usafiri. Hii ni kwa sababu rushwa imekithiri katika sekta hii kiasi kwamba wamiliki wa mabasi na malori wanatenga kabisa kiasi fulani cha pesa kwa kila safari kwa ajili ya kuwaonga askari wa usalama barabarani. Tumetumia taarifa hizi kuangalia ni kiasi gani cha pesa kinalipwa kama rushwa na magari ya kibiashara kati ya Njombe na Dar es Salaam kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Barabara ya kuelekea Dar es Salaam ndiyo inayounganisha Njombe kwenye kiini cha uchumi wa nchi yetu, Dar na pia kwa ulimwengu wa nje. Mabasi yanabeba abiria kutoka Njombe kuelekea Dar kwa sababu mbalimbali kama vile kikazi, kibiashara, kifamilia au kimasomo. Pia kuna malori mengi yanayotoka Njombe yamejaa bidhaa mbalimbali kama vile chai, viazi, mbao, mbogamboga, matunda, maua na mahindi kwa ajili ya kuuzwa Dar.

Kusafirisha mazao mbalimbali kwa ajili ya kuuzwa Dar au zaidi ni gharama kubwa kwa sekta ya kilimo hapa Njombe. Gharama za usafirishaji zinapopanda athari yake inamkumba mpaka mkulima anayelipwa bei kidogo kwa mazao yake. Iwapo gharama ya kusafirisha iko chini inamaana mkulima anatakiwa kupata pesa zaidi. Kuna gharama za usafirishaji ambazo hazikwepeki kama vile magari, mafuta na mshahara wa madereva. Rushwa ya barabarani ni gharama isiyo ya lazima ambayo inaathiri kipato cha mkulima wa Njombe.

Kupata kiasi cha pesa zinazotumika kama rushwa, tulizungumza na watu 11 wenye uzoefu kuhusu usafiri katika Njombe na Dar es Salaam. Idadi hii inajumuisha madereva watatu wa malori, dereva wa basi na askari watatu wa usalama barabarani. Tuliwauliza kila mmoja maswali matatu. Ni mabasi na malori mangapi yanayosafirisha bidhaa au abiria kutoka Njombe kuelekea Dar es Salaam kila siku? Je, madereva au wamiliki wa magari hayo wanatenga kiasi fulani cha pesa kwa ajili ya kutoa kama rushwa barabarani? Kama ndiyo, ni kiasi gani cha pesa wanachotenga kwa kila safari?

Ni majibu gani waliyotoa? Majibu yao hayakuwa na utofauti mkubwa sana. Madereva wote na wamiliki wa magari walikiri kuwa wanatenga kiasi cha pesa kwa kila safari. Askari wawili walikiri kuwa wanategemea kupata kitu kidogo kwa kila basi au lori linalowapita huku mmoja wao akikanusha kuwa hategemei kupokea rushwa kutoka kwa magari hayo.
Pia wote walitaja kiasi cha pesa zinazotengwa kuwa ni wastani wa 20,000/- kwa kila safari. Kuhusu idadi ya mabasi na malori yanayoondoka Njombe kuelekea Dar kila siku, majibu yao pia yalifanana wakisema ni kati ya 40 mpaka 100 katika misimu tofauti ya mwaka. Hivyo kwa wastani, magari zaidi ya 60 yanaenda Dar es Salaam kila siku.

Dereva mmoja wa zamani aliiambia Kwanza Jamii, “Unaweza kutumia kati ya shilingi 15,000 mpaka 20,000 kwa safari moja ingawa inategemea gari lako liko katika hali gani. Ila hata kama gari lako nzima lazima trafiki watakuomba uwape hata ya maji. Tena saa zingine hata hawakagui gari lako, anakwambia ‘tutoe bwana si unajua njaa kali’.”

Dereva mwingine wa lori alisema, “tunapoanza safari lazima ujiandae na kiasi kati ya 20,000 na 30,000 kwa ajili ya matrafiki njiani. Hili suala la rushwa hata mabosi wetu (wamiliki wa magari) wanalifahamu sana na ndio wanaotupa hizo pesa. Huu ni utaratibu ambao matrafiki wamejiwekea na sisi tumeuzoea na hali hii imekithiri sana kwenye hii barabara kati ya Njombe na Mafinga.”

Mmiliki mmoja wa gari alisema, “ni kweli huo utaratibu upo wametuzoesha na sisi tumeuzoea ingawa si mzuri lakini inatupunguzia matatizo. Mimi dereva wangu nampatia kama 20,000 au 30,000 kwa kila safari, itumike isitumike mimi sijui.”

Kwa kutumia makadirio haya tunaweza kusema kuwa jumla ya pesa inayotolewa kama rushwa katika barabara ya Njombe-Dar ni milioni 900 kwa mwaka. Gharama hizi zisizokuwa za lazima katika sekta ya usafiri ni hasara kwa mkulima wa Njombe ambaye angeweza kudai bei nzuri kwa mazao yake. Kwa lugha nyingine, Njombe inapoteza kiasi cha shilingi milioni 900 kila mwaka kutokana na rushwa katika sekta ya usafiri.

Pesa hizi zingekuwa mikononi mwa wananchi wa Njombe. wangewekeza hizi pesa kwa ajili ya maendeleo yao na jamii nzima kwa ujumla. Kwa mfano, hizi pesa zingeweza kusomesha watoto 4,500 wa elimu ya sekondari kila mwaka. Pia zingeweza kununua mifuko 13,000 za mbolea kwa ajili ya kilimo au kununua mabati ya kujengea nyumba 2,500 za kiwango cha kati.
 
Aisee nimependa takwimu duh! kama Mh. Magufuli......but inasikitisha sana kwa taifa
maskini kama Tz na hii ni sekta moja tu.
 
Sasa hiyo ela si inarudi kwene mzunguko hukohuko Njombe na kwingineko? Hao wene magari wenyewe wanakaribisha hayo mazingira ya rushwa kwa kutotimiza masherti ya vyombo vya usafirishaji na sheria za barabarani.
 
• Rushwa ya barabarani ni wastani wa milioni 900 kwa mwaka
• Pesa hii inaweza kusomesha watoto 4,500, kununua mifuko
13,000 ya mbolea, na mabati ya nyumba 2,500.


Njombe inapoteza kiasi cha shilingi milioni 900 kila mwaka kutokana na rushwa katika sekta ya usafiri.

Sitetei rushwa hata kidogo - lakini jee Njombe kweli inapoteza kiasi hicho cha pesa kwa mwaka? Jee hao askari si wanazitumia pesa hizo huko huko Njombe? Wanajenga, wanasomesha nk. Hata wakizinywea bado zinaingia kwenye uchumi wa Njombe.

Rushwa ya jinsi hii tatizo lake hasa ni kuchangia ajali za barabarani kwani makosa ya magari huachiwa. Rushwa hii huhamisha tu manufaa kutoka kwa kundi moja kwenda jingine - mfano kutoka kwa walipa nauli wanaoongezewa bei kwenda kwa maaskari.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom