Rostam Aingiza Mkenge TANESCO!

LordJustice1

JF-Expert Member
Jan 19, 2011
2,263
530
rostam_234.jpg


MPANGO wa wamiliki wa kampuni ya Dowans kuizunguka serikali na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ili kujinufaisha kiuchumi umegundulika.

Vyanzo vya habari vya gazeti hili vimesema Dowans wanaandaa mkataba utakaowezesha mitambo yake iliyopo Ubungo, mjini Dar es Salaam, kukodishwa kwa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) ambalo nalo litauza umeme utakaozalishwa kwa TANESCO.

Nyaraka zilizofikia MwanaHALISI zinaonyesha kuwa mazungumzo ya kufanikisha mpango huo yapo katika hatua nzuri kwani tayari TANESCO imejulisha mpango huo kwa Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo.

Menejimenti ya TANESCO iliwasilisha kilichoitwa “mapendekezo ya mpango” mbele ya kikao cha Bodi ya TANESCO kilichofanyika 15 Machi 2011.

Nyaraka zilizopo zinaonyesha kuwa bodi ya TANESCO iliarifiwa katika kikao hicho kwamba Dowans imeomba kuingia katika makubaliano ya “pande tatu” pamoja na CTI yanayohusu uzalishaji wa umeme megawati 100.

“Dalili za awali zinaonyesha CTI na Dowans wapo tayari wakati wowote wiki hii kusaini mkataba,” zinasema nyaraka za kikao cha bodi ya TANESCO.

Wakati TANESCO ikisubiri Dowans na CTI wasaini mkataba wa kukodishana mitambo, Mwenyekiti wa CTI, Felix Mosha amekana mpango huo.

Mosha aliliambia gazeti hili katika mahojiano maalum wiki iliyopita mjini Dar es Salaam kwamba habari za CTI kufanya mazungumzo na Dowans “zimekuzwa tu na baadhi ya watu.”

Alisema ingawa mgao wa umeme umeathiri (sana) sekta ya viwanda nchini, hakuna mkutano au makubaliano yoyote yaliyofanyika kuhusu suala hilo.

“Ndugu mwandishi, sisi (CTI) hatujaamua kununua wala kukodisha mitambo ya Dowans. Hilo ni suala nyeti ambalo mtu au taasisi hawezi kuchukua maamuzi kwa kukurupuka.

“Kwanza, katika hali ya kawaida kabisa, mtu hawezi kuzungumzia kuhusu uamuzi kama huo bila ya kuangalia athari zake. Ni kama kutafuta balaa vile. Wananchi watatuonaje? Serikali itatuonaje?”

“Kwa niaba ya CTI, niseme tu kwamba sisi hatujafanya bado uamuzi kuhusu mitambo ya Dowans na nafikiri kuna watu wameamua kulikuza hili kwa faida ambayo wenyewe ndio wanaoijua,” alisema Mosha.

Taarifa hizo zinaibuka mwezi mmoja baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kutoa amri ya kuzuia Dowans kufanya makubaliano na TANESCO nje ya mahakama.

Hoja juu ya mitambo ya Dowans iliibuka mahakamani wakati wa kutajwa kwa shauri lake linalotaka kusajiliwa kwa tuzo yake
ya Sh. 94 bilioni iliyoshinda katika mahakama ya kimataifa ya Usuluhishi ya Migogoro ya Biashara (ICC).

kampuni ya Dowans ilifungua shauri hilo kwa kile ilichodai, “serikali kuvunja mkataba wake.” Dowans ilirithi mkataba huo kutoka kwa kampuni ya kitapeli ya Richmond Development Corporation (LLC).

Aidha, kuibuka kwa taarifa hizi kumekuja wiki tatu baada ya aliyejiita mmiliki wa Dowans Tanzania Limited (DTL), Brigedia Jenerali Mohamed Sulaiman Al Adawi kudaiwa kuja nchini.

Katika mazungumzo yake na wahariri wa vyombo vya habari, Al Adawi alisema yeye ndiye mmiliki pekee wa Dowans.

Wakati Al Adawi akisema hivyo, nyaraka zinamtaja Bernal Zamora Arce anayejitambulisha kuwa rais wa kampuni hiyo, kuwa ndiye aliyetoa mamlaka ya kisheria ya kusimamia kampuni hiyo kwa Rostam Aziz, mbunge wa Igunga na mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Taarifa zinasema ni katika kipindi hicho, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima na Katibu Mkuu wa wizara, David Jairo waliwaita maofisa wa TANESCO na kuwaagiza kuwasha mitambo ya Dowans. Gazeti hili limeshindwa kuwapata Malima na Jairo.

Mtoa taarifa anasema, “TANESCO walikataa kutekeleza agizo hilo kwa kuhofia kuongeza mgogoro na kuingiza nchi katika matatizo zaidi.”

Anasema, “Wale wajumbe wa menejimenti ya TANESCO walimueleza wazi Malima na Jairo, kwamba kama mnataka tuwashe mitambo, ni lazima tuonyeshwe kibali cha baraza la mawaziri. Vinginevyo, katu hatuwezi kujiingiza katika mgogoro huu.”

Mtoa taarifa anasema, “hoja ya kutakiwa kibali cha baraza la mawaziri iliibuka baada ya taarifa kuvuja kuwa rais Kikwete amechoshwa na Dowans.”

Alipokuwa na mazungumzo na uongozi wa wizara ya nishati na madini aliyoitembelea katikati ya wiki iliyopita, rais Kikwete alimwagiza Ngeleja kuachia TANESCO kushughulikia utatuzi wa tatizo la umeme ili kuepuka kurudia alichoita “balaa jingine la Richmond.”

Alisema balaa hilo lilisababishwa na kitendo cha wizara hiyo kuingilia hatua za kutafutwa ufumbuzi wa tatizo la uhaba wa umeme lililoikumba nchi mwaka 2006.

“Unajua rais Kikwete alipokuwa nje ya nchi na waziri wa nishati na madini alisikika akisema, ‘haya mambo ya Dowans yamenichosha. Miaka minne yote ni Dowans, Dowans kila kukicha. Sitaki kusikia, labda kama watakuja kwa kupitia kampuni nyingine.”

Mtoa habari huyo alisema, “Ni katika mazungumzo hayo, ndipo wanaojiita wamiliki wa Dowans nchini, wakapata mwanya na kuanza kuwatumia baadhi ya maofisa wa CTI kufanikisha dili.”

Taarifa ilizonazo MwanaHALISI zinasema kuwa mapendekezo ya Dowans yaliwasilishwa mbele ya Bodi katika ajenda iliyoitwa Taarifa kuhusu kesi zinazohusu Dowans na Hali ya Sasa.

Uongozi wa TANESCO ulieleza kikao kuwa walikuwa na kikao na Bodi ya Wakurugenzi na CTI tarehe 4 Machi 2011 cha kujadili hali mbaya ya umeme na ufumbuzi wake. TANESCO na CTI waliwasilisha kila upande maelezo yake na kikao kikaafiki kukutana tena siku nyingine huku CTI wakitakiwa kuhudhuria.

Taarifa zinaonyesha kuwa Bodi ya TANESCO iliarifiwa ilifahamishwa kwamba TANESCO ilipokea mapendekezo ya Dowans tarehe 9 Machi yaliyoomba kufanyike makubaliano ya “pande tatu” pamoja na CTI yanayohusu uzalishaji wa umeme kiasi cha megawati 100.

Mwanachama mmoja wa CTI mwenye utitiri wa viwanda nchini, amekuja juu aliposikia taarifa hizo na ametoa msimamo tofauti. Anasema hayuko tayari kuona CTI inaingizwa katika ubia wenye mashaka.

“Nitapinga mpango huo mpaka mwisho wa nguvu zangu hadi watakapoamini kuwa hicho wanachokipanga kitatuangamiza sisi na taifa letu,” alisema mjumbe huyo aliyetoa maoni yake kwa sharti la kutotajwa gazetini.

Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Peter Ngumbullu, alipoulizwa kama bodi imeridhia mapendekezo ya TANESCO ya ushirikiano na Dowans na CTI, alisema bodi haijaridhia jambo hilo.

Ngumbullu alikiri kwa njia ya simu juzi Jumatatu, kuwa suala hilo limefikishwa kwenye bodi lakini “halijafika mwisho wake.”

“Nadhani baada ya siku mbili tatu hivi tunaweza tukawa tumefikia hatua nzuri ya kukubaliana. Kwa hiyo ukinipigia baada ya siku mbili au tatu nitakuwa na maneno kamili ya kusema. Hayo ndiyo ninayoweza kusema leo (juzi),” alihitimisha maelezo yake.

TANESCO imekuwa ikihangaika kutafuta ufumbuzi wa tatizo la umeme huku likiomba serikali kutoa fedha ili liweze kutekeleza miradi yake ya maendeleo lakini halijafanikiwa.

Katika hatua nyingine, TANESCO inaendelea kupambana mahakamani na Dowans ikiwemo kuitaka mahakama itengue zawadi ya Dola 64.2 za Marekani ilizopewa Dowans.

Mvutano wa Dowans na TANESCO umezaa kesi ndani ya kesi zikiwemo zilizofunguliwa na Kituo cha Huduma za Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali na kesi nyingine mwananchi Timothy Alvin Kahoho wa Dar es Salaam dhidi ya Dowans SA na wenzake.

Lakini zipo taarifa mpya zisemazo kwamba Dowans imeshauza mitambo yake iliyopo nchini kwa kampuni moja ya nchini Cyprus.


Source: MwanaHalisi.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom