Elections 2010 Redet, Synovate watetea tafiti zao

Kaa la Moto

JF-Expert Member
Apr 24, 2008
7,903
1,053
Redet, Synovate watetea tafiti zao Tuesday, 12 October 2010 19:41 Fidelis Butahe

BAADA ya watu wa kada mbalimbali kuponda tafiti zilizofanywa na Synovate na Redet, watendaji wa taasisi hizo wametetea matokeo ya tafiti zao na kuwataka wenye shaka nayo wafike ofisini kwa ajili ya kupata ufafanuzi. Taasisi za Redet na Synovate zilizotoa matokeo ya tafiti zake yanayoonyesha kutofautiana juu ya kiwango ambacho mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete anaongoza dhidi ya wapinzani wake kwenye kinyang'anyiro hicho ambao ni Dk Willibrod Slaa wa Chadema na Ibrahim Lipumba wa CUF.

Wakati Synovate ilionyesha kuwa Kikwete anaongoza kwa asilimia 71.2 ya kura za maoni, Redet ilionyesha kuwa mgombea huyo wa CCM anaongoza kwa asilimia 61 ya kura za maoni. Synovate pia walionyesha kuwa Dk Slaa anafuatia kwa asilimia 12.3 na Prof Lipumba asilimia 10.3, lakini Redet walionyesha Dk Slaa 16 na mgombea huyo wa CUF asilimia 5.

Wasomi waliyaelezea matokeo hayo kuwa ni ya kupikwa na yaliyolenga kukibeba chama kimoja cha siasa, lakini taasisi hizo jana zilikuwa na ufafanuzi dhidi ya makombora hayo.

Watendaji wa Redet na Synovate walisema wanaamini tafiti zao na kwamba wanamkaribisha yeyote mwenye shaka nazo kwenda kwenye ofisi zao ili waonyeshwe njia zilizotumika kupata matokeo hayo.

Mwenyekiti mwenza wa Redet, Dk Benson Bana aliiambia Mwananchi jana akisema: “Utafiti huu ni wa 17... hatubahatishi na hatujawahi kupata malalamiko yoyote. Unajua watu wana matarajio na ushindi wa vyama vyao, sasa wakiona katika utafiti vyama vyao vina asilimia ndogo, lazima watazungumza tu.”

Aliongeza kusema: “Unajua ukiwa unatoa matokeo ya utafiti, kila mtu anatarajia kuwa chama anachokipenda au kukishabikia kitapata ushindi sasa inapokuwa kinyume chake lazima yatatokea maneno tu.”

Alisema kuwa kama kuna mtu yeyote mwenye wasiwasi na matokeo yaliyotolewa na taasisi hiyo, anaruhusiwa kufika ofisi zao ili apatiwe njia zilizotumika kufanyia utafiti huo.

“Atapewa ushirikiano," alisema Dk Bana. "Mwaka 2006 kuna waziri mmoja alikuja kwenye ofisi zetu kujua ukweli wa utafiti tuliokuwa tumeufanya, tulimpa kila kitu tulichokitumia kufanyia utafiti wetu, aliridhika kabisa na hakuwa na maswali tena. Matokeo ya utafiti yanategemea na kipindi ambacho utafiti huo ulifanyika,” alisema Dk Bana.

Dk Bana alisema kuwa njia zote zinazotumika kufanyia utafiti huwa zina mapungufu na mazuri yake na kuongeza kuwa maswali wanayoyatumia kuwauliza wananchi katika tafiti zao ni yale yale.
“Maswali tunayoyatumia ni yale yale yapo valid, ni sahihi; yamehakikiwa na yanatoa majibu sahihi,” alisisitiza Dk Bana.

Akitolea mfano utafiti wa Redet wa mwaka 2005, Dk Bana alisema kuwa matokeo yalionyesha kuwa Kikwete angeibuka na ushindi wa asilimia 78, lakini baada ya uchaguzi mkuu Kikwete alipata ushindi zaidi ya kiwango hicho.

“Mimi ni mtoa taarifa tu ila hapa Redet tuna wataalam wetu ambao wamethibitishwa na wanaweza kufanya kazi za kitafiti nchi yeyote duniani. Kwa hiyo mtu yeyote akija ofisini kwetu, tutamuelekeza aonane na hawa wataalam wamueleza utafiti ulifanyikaje,” alisema Dk Bana,
“ Matokeo ya utafiti hukanushwa na utafiti mwingine na habari za uchunguzi zinakanushwa kwa uchunguzi.”

Dk Bana alisema kuwa tangu walipotoa matokeo ya utafiti huo amekuwa akipata ujumbe mfupi wa maneno (sms) wa vitisho pamoja na kutupiwa lawama katika mitandao mbalimbali.

Mkuu wa taasisi ya Synovate, Aggrey Oriwo jana hakutaka kuzungumza mambo mengi kuhusu tuhuma hizo lakini alieleza kuwa yupo tayari kutoa ushirikiano kwa mtu yayote atakayehitaji kujua jinsi utafiti huo ulivyofanyika.

“Umenieleza kuwa maprofesa na wanataaluma wamezungumza kuhusu tafiti yetu... mimi siwezi kujibu hilo kutoka kwa watu hao ila nakueleza kwamba mwananchi yeyote akihitaji kujua jinsi tulivyofanya utafiti anitafute tu nitamueleza,” alisema Owiro,

Aliongeza kusema: “Mimi siwezi kuingia katika malumbano. Hayo ni maoni yao lakini kama kuna mtu wa kuniuliza swali aniulize tu nitampatia jibu.”

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) jana kilitoa taarifa ya kuponda matokeo ya tafiti ya Redet na Synovate kuwa yamejaa ufisadi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa na mkurugenzi wa Tamwa, Ananilea Nkya kupingwa kwa matokeo ya tafiti kunadhihirisha kuwa Watanzania wako macho kubaini njama za mafisadi kutaka kupora wananchi mamlaka ya kuwaweka madarakani viongozi waadilifu, wachapa kazi na wanaowajibika kwa wananchi.

“Wananchi kupinga matokeo ya tafiti za Synovate na Redet kunapaswa kuwa changamoto kwa baadhi ya wasomi ambao kwa kujua au kutokujua kuwa wakishirikiana na baadhi ya viongozi mafisadi na wala rushwa kujitajirisha huku wananchi wakibaki mafukara,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Ilieleza kuwa hivi sasa Watanzania wanatambua umuhimu wa nchi kupata viongozi waadilifu na wenye upeo ili waweze kuondokana na umasikini na kwamba wananchi wanapaswa kuchagua viongozi wao kupitia sanduku la kura.

“Kikundi au taasisi yoyote kutoa picha ambayo hailingani na matakwa ya wananchi itapingwa na wananchi wenyewe,” ilieleza taarifa hiyo.

Katika taarifa hiyo chama hicho kiliwapongeza wananchi kwa kuweka bayana nani wanayemtaka kuwa rais, mbunge au diwani wao katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

“Tunaamini kabisa kwamba kama tafiti hizo zingekuwa zimeonyesha hali halisi ilivyo kisiasa nchini, wananchi wa kada mbalimbali wasingeyapinga,” inaeleza taarifa hiyo.

Source:Gazeti la Mwananchi-http://www.mwananchi.co.tz
 
Back
Top Bottom