Rangi zile zile lakini CCM si ile ile!

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,007
Rangi zile zile lakini CCM si ile ile!

Lula wa Ndali-Mwananzela Machi 25, 2009

Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

NI kama binti uliyekuwa umempenda mlipokuwa shuleni au jeshini enzi hizo. Au ni kama kijana uliyekuwa umemfia na nusura ukimbie kwenu baada ya kukolewa na penzi lake. Ulimpenda naye ulijua anakupenda, mlikuwa mmeshibana na kila mtu mtaani au kokote mlikokuwa alijua kabisa kuwa ninyi wawili kweli mlipendana.

Hata hivyo kutokana na maisha na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wenu, mahusiano yenu hayakuweza kuendelea na kuachana kwenu kulikuwa kwa machozi na kupangusa makamasi! Mlijikuta mnatengana si kwa mapenzi yenu bali kwa nguvu zilizo juu yenu. Labda wazazi walihama, ajira mpya, au jambo fulani ambalo mlijua kabisa kuwa mngekuwa na uwezo msingetengana, lakini ukweli wa maisha uliwalazimisha kukubali hali halisi hiyo. Mkaachana mkiombeana baraka tele na kuahidiana mkikutana huko mbeleni lazima “mkumbushiane” (usiniulize kukumbushiana nini!).

Siku zikapita na miaka ikaenda. Siku moja ukiwa “huna hili wala lile” katika mitaa ya soko fulani unasikia mtu anakuita kwa jina lako! Unageuka na mara moja unaona ni sura ambayo kwa kweli siyo ngeni. Ni “kama unamfahamu” hivi. Unamuangalia kwa karibu unapigwa na butwaa!

“Lula ni wewe!?” anakuuliza. Sauti pia unaifahamu, macho yake ni yale yale. Lakini dada wa watu dhaifu, kakonda, kapigwa na jua, kachoka, mgongoni ana mtoto, pembeni yupo mwingine analia kuchoka, tena ni mjamzito pia! Unashangaa “ni yeye huyu?”

“Mbona unaniangalia kama umenisahau?” anakuuliza kama kwa kejeli lakini unajua anamaanisha. Siyo kwamba umemsahau, siyo kwamba humkumbuki kabisa, bali ukweli ni kuwa huyu aliyeko mbele yako siye! Siye yule mliyependana mkashibana, siye yule ambaye mliachana kwa machozi na ahadi ya “kukumbushiana”. Kwa kweli hamu yote ya “kukumbushiana” inapeperuka utadhani tiara iliyokatika uzi au kama puto lililotobolewa. Kumbukumbu yako inabakia vipande vipande!

Mnapoachana hapo baada ya kusalimiana unabakia na mawazo. Unajiuliza nini kimemsibu. Hujui ilikuwaje “akaishia” kuwa hapo alipo. Upande mmoja unatamani ungeweza kumsaidia, lakini upande mwingine hata hujui uanzie wapi.

Unabakia kutikisa kichwa tu kwa masikitiko. Unakubaliana akilini kuwa binti yule uliyemfahamu enzi za shule siye huyu uliyekutana naye hivi leo. Unabakia na maswali. Hata hivyo una uhakika wa asilimia mia moja, kuwa kuna kitu Fulani, kwa hakika, kilikwenda kombo.

Ndugu zangu, vivyo hivyo CCM. Leo hii tunasikia “Chama cha Mapinduzi kimefanya hivi au vile”, utasikia “Mwenyekiti wa CCM amesema kuwa…” au “Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi amewaambia wapinzani kwamba…” Ukisikiliza maneno hayo unaweza kuamini (japo kwa makosa) kuwa wanapozungumzia CCM wanazungumzia chama “kile”.

Utawaona wakiitisha maandamano mamia ya wana “CCM” waliovaa sare zao za kijani na nyeusi, wakipepea bendera zao zenye jembe na nyundo, huku wakiimba kwa mdundo wa kwaya ya TOT kuwa CCM ni nambari wani unaweza kuamini kabisa kuwa chama hicho ndiyo kile kile; sicho.


CCM ile ilikuwa inaongozwa na itikadi za Ujamaa na Kujitegemea. CCM ya leo inaongozwa na itikadi ya tamaa na kujimegea! Mwanzilishi wa Chama cha Mapinduzi ambaye CCM haweshi kubandika kauli zake kwenye kumbi zao na kupamba ofisi zao kwa picha zake alisema hivi kuhusu Ujamaa; “Mtu binafsi, au hata taifa, utalitambua kama ni taifa la Ujamaa au si la Ujamaa kwa tabia yake, Ujamaa hauhusiani hata kidogo na mtu kuwa na mali au kutokuwa na mali. Maskini wanaweza kuwa na roho za kibepari – wanyonyaji wa binadamu wenzao. Vile vile, tajiri anaweza akawa na roho ya ujamaa; anaweza akathamini mali yake kwa sababu tu inaweza kutumiwa kuwasaidia binadamu wenzake. (Ujamaa, 1962, kuchapishwa 1971)

Leo hii hatuna shaka juu ya hilo. Waliokuwa maskini enzi zile leo wamegeuka makuhani wa ubepari, na wale ambao tuliwadhania mabepari ndiyo wanajionyesha kuwa na roho ya Ujamaa.

CCM iliuelewa Ujamaa vizuri na kuuweka katika katiba yao na sera zao. Lakini walipopata nafasi ya kuwanyonya wengine, hawakuchelewa kuchomeka mirija yao yenye ncha kama za miiba katika migongo ya Watanzania na kufyonza. Wamefyonza mpaka wanashindana wenyewe wakigombea mahali pa kufyonza!

Ndiyo, ilikuwa inaongozwa na sera za kujitegemea. Angalia CCM hii inavyotegemea fedha kama msingi wa maendeleo. Muasisi wake na Baba wa Taifa letu aliwaambia mapema kuwa fedha siyo msingi wa maendeleo. Wao wameacha hayo. Leo hii Tanzania, chini ya CCM, inapokea mabilioni ya shilingi kila mwaka ambayo ukigawa kwa kila siku au saa utashangaa kiasi kinachoingizwa Tanzania.

TANU (anayedaiwa kuwa ni mzazi wa CCM ya leo) ilisema hivi kuhusu hili katika Tangazo la Azimio la Arusha: “Ni jambo la kijinga kuchagua fedha kuwa ndiyo chombo chetu kikubwa cha maendeleo na hali tunajua kuwa nchi yetu ni maskini. Ni ujinga vile vile, kwa kweli ni ujinga zaidi, tukidhani kuwa tunaweza kuondoa hali hii ya unyonge wetu kwa kutegemea fedha za kutoka nje badala ya fedha zetu wenyewe.”

Tena wao wenyewe enzi hizo walitahadharisha kuhusu kutegemea mikopo ya kigeni kuwa msingi wa maendeleo: “Kujitawala kwa kweli hakuwezekani ikiwa Taifa moja linategemea misaada na mikopo ya Taifa jingine kwa maendeleo yake. Hata kama pangetokea Taifa au mataifa ambayo yako tayari kutupa fedha zote tunazohitaji kuendesha mipango yetu ya maendeleo isingekuwa sawa kwa nchi yetu kuipokea misaada hiyo bila kujiuliza matokeo yake yatakuwa nini kwa Uhuru wetu na uzima wetu.”

CCM ya leo siyo tu imeutupa Ujamaa bali pia imebeza kujitegemea. CCM hii siyo ile!

CCM ile tunayoikumbuka ilikuwa ni chama cha wakulima na wafanyakazi kweli. Leo hii chama hicho ambacho tunakiona leo hii kimebakia na sera hizo kwenye vitabu, lakini katika hali halisi haina rekodi ya kumuinua mfanyakazi wa Tanzania au mkulima wa Tanzania. Matokeo yake hata ni kuwa wakulima wamebakia pembezoni mwa uchumi wetu huku wakigereshwa kwa ahadi motomoto na mambo mawili matatu ya ishara.

Hakuna mpango kamambe wa kuondokana na jembe la mkono au hata la ng’ombe! Bado watawala wanafikiria kilimo kama moja wapo ya kazi za shurba na matokeo yake ni kuwa mkulima wa Tanzania bado anahenyeka pasipo sababu ya msingi. Mfanyakazi wa Tanzania naye vivyo hivyo. Bila “madili na mitkasi” ya hapa na pale maisha yake hayaendi.

Usishangae kuwa hata wale wanaosikitishwa na ufisadi mkubwa wa BoT au na ufisadi mwingine ndiyo wale wale wanafanya ufisadi wao “mdogo mdogo” huko chini ili maisha yao yaende. Wafanyakazi wa Tanzania imebidi watulizwe kwa viposho na vi-perdiem vingi ili kuyafanya maisha yao yaende.

Siku akitokea kichaa Tanzania na kuamua kuminya hii mianya ya ulaji, na kutaka mfanyakazi wa Tanzania aishi kwa kipato chake cha mwanzo hapo ndipo tutaona kuwa embe kweli ni tunda na nyanya ni kiungio cha mboga!

Ni kwa sababu hiyo basi CCM ya leo imebakia kuwatuliza wafanyakazi kwa kuwamwagia mapesa na kufungulia hazina ya pesa ili watulie tu. Si kwa sababu ya kuzalisha au kufanya mambo fulani yawe bora bali kwa sababu wafanyakazi watawasumbua.

Jinsi wanavyowatendea wafanyakazi wetu ni kama mtu anayetaka kupora lakini getini kuna mbwa mkali. Matokeo yake ili aweze kupora inabidi aje na mfuko wa nyama ambao anamrushia mbwa yule na kuyakata makali yake. Leo, viongozi wa vyama vya wafanyakazi hawana makali ya kina Bruno Mpangala au hata kina Mama Sitta enzi zao! CCM hii siyo ile!

CCM ile iliweza kujichunguza mambo yalipokuwa hayaendi sawasawa. Mwaka 1969 Mwalimu aliandika “Kupanga ni Kuchagua” na Mwaka 1971 Mwalimu aliandika “Miaka 10 Baada ya Uhuru”. Vile vile mwaka huo 1971 TANU ilikuja na kile tunachokikumbuka kama “Mwongozo wa TANU”. Vyote hivyo vitatu kwa kiasi kikubwa vilikuwa ni majaribio ya ndani ya TANU kujichunguza na kujikosoa.

Utaratibu huo ulirudiwa tena kwenye Mwongozo wa CCM wa 1981. Sura yake moja ilipewa jina hili “uchambuzi wa kujikosoa kama chama”. Na ukisoma mwongozo huo wa CCM utaona ni jinsi gani walienda ndani na kuangalia ni kwa kiasi gani matatizo ya Tanzania ya wakati ule yangeweza kuelezeka.

Kinachonifurahisha mimi ninapoikumbuka CCM ile ni kuwa hawakuhofu kukubali makosa yao kama chama na kuanza mpango wa kujisafisha.

Mwongozo ulitoa sababu kubwa tatu za matatizo ya kiuchumi ya wakati ule (zile mbili nyingine uzitafute). Ninaipenda ile ya tatu kwani inasema hivi: “Jambo la tatu lililodhihirika vile vile ni kwamba sisi wenyewe kama taifa hatukutumia kwa kiasi cha kutosha nguvu za Chama, Serikali na za wananchi katika kutatua matatizo ya uchumi ambayo ufumbuzi wake tuna uwezo nao.”

Kwa maneno mengine, TANU ya wakati ule ilikubali kuwa tatizo jingine halikuwa nje ya uwezo wetu kwani lilikuwa ni “sisi wenyewe”.

Mwongozo huo uliwashitaki viongozi wake bila kuwaonea haya. Kwa maneno ya kumiliki makosa yao mwongozo ulisema “Karibu viongozi wote tulishughulika na mikutano ya hadhara, mikutano ya wananchi kwa jumla bila ya kujali kukutana na wanachama. Viongozi wengine wa Chama tulilemazwa na umangi meza na wengine hata kufikiri wangeimarisha utekelezaji wa shughuli za Chama kwa njia ya vyombo vya habari tu.”

Laiti wana CCM wa leo wangerudi na kujifunza juu ya chama “kile”. Leo hii nashangazwa na kina Makamba na Chiligati ambao bila haya wala soni wanataka wananchi waamini kuwa CCM ni safi! Kwamba ndani yake hakuna makosa. Kwamba viongozi hawana makosa. Kwamba ufisadi ni “ni mtu mwenyewe na chama hakikumtuma”. Laiti na wao leo wangemiliki makosa yao kama chama labda wangeanza kweli kupambana na ufisadi.

Inashangaza leo kina Makamba wanaona fahari kwa CCM kutokuta kauli ya kulaani yaliyotokea Benki Kuu. Inashangaza leo wana CCM ambao Mwongozo uliwaita maaskari wa kujenga Ujamaa wanashindwa kuandamana na kupinga kilichotokea Deep Green, Mwananchi Gold, Kagoda nk. Bado ati wanajiita wao ni chama cha Mwalimu! Watambe?

Ndugu zangu, pasipo shaka, wala utata, wala kujiumauma meno; CCM mnayoiona leo hii siyo ile. Haiwezekani kuwa ndiyo chama cha Mwalimu hiki. Haiwezekani kuwa hiki ndicho chama kilichotangaza Ujamaa na Kujitegemea. Haiwezekani kuwa chama hiki leo kinashindwa kusimamia nidhamu ya wanachama wake na badala yake viongozi wake wanalalamika pembeni tu!

CCM hii siyo ile. Kitu pekee kinachofanana na kile cha chama kile ni magwanda tu! Kweli ni hizo sare za kijani, njano na nyeusi ndivyo vinafanana. Na kama yule niliyekusimulia hapo juu au hata wewe mwenyewe rafiki yako unayemkumbuka lakini sasa mwenye “hali mbaya” utaona kuwa CCM imebakia na magwanda tu!


Sera zake si za kijamaa, itikadi zake si za kibepari, mawazo yake si ya kimapinduzi, na mwelekeo wake si wa ujenzi wa taifa huru tena. Wameziacha fikra za Mwalimu, na itikadi za wazazi wao na sasa wanatuburuza tu. Wamefikia mahali wanatafunana wenyewe bila haya mbele ya umma, na bila woga wanasimangana.

Nyerere hakusita kuchukua hatua dhidi ya muasisi mwenzake (Jumbe). Hakusita kuchukua hatua dhidi ya mmoja wa vijana wake (Seif). Chama kile kilikuwa na Mwenyekiti mwenye nguvu, mwenye ushawishi, na mwenye ujasiri wa kusimama na kupambana na ufisadi ndani ya chama chake. Laiti leo CCM ingekuwa na mtu huyo. Bahati mbaya hawana. Viongozi wake wa juu kabisa wa sasa wanaingia madarakani kwa ufisadi, wanapambwa kwa mataji ya kifisadi. Leo hii Taifa linavuna mbegu za ufisadi kwa sababu Rais aliyetangulia aliukumbatia ufisadi.

Matokeo yake ndani ya CCM wale wachache ambao wanaonekana wanapambana na ufisadi ndiyo wanatajwa kuwa maadui, na wale maadui wa Ujamaa na Kujitegemea wanatukuzwa kama marafiki na wafadhili wa chama!

Kweli, CCM hii mnayoiona siyo ile! Mnabisha?
 
Nyerere ndie alieasisi udikteta na kupandikiza mizizi ya "ukubwa" katika CCM siku hizo alikuwa yeye na "wanafunzi" wake wachache tu ambao miongoni mwao aliwapigia debe wakawa wakuu wa nchi (Mkapa), siku hizo hakuna aliyesema kwa kuwa "darasa" la mwalimu Nyerere lilikuwa kama uhusiano kati ya msomaji, taarifa ya habari na mtazamaji kati t.v, na wanafunzi wa Nyerere ambao hakuna kuuliza maswali. Matokeo yake waliofuatia waliendeleza mafunzo hayo ya Mwalimu, kwa kufanya mambo kimyakimya hakuna aliewahoji, "ukubwa" waliorithishwa na Mwalimu, na namna ya kuwashughulikia watakao hoji namna ukubwa huo unavyopeleka mambo ya nchi,umeleta athari kubwa na matokeo yake leo ndo haya, wakati ule walijitokeza mashujaa kama Jumbe, Seif Shariff,Ramadhanb Haji, Bibi Titi Mohd, Kasanga Tumbo, Kasela Bantu,n.k waliodiriki kumwambia Mwalimu Nyerere uso na macho kuwa huku tunakokwenda siko na hilo ni wazi kwa kua Mwalimu alifanya makosa na yeye hakuwa malaika au mwana wa Mungu kuwa hakukose, alichokifanya badala ya kuzingatia wakosoaji wake aliwafanya maadui na kuwatoa mhanga.Hakujua kuwa wanafunzi watakao mfuata watafanya yaleyale lakini si kwa watakao wahoji tu wanatakavyopeleka mambo bali hata kutumia "ukubwa" wao kuchezea kila senti halali ya watanzania na kuitia katika mikono yao haramu, hivyo wanafunzi wameli expand somo la mwalimu kutoka kuchezea watu na kwend ktika kuchezea mali ya umma.
 
Nilivyomsikiliza mzee Malecela nimeamini kuwa kweli CCM hii siyo ile. Alivyokuwa anazungumza alikuwa anazungumza kama CCM ile kumbe siyo. Nina wasiwasi wanaweza kuwa wamemuacha kwenye mataa yeye!
 
Nilivyomsikiliza mzee Malecela nimeamini kuwa kweli CCM hii siyo ile. Alivyokuwa anazungumza alikuwa anazungumza kama CCM ile kumbe siyo. Nina wasiwasi wanaweza kuwa wamemuacha kwenye mataa yeye!

Mkjj, anaelewa sana kinachoendelea bali anataka kuendelea kutuzuga tu kwamba CCM ile iliyokuwa chama cha wafanyakazi na wakulima wanyonge ndiyo CCM hii ya leo, lakini ukweli umeshajulikana kwamba CCM hii ya leo ni chama cha mafisadi hakuna siri juu ya hilo.
 
Nyerere ndie alieasisi udikteta na kupandikiza mizizi ya "ukubwa" katika CCM siku hizo alikuwa yeye na "wanafunzi" wake wachache tu ambao miongoni mwao aliwapigia debe wakawa wakuu wa nchi (Mkapa), siku hizo hakuna aliyesema kwa kuwa "darasa" la mwalimu Nyerere lilikuwa kama uhusiano kati ya msomaji, taarifa ya habari na mtazamaji kati t.v, na wanafunzi wa Nyerere ambao hakuna kuuliza maswali. Matokeo yake waliofuatia waliendeleza mafunzo hayo ya Mwalimu, kwa kufanya mambo kimyakimya hakuna aliewahoji, "ukubwa" waliorithishwa na Mwalimu, na namna ya kuwashughulikia watakao hoji namna ukubwa huo unavyopeleka mambo ya nchi,umeleta athari kubwa na matokeo yake leo ndo haya, wakati ule walijitokeza mashujaa kama Jumbe, Seif Shariff,Ramadhanb Haji, Bibi Titi Mohd, Kasanga Tumbo, Kasela Bantu,n.k waliodiriki kumwambia Mwalimu Nyerere uso na macho kuwa huku tunakokwenda siko na hilo ni wazi kwa kua Mwalimu alifanya makosa na yeye hakuwa malaika au mwana wa Mungu kuwa hakukose, alichokifanya badala ya kuzingatia wakosoaji wake aliwafanya maadui na kuwatoa mhanga.Hakujua kuwa wanafunzi watakao mfuata watafanya yaleyale lakini si kwa watakao wahoji tu wanatakavyopeleka mambo bali hata kutumia "ukubwa" wao kuchezea kila senti halali ya watanzania na kuitia katika mikono yao haramu, hivyo wanafunzi wameli expand somo la mwalimu kutoka kuchezea watu na kwend ktika kuchezea mali ya umma.
bila Nyerere kuifanya CCM hii ya leo nchi ingetawaliwa na upinzani wa kipuuzi sana kama tunavyouona sasa. CCM iliyoasisiwa na nyerere ndani ya rais Magufuli. Ndoto ya Magufuli ni kuwa na CCM imara ya kuisimamia serikali ipasavyo na ndilo lengo ya CCM ya Nyerere na si udikteta kama unavyojaribu kuaminisha watu
 
bila Nyerere kuifanya CCM hii ya leo nchi ingetawaliwa na upinzani wa kipuuzi sana kama tunavyouona sasa. CCM iliyoasisiwa na nyerere ndani ya rais Magufuli. Ndoto ya Magufuli ni kuwa na CCM imara ya kuisimamia serikali ipasavyo na ndilo lengo ya CCM ya Nyerere na si udikteta kama unavyojaribu kuaminisha watu
Duh... Kweli wewe ni "member", karibu sana JF.. Huu uzi ni wa miaka 9 iliyopita.. Eti, Unasema CCM inasimamia serikali? Ha ha ha haaa, CCM si Magufuli? Na serikali si Magufuli?


Mkuu BAK popote ulipo tumekukumbuka sana.
 
Duh... Kweli wewe ni "member", karibu sana JF.. Huu uzi ni wa miaka 9 iliyopita.. Eti, Unasema CCM inasimamia serikali? Ha ha ha haaa, CCM si Magufuli? Na serikali si Magufuli?


Mkuu BAK popote ulipo tumekukumbuka sana.
Nenda KT utamkuta huko.
 
Back
Top Bottom