Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,268
- 33,040
Nakumbuka siku Mheshimiwa Sigalla anakuja ofisini kwangu ndio siku ambayo magazeti karibu yote nchini yalikuwa yameandika juu ya hali ya Rais wetu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, kuwa mbaya akiwa Jukwaani huko Mwanza alikokuwa amealikwa kwenye sherehe za Kanisa la African Inland Church kutimiza miaka mia moja.
Asubuhi hiyo nikiwa na Mkuu wa Wilaya ofisini kwangu, miongoni mwa maswali niliyomuuliza Mheshimiwa Norman wakati wa mazungumzo yetu lilikuwa ni la anaionaje hali ya nchi yetu tulipotoka, tulipo na tunakokwenda! Hili ndilo swali ambalo mara nyingi napenda kuwauliza watu wanaofikiria sana kuhusu nchi.
"Kama kila mmoja wetu atatimiza wajibu wake, badala ya kumwachia Rais wetu kila kitu, basi nchi yetu itaendelea na tutafanya mambo ambayo watu watakoishi baada ya sisi watasema ni bora sisi tuliishi kabla yao…" hilo ndilo lilikuwa jibu la Norman.
Kauli hii ya Norman ndio ilikuwa chachu ya mimi kuandika makala haya unayosoma leo, nakubaliana na Mwanasiasa huyu kijana kwa asilimia mia moja kwamba kama sote tutatimiza wajibu wetu, hakika hatutahukumiwa na vizazi vitakvyokuja baada yetu na hapo ndipo hasa tatizo kubwa lililopolala, hiki ndicho kiini cha matatizo yote tuliyonayo kama nchi; watu kutotaka kutimiza wajibu wao na kutafuta watu wa kulaumu katika kila jambo.
Nchi yetu ni kubwa, lakini imegawanywa katika mikoa, wilaya, tarafa, kata na hatimaye mashina! Juu ya mgawanyiko wote huo kuna mtu mmoja mkubwa kuliko wote, huyu anaitwa Rais wa Jamhuri, huyu ndiye baba, huyu ndiye mtunzaji wa Watanzania wote milioni zaidi ya arobaini! Kwa sababu ni mtu mmoja aliyepewa mamlaka na watu wote milioni arobaini kuwaongoza, Rais hulazimika kuteua watu wa kumsaidia kuzifanya kazi zake zote, sababu hawezi kuwepo kila mahali na hatuwezi sote kumfuata Ikulu kumweleza shida zetu.
Huu si utamaduni mpya, umekuwepo duniani kwa miaka maelfu, hata enzi za Musa na safari yake ya Wana wa Israel kwenda Kanan, alilazimika kuteua wazee wa kumsaidia kazi! Uamuzi huu ulifikiwa baada ya Musa kuzidiwa na kazi, maana kila mtu alimfuata yeye, akahisi kuchanganyikiwa akili. Wazee aliowateua walimsaidia kusikiliza shida za watu na baadaye kumwakilishia yeye, huko ndiko mfumo wa serikali na wa Baraza la Mawaziri ulikozaliwa.
Kwa utaratibu huu, Rais wa Jamhuri ambaye ndiye baba wa watu wote milioni arobaini kulazimika kuteua watu wa kumwakilisha, ambao hufanya kazi ambazo angetakiwa kuzifanya yeye kwenye eneo husika; hawa huitwa Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Majeshi, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya nk. wote hawa humwakilisha Rais kwenye maeneo waliyoteuliwa kuongoza.
Kama watu hawa walioteuliwa, wakimwakilisha Rais vizuri kwenye maeneo yao, Mawaziri wakajiepusha na tamaa za kujitajirisha, Majaji wakatoa haki sawa kwa wananchi, Wakuu wa Mikoa na wilaya nao wakafanya hivyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi akatimiza wajibu wake vizuri kwa kuteua Makamanda wa polisi wa Mkoa na Wilaya wenye sifa zinazostahili badala ya upendeleo au kutoa vyeo zawadi, nchi yetu itatulia amani itadumu na maendeleo yatakuja tena kwa kasi ya ajabu. Kiini cha maendeleo ya nchi yoyote duniani ni watu kutimiza wajibu wao, hakuna jingine.
Mfano, kama Wilaya moja tu katika nchi yetu ambako mkuu wa wilaya hiyo anafanya kazi kama Rais, Mkuu wa polisi wa wilaya (OCD) ambaye katika wilaya hiyo humwakilisha Mkuu wa jeshi la polisi nchini, itakuwa na matukio mengi ya ujambazi na mauaji kwa sababu tu viongozi hawa wawili watashindwa kutimiza wajibu wao vizuri, sifa ya nchi nzima ya Tanzania na Rais wa Jamhuri ya Muungano itachafuka! Hapa ni suala moja tu linalofanya kazi, Uwajibikaji (Accountability)
Tunaposikia mauaji ya Albino yamekithiri nchini Tanzania mpaka dunia nzima inatushangaa, hili si tatizo la Tanzania nzima, limetokea katika wilaya fulani tu, lakini sifa hiyo imechafua nchi yetu kila mahali tunakopita tunaulizwa "Wewe unatoka kwenye nchi wanakouza viungo vya albino?." Hii ni aibu, lakini imetokea kwenye wilaya moja ambako inawezekana kabisa Mkuu wa wilaya husika na Mkuu wa polisi wa wilaya yake hawakutimiza wajibu wao, mwisho wa siku Rais wa nchi anaonekana hafai.
Duniani hakuna mafanikio ya mtu mmoja, kila unapoona mafanikio sehemu fulani lazima ujue kuna timu iliyohusika kuyaleta mafanikio hayo! Kuna watu wapo nyuma ya Bill Gates, wengine wala hawatajwi, kuna watu wapo nyuma ya Barrack Obama lakini hakuna anayewaongelea, kila Rais huyu anapopata mafanikio sifa zote zinamwendea yeye! Kuna watu walikuwepo nyuma ya Rais Bush, waliomshauri vibaya mpaka akaondoka madarakani kwa aibu.
Nimeamua kuandika makala hii leo kuwakumbusha viongozi wa nchi yangu, kuanzia Ikulu mpaka kwenye Shina kwamba, kama kuna kosa kubwa kiongozi anaweza kufanya ni kutoa vyeo kama zawadi au shukrani kwa mema aliyofanyiwa! Kama kuna kosa Marais wa Afrika wanafanya ni hili na ndilo limezamisha Bara la Afrika katika matatizo.
Kama tunataka kufanikiwa, inabidi tubadilike mara moja na kuanza kuteua watu kutokana na sifa zao, wanaostahili kushikilia nyadhifa wanazopewa na kumwakilisha Rais vizuri kwenye maeneo yao! Tujiepushe na kutoa vyeo au mamlaka kama zawadi, ndio maana katika nchi za wenzetu wanaofanya vizuri, hata mtu akiteuliwa na Rais ni lazima apitishwe na Bunge ili kuthibitishwa kama kweli ana sifa za kushika wadhifa huo, wengi waliteuliwa lakini baadaye uteuzi wao ukabatilishwa na Bunge.
Ningetamani sana mfumo huu siku moja uingie katika nchi zetu za Kiafrika, itatuepusha kuwa na watu waliopewa vyeo kama zawadi, mwisho wa siku wakashindwa kutimiza wajibu wao kwenye maeneo waliyopelekwa kumwakilisha kiongozi wa nchi na kuharibu sifa au kuiingiza nchi kwenye matatizo! Hili si jambo jema, inabidi liepukwe mara moja.
Juzi tu Rais ameteua mwanasheria Mkuu mpya, Makatibu wakuu, wakuu wa wilaya na kuhamisha baadhi kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Naamini uamuzi huu ni kwa nia ya kuboresha utendaji, hajatoa vyeo zawadi na anafahamu anachokifanya ni vyema tukampa nafasi, lakini jambo moja anatakiwa kulifahamu ni kwamba mwisho wa siku wananchi watapima utendaji wake na kufanya maamuzi yao kwenye boksi la kupigia kura!
Walioteuliwa ni lazima watimize wajibu wao, lazima wamwakilishe kiongozi wa nchi vizuri kwenye maeneo yao ya kazi, uzembe kidogo ndio utamfanya Rais wetu afanye kazi nyingi kupita kiasi sababu anataka kufanikiwa, yeye ni miongoni mwa watu ambao akimtuma mtu kitu na mtu huyo badala ya kukimbia akatembea polepole, yeye huondoka akikimbia na kwenda kukichukua hicho kitu! Naamini hili ndilo limemfanya asipumzike, asipate usingizi wa kutosha, akiuke hata ushauri wa madaktari wake na kujikuta akijisikia vibaya jukwaani.
Yote haya ni kwa sababu ya watu wengi wanaomzunguka kushidwa kutimiza wajibu wao, jambo la hatari kabisa katika uongozi wa nchi, wengi wa wateuliwa huwa ni watu wa kuwaitikia viongozi "Ndio mzee" halafu kiongozi akiondoka hawafanyi lolote, mfumo wa funika kombe mwanaharamu apite, ndio hutumika zaidi katika serikali nyingi za Kiafrika.
Ninachosema mimi ni kwamba mpaka siku wateule wa Rais watakapotimiza wajibu wao ndipo maendeleo katika nchi yetu yatakuja, ni wateule wake ndio wanaomwangusha. Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
Chanzo: Global Publishers