Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,299
- 33,079
Rais Jakaya Kikwete.
Rais Jakaya Kikwete amesema kwamba idadi kubwa ya Watanzania wanapinga kufutwa kwa adhabu ya kifo na wanataka iendelee kuwapo katika vitabu vya sheria.
Hili ni jambo lililoulizwa na Kamati ya Jaji Nyalali. Watu walikataa kufutwa kwa adhabu ya kifo. Tanzania kwa muda mrefu haijapata kunyonga mtu hata kama Sheria ya Kunyonga imeendelea kuwapo katika vitabu vyetu, alisema na kuongeza:
Majuzi nilibatilisha kiasi cha hukumu 75 za vifo kuwa vifungo vya maisha. Lakini bado waliohukumiwa kifo kwenye magereza yetu ni wengi, pengine kufikia watu 200, hata kama sijahesabu.
Rais Kikwete alitoa msimamo huo Jumanne wiki hii, wakati wa chakula cha usiku katika makao makuu ya Jumuiya ya Kilei ya Kanisa Katoliki Duniani ya Mtakatifu Eggidio, jijini Rome, Italia.
Sheria ya adhabu ya kifo inapingwa na jumuiya ya kimataifa pamoja na Jumuiya ya Eggidio.
Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete pia alisema kuwa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini, siyo tu ni mauaji ya kusikitisha bali ni mauaji ya kijinga kabisa kutokea katika dunia ya leo ya sayansi na teknolojia.
Rais Kikwete alisema kuwa katika moja ya mambo yaliyoiabisha zaidi taifa la Tanzania katika muda mfupi ni mauaji na kijinga ya albino.
Kwamba watu wanaweza kuwa wajinga kuamini kuwa ukipata kidole cha albino utatajirika ni jambo gumu sana kuamini katika dunia ya leo ya sayansi na teknolojia.
Lakini napenda kuwahakikishieni kuwa sasa Serikali imeyadhibiti mauaji haya, alisema Rais Kikwete na kuongeza:
Tuliendesha kura ya maoni. Watu wengi wametiwa mbaroni na wengine wako mahakamani. Kati yao wengine wamehukumiwa kunyongwa.
Aidha, Rais Kikwete alirejea onyo lake kuwa vyombo vya habari kuwa haviwezi kutumia uhuru wake kwa madhumuni ya kuvuruga amani na kuvunja umoja wa kitaifa, na bado vikaachiwa kuwa huru kuendelea na shughuli zake bila kuchukuliwa hatua.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema kwa vyombo vya habari vyenyewe lazima vijirekebishe na kuwa na wajibu ambao ni sehemu muhimu ya uhuru huo wa habari
Kama nilivyowaambia pale Musoma majuzi wakati wa kuadhimisha miaka 10 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, huu hauwezi kuwa uhuru wa kuvunja taifa, uhuru wa kugawa watu, uhuru wa kuchochea maasi na magomvi kati ya dini mbalimbali, kati ya makabila, kati ya watu wenye rangi mbali mbali, alikumbusha.
Alisema kuwa: Baadhi ya vyombo vyetu havina wajibu kabisa. Vinachochea maasi ya kuvunja nchi na kuleta mfarakano kati ya watu wetu. Vinajaribu kugawa watu wetu, kugawa mataifa yetu na kusababisha maafa makubwa. Hatuwezi kuvumilia vyombo vya habari vya namna hiyo vinavyotumia uhuru kuleta balaa kwa watu.
Viongozi wa Mtakatifu Eggidio walimwambia Rais Kikwete kuwa wanaipenda Tanzania kwa sababu ni mfano wa jinsi watu wanavyoishi kwa amani duniani bila kusukumwa kuvunja nchi na sababu za kikabila, kidini ama hata rangi.
Rais Kikwete na viongozi hao wa Jumuiya ya Mtakatifu Eggidio pia walijadili migogoro inayoendelea katika Afrika. Jumuiya hiyo ilishiriki katika majadiliano ya kuleta amani katika nchi za Burundi na Msumbiji.
Ujumbe huo wa Mtakatifu Eggidio uliongozwa na mwanzilishi wa Jumuiya hiyo, Profesa wa Historia katika Chuo Kikuu cha Rome, Andrea Riccardi, na msaidizi wake wa kiroho, Padre Matteo Zuppi.
Ujumbe wa Tanzania kwenye mazungumzo hayo uliwajumuisha Waziri wa Kilimo na Usalama wa Chakula, Steven Wassira na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Seif Iddi.
Rais Kikwete ambaye alikuwa Italia kuhudhuria Mkutano wa wakuu wa nchi na serikali kujadili Usalama wa Chakula Duniani, alirejea nchini jana.
CHANZO: NIPASHE