Rais Kikwete lichambue upya Baraza lako la Mawaziri

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,007
Posted Date::4/21/2008

Rais Kikwete lichambue upya Baraza lako la Mawaziri
Mwananchi

HATIMAYE aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, ameachia ngazi baada ya vyombo vya habari kumwandama kila kukicha, kutokana na tuhuma za kumiliki Dola za Marekani 1 milioni (Sh1.2 bilioni), alizoficha kwenye akaunti yake iliyoko kwenye Kisiwa cha Jersey, nchini Uingereza.

Taarifa za kujiuzulu kwa Chenge zilitolewa jana, baada ya kuwasilisha barua yake ya kuachia ngazi kwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye alikubali ombi lake, akisema kuwa amefanya uamuzi wa maana.

Chenge ambaye Jumatano wiki iliyopita, alikaririwa akisema kuwa, hawezi kujiuzulu alipoulizwa na waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, kama atachukua hatua hiyo kufuatia tuhuma mbaya zinazomkabili, amelazimika kufanya hivyo si tu kwa shinikizo la vyombo vya habari, bali hata kelele za wananchi wa kada mbali mbali, ambao baadhi yao walifikia hatua ya kuandaa maandamano ya kupinga kuingia kwake bungeni.

Mbali na tuhuma hizo, kilichowaudhi watanzania ni kutokana na kauli yake aliyotoa mbele ya waandishi katika uwanja wa ndege alipowasili kutoka China, alikoambatana na Rais Kikwete kwamba, anakabiliwa na tuhuma ya 'vijisenti', akimaanisha kuwa fedha anazodaiwa kumiliki ni vijisenti!

Tunashukuru ameamua kujiuzulu, ili kupisha uchunguzi na kutoendelea kulipaka matope Baraza Jipya la Mawaziri ambalo Rais aliliunda Januari, mwaka huu, baada ya lililokuwapo kuvunjwa kufuatia aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa pamoja na mawaziri wengine wawili kujiuzulu, kutokana na kuhusishwa kwao kwenye kashfa mbaya ya Richmond.

Chenge ni waziri wa nne kujiuzulu kwa kashfa za ufisadi ambazo zilianza kushika kasi mwishoni mwa mwaka jana, baada ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa akishirikiana na baadhi ya viongozi wa upinzani kutaja majina hadharani ya vigogo serikalini aliodai kuwa ni mafisadi, likiwemo la Chenge.

Licha ya kufanya walichotaka, kujiuzulu kwake kunapokelewa kwa mitazamo mbali mbali, ukiwemo wa kwamba alichelewa kufanya hivyo, kwani alitakiwa kuchukua hatua hiyo pengine tangu alipopata taarifa ya kuanza kuchunguzwa na Taasisi ya Kuchunguza Makosa Makubwa ya Jinai (SFO) ya nchini Uingereza, ambayo ilikuwa imeshapata kibali na tunaamini kwamba alikuwa na taarifa hizo.

Tabia hii ya viongozi kutopenda kuwajibika wanapotuhumiwa kwa kashfa mbaya kama hizo, mpaka washinikizwe na kuchafuliwa au waandamwe na vyombo vya habari, huku wakijigamba kwamba hawawezi kujiuzulu mpaka rais aliyewateua achukue hatua, si ya kiungwana hata kidogo kwa viongozi wa umma.

Mtazamo mwingine ni ule wa rais kutoyafanyia kazi malalamiko ya wananchi juu ya watu anaowapa nyadhifa, kwamba hawafai kutokana na rekodi zao za nyuma, kunawapa kiburi wateule wake na kuipunguzia hadhi na heshima serikali yake.

Kwa mfano, kabla ya kuvunjwa kwa baraza la mawaziri kulikuwa na malamiko kwamba, ndani ya baraza lake kuna watu wasio waadilifu, ambao walitegemea wangeachwa, lakini haikuwa hivyo. Hata alipoteua baraza jipya, wananchi kutoka kona zote za nchi walilalamika kuwa, rais amekosea kuteua baadhi ya watu, ambapo waliwataja mawaziri wawili akiwamo Chenge, kwamba hawafai kuwemo kwa madai ya kuwa si waadilifu.

Hapana shaka kwamba, yanayojitokeza sasa yanampa fundisho Rais Kikwete kuwa, anatakiwa kuchukua hatua za haraka kuiangalia kwa upya safu ya mawaziri wake na kuchukua hatua ya kuwaondoa wasiofaa, kwa msaada wa vyombo vyake vya usalama kumpa taarifa na ushauri sahihi, juu ya watu anaotaka kuwapa vyeo na si kwa kuangalia sura au ukaribu.

Pia tunawaomba mawaziri na watendaji wote wa umma ambao wanajua kwamba, wana kashfa za ufisadi, wajiuzulu kabla mambo yao hayajawekwa hadharani.
 
Back
Top Bottom