Rais Kikwete atangaza vita kwa wanasiasa

Josh Michael

JF-Expert Member
Jun 12, 2009
2,523
77
ASEMA WATAKAONUNUA KURA, WATAKAOOMBA RUSHWA KUKIONA


Frederick Katulanda, Mwanza

RAIS Jakaya Kikwete amesema ataisaini kwa mbwembwe sheria ya matumizi ya fedha katika uchaguzi na kuwaonya watakaojihusisha na rushwa katika uchaguzi mkuu ujao kwamba, watakumbana na mkono wa dola.

Alisema tofauti na sheria zingine ambazo amekuwa akisaini kimyakimya, sheria hiyo ataisaini kwa namna ya pekee ili watu waijue na kuitambua.

"Sasa ole wao wahongaji, ole wao wahongwaji na ole wao wanaoomba kuhongwa. Nafarijika ahadi niliyoitoa Desemba 30, 2005 wakati wa kuzindua bunge letu hili imetimia.

Takukuru ndiyo mtakaotazamiwa kufanya kazi kukazia utekelezaji wa sheria hii mpya,"alisema Rais Kikwete alipokuwa akifungua mkutano wa mwaka wa Takukuru uliofanyika katika ukumbi wa chuo cha Benki Kuu jijini hapa.

Alisema kupitishwa kwa sheria hiyo mpya ni jambo la kihistoria na ni hatua ya kimapinduzi kwa kuwa itasaidia kudhibiti rushwa na kuzuia taifa lisifike mahali pabaya.

Alibainisha kwamba, hali inaonyesha kuwa mbaya zaidi sasa kutokana na rushwa katika uchaguzi kuanza kuwa tatizo kubwa, hususan katika mchakato wa kuchagua wagombea wa chama wakati wa kura za maoni.

Alisema sheria hiyo inaiweka serikali mahali pazuri katika kupambana na watu wanaotaka kupata uongozi kwa nguvu ya pesa na kwamba, inasaidia kuwabana watu wanaogeuza haki yao ya kupiga kura kuwa mradi au bidhaa ya kunufaika nayo kipesa kwa kuiuza.

Kikwete ambaye alikuwa akizungumza kwa furaha aliwaagiza makamanda wa Takukuru kuanza kujipanga kufanya kazi ya kudhibiti wanunua uongozi na kubainisha kuwa tayari kuna wagombea wameshaanza kupita mitaani wakigawa mipira na wengine kukarabati ofisi za CCM.

"Anzeni sasa kujipanga kuifanya kazi hiyo kwani naambiwa wanunuaji wa uongozi wameshaanza, wengine wanapita na kugawa mipira na wengine wanakarabati majengo ya ofisi za CCM.

Sheria inaruhusu kudhibiti rushwa kabla na wakati wa kura za maoni ndani ya vyama vya siasa na wakati wa uchaguzi, nawaomba muanze kufuatilia na kuchukua hatua zipasazo," aliongeza.

Akielezea kuhusu sakata la rushwa katika uchaguzi, Rais Kikwete alisema: "Rushwa kubwa kwenye uchaguzi ipo wakati wa kura za maoni katika vyama pengine hata kuliko wakati wa uchaguzi wenyewe na kuahidi kuwa yeye kama rais yuko tayari kufanya kila linalowezekana ili kuiwezesha Takukuru kufanikisha kazi ya kudhibiti vitendo hivyo na kuwataka waanze kazi hiyo sasa.

Aliasa kuwa rushwa katika uchaguzi imeanza kukomaa na iwapo hatua hazitachukuliwa, kuna hatari itageuza uongozi kuwa bidhaa ya kununuliwa kama shati, au njugu jambo ambalo alisema ni hatari kwa vile hata mwendawazimu akiwa na fedha anaweza kuununua.

Alisema furaha yake baada ya kupitishwa kwa sheria ya fedha za uchaguzi ni kuona wakati yeye na wenzake watakapomaliza muda wao wa uongozi, wawe wamejenga misingi imara ya utawala bora, demokrasia na maadili ya viongozi wa umma.

Alisema lengo ni kuhakikisha kuwa misingi hiyo inajikita katika sheria za nchi na baadaye kuwa utamaduni wa kudumu kuendesha shughuli za siasa nchini.

Aidha Kikwete aliwapongeza Takukuru kwa kufanikiwa kuokoa fedha za taifa kiasi cha Sh7,587,968,099 kupitia changuzi mbalimbali pamoja na ukaguzi wa fedha za miradi ya serikali na kuwataka kuanza kushughulikia rushwa katika sekta binafsi.

Alisema sekta binafsi inapaswa kuhusishwa kwani nao wamekuwa wahusika wakuu katika vitendo vya rushwa na kubainisha kuwepo kwa maofisa na watendaji katika kampuni binafsi wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya kutoa, kudai na kupokea rushwa.

Bunge lilipitisha sheria ya gharama za uchaguzi, Februari 11 ambayo hata hivyo ilizua mjadala mkali kabla ya kupitishwa huku wabunge wakitoa mapendekezo ya kurekebishwa kwa vifungu kadhaa na vingine kuvifanyia marekebisho huku kampeni za chinichini zikielezwa kuanza katika majimbo mbalimbali ya uchaguzi.

Awali wabunge waliupinga muswada wa sheria hiyo wakisema umechelewa kufikishwa hivyo usuburi hadi uchaguzi mkuu utakapoisha ili kufanya maandalizi ya kutosha. Hivyo kutaka iwasilishwe katika bunge lijalo ili ianze kutumika katika chaguzi za baada ya hapo.

Walidai kuwa muda uliosalia ni mfupi kwa sheria hiyo kupitishwa na kuanza kutumika kwa sababu inatakiwa kuelewaka vizuri kwa wadau wote. Walionya kuwa sheria hiyo itapitishwa, wabunge na baadhi ya watu watafungwa kwa kufanya makosa kutokana na kutoielewa vizuri.
Hata hivyo siku moja kabla ya mkutano wa 18 wa bunge haujafungwa, muswada huo ulipita baada ya majadiliano makali, hasa katika kipengele cha kuwakirimu wapambe wa mgombea na kufanya marekebisho kadhaa.
 
Na kama kweli kutakuwa na usawa katika uchaguzi na pia hata ruzuku zao zinaweza kuwa rushwa kama tulivyona katika kipindi kilichopita
 
Act iliyoianzisha PCCB ina yote yaliyo kwenye sheria hii mpya. Imetusaidia nini? Rushwa iko palepale!
 
Alituahidi maisha bora kwa kila Mtanzania kuwa yangekuja kwa ARI MPYA na KASI MPYA yako wapi? Hizo ni ahadi za uongo!! Wanamtandao wake ndio wahongaji wakubwa lakini hawatakamatwa aslani!. Ataipitisha kwa mwembwe kwasababu vitu alivyovitaka kwenye sheria hii ili vimsaidie kushinda urais havikuondolewa na hao wabunge wake kwahiyo muungwana uRAIS tambarale!!
 
Jamaa anasoma alama za nyakati na kuanza kurap kwa style ile ile kama kipindi kile cha wakati ule
 
Alituahidi maisha bora kwa kila Mtanzania kuwa yangekuja kwa ARI MPYA na KASI MPYA yako wapi? Hizo ni ahadi za uongo!! Wanamtandao wake ndio wahongaji wakubwa lakini hawatakamatwa aslani!. Ataipitisha kwa mwembwe kwasababu vitu alivyovitaka kwenye sheria hii ili vimsaidie kushinda urais havikuondolewa na hao wabunge wake kwahiyo muungwana uRAIS tambarale!!
Si ajabu mwaka huu akapita bila kupingwa. Wale wasindikizaji wa miaka yote akina Lipumba, Mrema na hata Mbowe inasemekana wanajiandaa kugombea Ubunge
 
Si ajabu mwaka huu akapita bila kupingwa. Wale wasindikizaji wa miaka yote akina Lipumba, Mrema na hata Mbowe inasemekana wanajiandaa kugombea Ubunge
Kuna hizo dalili maana wanaimba ngonjera hizo hizo na anaweza kupita bila ya kupigwa
 
Anajishaua tu.Kashindwa kuwawajibisha Mafisadi walioiba mabilioni ya shilingi amabo ni wachache tena ushahidi anao,ataweza wa uchaguzi,Tz ina majimbo takribani 232,ataweza?
 
Hii yote ni njaa tu yao na kuna sababu kama kweli wanataka kuwa na uchaguzi wa amani na uswa basi warekebishe sheria ya RUZUKU kwa vyama vya Siasa, Huwezi kuwa na chama Kinapata Bilioni moja na Chama cha DP ambacho hakina kabisa ruzuku then hapa kuna usawa, Sisi kama Watanzania kuna ulazima wa kurekebisha sheria ya ajabu kama hii na kuwa na usawa katika vyote
 
USANII MTUPU!....alikuwa wapi tangu alipoingia madarakani 2005 hadi hii leo miezi minane kabla ya uchaguzi ndiyo anaibuka na hii sheria!? Je, sheria hii ingetumika katika uchaguzi wa 2005 ambapo yeye na kundi lake la mtandao walitumia mabilioni kununua kura ili awe mgombea wa CCM wangepona!? Kwa maoni yangu hakuna jipya bali ni usani mtupu.
 
Hivi kuna mtu yeyote anayeamini kuwa anayosema JK ni kwa manufaa ya taifa au ni kwa faida yake binafsi?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom